KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 23 August 2012


Kagasheki awadhibiti wajumbe wa bodi



na Mwandishi wetu


KATIKA hatua za kupambana na ufisadi kwenye bodi mbalimbali zilizoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Balozi Khamis Kagasheki, amebadili utaratibu wa kuwapata wajumbe wa bodi hizo.
Taarifa ya Waziri Kagasheki, iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari na msemaji wa wizara hiyo, George Matiko, ilisema kuanzia sasa wajumbe wa bodi hizo watapatikana kwa njia ya ushindani badala ya kuteuliwa moja kwa moja na waziri.
Kwa sasa, kuna bodi nane ambazo muda wake umeisha au unakaribia kwisha, ambazo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri), Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori), Makumbusho ya Taifa na Chuo cha Mafunzo, Usimamizi wa Wanyamapori (Mweka), Chuo cha Mafunzo ya Wanyamapori Pasiansi, Wakala wa Mbegu za Miti (TTSA) na Bodi ya Leseni za Utalii (TTLB).
Kwa utaratibu huo mpya, Waziri Kagasheki, amewataka Watanzania wenye sifa za kuwa wajumbe wa bodi hizo kupeleka maombi kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo na kwamba maelezo zaidi ya namna ya kupeleka maombi yatawekwa kwenye magazeti na tovuti ya wizara ya www.mnrt.go.tz.
Agosti 13 mwaka huu, Waziri Kagasheki, alitangaza kuwatimua kazi vigogo watatu wa wizara hiyo akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori, baada ya kubainika kuhusika katika kashfa ya utoroshaji wanyamapori hai kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda nje.
Waziri Kagasheki alisema kuwa vigogo hao wamefukuzwa kazi baada ya tume iliyoundwa kuchunguza kadhia hiyo kufanya uchunguzi na kumaliza kazi yake.
Katika kashfa hiyo, vigogo hao wanadaiwa kuhusika na usafirishaji wa wanyamapori hai 116 na ndege 16, Novemba 24 mwaka 2010,  kwenda nje ya nchi kupitia KIA.
Aliwataja vigogo hao kuwa ni Obeid Mbangwa, Mkurugenzi wa Wanyamapori ambaye wakati wa kadhia hiyo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori.
Wengine ni Simon Charles Gwera, Ofisa Uwindaji wa Kitalii Cites na Utalii wa Picha – Arusha na Frank Mremi, Ofisa Uwindaji wa Kitalii Cites na Utalii wa Picha-Arusha.

No comments:

Post a Comment