Lissu shahidi mkuu rushwa ya Wabunge
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Spika Makinda, baada ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), kuomba mwongozo wa Spika mara baada ya matangazo ya wageni.
Ole Sendeka aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni 68 (7), ambayo pamoja na ibara ya 100 ya Katiba inaeleza kuhusiana na uhuru na utaratibu wa majadiliano bungeni.
“Nikitambua ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo bila kuathiri utaratibu na uhuru wa majadiliano katika Bunge na nikitambua ibara ndogo ya pili ya ibara ya 100 inayozuia au inayoweka kinga kwa Mbunge kushitakiwa ndani ya Mahakama ama katika mahali pengine popote katika jambo ambalo amesema ndani ya bungeni,” alisema na kuongeza:
“Pamoja na kutambua uhuru huu jana (juzi) mmoja wa Wabunge wenzentu Mheshimiwa Tundu Lissu alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuwashutumu baadhi ya Wabunge nikiwemo mimi mwenyewe kuhusishwa na kutetea baadhi ya makampuni anayoyadai kuwa yamekosa zabuni.
Nilichokiona ni kwamba kauli yake haikunitendea haki, nimesimama kuomba mwongozo wako kwa kauli aliyoitoa Mheshimiwa Spika, nje ya ukumbi kwamba ina kinga kwa mujibu ibara ya 100.”
Alisema kama kauli hiyo iliyotolewa katika ukumbi wa kambi ya upinzani juzi ina kinga, atapeleka hoja kwa Spika ili kwa kutumia mamlaka aliyopewa ya kanuni kupeleka katika kikao kinachohusika ili ukweli uweze kudhihirika.
Alisema hilo linatokana na maneno aliyotamka Lissu dhidi yake na Wabunge wenzake ambayo yamenidhalilisha kwa kuwa ni kauli ambayo haina chembe ya ukweli.
“Nitalazimika kama haina kinga kwenda mahakamani ili Mheshimiwa Tundu Lissu aweze kwenda kuyathibitisha haya mahakamani, haya aliyozungumza na waandishi wa habari. Kwa hiyo nimesimama hapa kuomba mwongozo wako kama hayo aliyoyafanya nje ya Bunge yana kinga,” alisema Sendeka na kuongeza kuwa:
“Na kama hayana kinga niweze kuchukua hatua ya kwenda mahakamani juu ya kauli ambayo ina lengo la kudhalilisha hadhi ya Bunge na kundi moja ndani ya Bunge ili hali akiomba uchunguzi ufanyike kwa Mbunge mmoja aliyemtaja ndani ya chama chake huku wengine akiwa tayari ameshatoa hukumu dhidi yao hata pale ambapo maneno hayana chembe ya ukweli.”
Akijibu Spika alisema: “Kwanza kabisa naomba Bunge hili liwe na subira kwa hili ambalo lilijitokeza siku ya Jumamosi na mimi nikalitolea uamuzi sijui kwanini mnapenda kulichafua chafua kila mahali.”
Spika aliwaomba Wabunge kuwa na subira wakati Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge aliyoipa kazi hiyo ikifanya uchunguzi kuhusiana na jambo hilo.
“Kuhusu yaliyosemwa jana (juzi), humu ni sehemu ya Bunge popote eneo linalohusu mipaka ya Bunge ni sehemu ya Bunge kwa hiyo basi kitu ambacho tunashukuru kwa Mheshimiwa Lissu kusema vile basi atakuwa ni msemaji wa kwanza kutoa ushahidi ndani ya Kamati ya Bunge ambayo nimeipa kazi hii. Kwa hiyo ataenda kwake na kusema hayo aliyoyasema jana. Na huko ndipo tutakapomsikiliza vizuri,” alisema Makinda.
Juzi Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), aliwataja Wabunge sita kuwa wana mgongano wa kimaslahi na Tanesco, kinyume na Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma.
NAPE AMVAA LISSU
Chama Cha Mapinduzi CCM kimeibuka na kuwakingia kifua Wabunge wake wanaotuhumiwa na rushwa katika sakata lililoibuka bungeni kuhusu tuhuma za baadhi ya wabunge kuhongwa.
Akizungumza na waandishi wahabari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alilaani Lissu kutoa orodha ya Wabunge wanaotuhumiwa kuwa na maslahi Tanesco.
Nape alisema anashangazwa na orodha hiyo yenye wabunge wa CCM pekee wanaotuhumiwa wakati wote wanajua kuwa yapo majina ya baadhi ya vyama vingine wanaohusika katika tuhuma hizo, kikiwemo Chadema.
“CCM tunalaani kwa nguvu zote juhudi zinazofanywa na baadhi ya wanasisa na vyama vya siasa katika kujaribu kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,” alisema Nape.
Alisema juhudi za Lissu na wenzake zinalenga kuuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa chama chake wanaohusishwa na tuhuma hizo na kuwataka kuacha mara moja njama hizo na kutoa nafasi kwa vyombo vinavyohusika kuchunguza na matokeo yake yatangazwe hadharani.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martin Shigela, amesikitishwa na wawakilishi wa wananchi kujihusisha na rushwa na kuampongeza Spika Makinda kwa hatua alizochukua za kuvunja Kamati ya Nishati na Madini.
Alisema watu na taasisi wanaojitokeza kutaja majina ya watuhumiwa wa rushwa ni vema wasaidiane na dola kwa kuwataja wanaohusika kwa kutoa taarifa kamili na sio kutafuta umaarufu ili umma wa Watanzania wawajue.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Dodoma na Leonce Zimbandu na Happy Kaiza, Dar.
No comments:
Post a Comment