Mkuu mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone akimkabidhi boksi la chakula cha msaada mwenyekiti wa kitongoji cha Kipamba, Agostino (mwenye shati jeupe).Chakula hicho kimetolewa ili jamii hiyo isiende porini kuwinda ibaki kwenye kaya zao kuhesabiwa.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Jamii ya Kihadzabe inayoishi katika kijiji cha Munguli kata ya Mwangeza jimbo la Iramba mashariki, imejitokeza kwa wingi kushiriki sensa ya watu na makazi iliyoanza Agosti 26 mwaka huu.
Jamii hiyo ilijitokeza baada ya ‘kupewa motisha ya msaada wa nyamapori ya kutosha na vyakula mbalimbali.
Jamii hiyo iliiomba serikali ya mkoa wa Singida nyamapori ya kutosha ili isiende porini kuwinda wakati wa sensa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone, amesema jamii hiyo ambayo chakula chake kikuu ni nyamapori, matunda pori, asali na mizizi ya miti pori, kabla ya kuanza kuhesabiwa, iligawiwa nyama ya nyumbu wakubwa watatu na nusu na mbuzi mmoja.
Amesema kitendo hicho kilisababisha jamii hiyo isiende kuwinda porini kama kawaida yao, ilibaki kwenye kaya zao kusubiri makarani wa sensa.
Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kusema kuwa iliwalazimu kuwakubalia ombi lao la msaada wa chakula na nyama pori ili wabaki kwenye kaya  na kambi zao, ili waweze kuhesabiwa.
Jamii hii ilibaki kwenye kaya zao na ilijibu kwa ufasaha mkubwa maswali yote iliyokuwa ikiulizwa na makarani.
Hata hivyo, kulijitokeza tatizo dogo la mawasiliano, kwa maana ya kuwa baadhi ya Wahadzabe hawajui kuongea Kiswahili, kwa hiyo walitafutwa wakalimani na walifanya kazi vizuri ya kutafsiri na hapo madodoso yalijibiwa ipasavyo.
Dk.Kone alisema pamoja na nyamapori hiyo, pia walitoa msaada wa magunia mawili ya unga wa mahindi na tani moja ya chakula kilichotolewa msaada na shirika lisilo la kiserikali la Outreach International Africa lenye makazi yake nchini Marekani.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa katika sehemu zingine za mkoa, mambo yamekwenda vizuri mno.
Kulikuwepo na mapungufu madogo madogo nayo yalirekebishwa bila kuleta athari yo yote.
Dkt. Kone ametumia fursa hiyo kuwashukuru wakazi wa mkoa wa Singida kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa ushirikiano wa dhati kwa makarani wa sensa.