Dk.Slaa ashangaa madai ya Nape
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwafundisha viongozi walio chini kuzungumza mambo yenye tija.
Dk. Slaa alisema ni kawaida ya mtu mwenye tabia mbaya kama vile mwizi kujishtukia na kufikiria kuwa hata wenzake pia ni wezi.
Dk. Slaa alisema hayo kwa nyakati tofauti wakati akihutubia mikutano ya hadhara ya chama hicho katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya Operesheni Vuguvugu la Mabadiliko ( M4C).
“Nataka nieleze suala moja, ambalo limetolewa kama tamko na kijana mmoja wa CCM anaitwa Nape. Sasa kwa sababu ni kama kinda la njiwa kwangu, sitamjibu yeye, lakini alichokisema kwa watu wanaojua, tunamshangaa Rais Kikwete kwa kuachia mambo ya chama chao na serikali yake kwa ujumla kujiendea au kuendeshwa hovyo hovyo namna hii.
“Namtaka Kikwete atuambie hayo maneno aliyosema Nape yana ruhusa yake au kaamua kujiropokea mwenyewe kama ilivyo kawaida yake huyo kijana.,” alisema.
“Kitendo cha Nape kuzungumza eti tunapewa ufadhili, mara eti tumeweka nchi rehani vinazidi kuivua nguo CCM na kudhihirisha kuwa serikali yake imeshindwa kuongoza tena,” alisema Dk. Slaa.
Alisema alichofanya Nape hakina tofauti yoyote na kauli aliyowahi kuitoa Katibu Mkuu wa CCM, Willson Mukama wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga kuwa Chadema kilikuwa kimeingiza nchini makomandoo kutoka nje ya nchi, zikiwemo Afghanistan, Israel, lakini alipotakiwa kuthibitisha baadaye alishindwa.
“Hizi sasa si propaganda tena, bali ni ujinga, ujinga ambao unaivua nguo serikali na chama hicho kuwa kimeshindwa, maana kama Chadema wanaweza kupokea fedha kutoka nje, wakaingiza fedha chafu ndani ya nchi, ikaingiza makomandoo kutoka nje ya nchi, serikali ya CCM ipo tu, haina ushahidi, wakati wana jeshi, wana Usalama wa Taifa, wana Uhamiaji wana Mahakama, basi serikali hii imeshindwa.
Juzi Nape alidai kuwa Chadema kinapokea fedha nyingi kutoka nje na kutaka kwaeleze wananchi wanakozipata.
No comments:
Post a Comment