KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday 31 August 2012

Dkt. Slaa aanika hadharani mazungumzo na mipango ya CHADEMA na Samuel Sitta (Mb)
Iringa -- Siku moja baada ya Waziri wa Afrika Mashariki na Mbunge wa jimbo la Urambo Mashariki, Samuel Sitta kumrushia kombora mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, katibu mkuu wa CHADEMA Dkt. Willbroad Slaa amemtuhumu Sitta na kumwita msaliti.

Dkt. Slaa amedai kuwa Sitta ndiye alikuwa katika makubaliano ya kuja kugombea Uspika kupitia CHADEMA ila alisaliti pamoja na kukubaliana vizuri kuwa angekihama chama chake CCM.

Dkt. Slaa alitoa tuhuma hizo leo (Ijumaa, Agosti 31, 2012) mjini Iringa alipozungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya M.R alisema ilikuwa Mei mwaka 2010, Sitta alikutana na viongozi wa CHADEMA na kuonesha dhamira ya kujitoa CCM na kujiunga na chama chao.

Dkt. Slaa alisema Sitta ni mmoja wa waanzilishi wa chama cha CCJ katika nchi hii wakiwa na Waziri wa Uchukuzi wa sasa, Dkt. Harrison Mwakyembe kwa lengo la kuhama CCM na kwamba waliandika katiba inayofanana na ya CHADEMA wakiwa na dhamira ya kujaribu upinzani huku wakisema wakishindwa watajiunga na CHADEMA.
Alisema kuwa katika mazungumzo hayo yaliyoendelea kufanywa katika kipindi chote cha bunge la bajeti lililokuwa la mwisho kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, katika masharti yake ya kujiunga na CHADEMA, Sitta ambaye kwa wakati huo alikuwa Spika, alitaka apewe nafasi ya kuwania urais kupitia chama hicho na vikao vilikuwa vikifanyika ofisini kwake Dodoma.

Alisema ameamua kutoa siri hiyo baada ya Sitta kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari juzi akidai kwamba Dkt. Slaa ndiye mtu pekee ndani ya CHADEMA ambaye ni tishio kwa Urais katika uchaguzi ujao, huku akimponda Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwamba ni mchezesha disco.

Alidai kushangazwa na Sitta kuanza kuzungumzia mambo ya watu badala yakujibu hoja. Dkt. Slaa akasema CHADEMA haipendi kuzungumza habari za watu bali maendeleo, "Kwa muda mrefu tumemhifadhi Sitta, lakini baada ya kupeleka mashambulizi sehemu isiyohusika sasa tunampiga ngumi za tumbo na uso" alisema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa akaendelea kusema kuwa, wakati akitaka aandaliwe mazingira ya kujiunga na CHADEMA na kupewa nafasi ya kuwania urais, Sitta alidai ana kundi la wabunge zaidi ya 55 waadilifu kutoka katika chama hicho ambao angetoka nao CCM na kuhamia CHADEMA kabla ya Bunge kuvunjwa.

Slaa akasema, kwa kuwa CHADEMA haina ubinafsi, ilihadi kuyafanyia kazi maombi yake ya kuwania Urais kwa uzito mkubwa, hata hivyo katika mazingira ya kushangaza, Sitta aliwatelekeza.

Dkt. Slaa alisema Sitta ambaye uzoefu wake katika siasa na umakini wake katika kushughulikia maendeleo ya nchi umeanza kuwatia shaka Watanzania, alisahau jinsi alivyowatelekeza kabla ya Uchaguzi Mkuu na baada ya uchaguzi huo akaja na hoja mpya kitaka CHADEMA wampe nafasi ya kuwania Uspika kwa kile alichodai kuwepo kwa mizengwe ndani ya CCM.

Dkt. Slaa akadai kuwa CCM walipobadili utaratibu na kumtaka mgombea Mwanamke yeye (Sitta) alichukizwa na suala hilo.

Lakini badala ya kufikia uamuzi wake wa kuhamia CHADEMA kama dhamira yake ilivyomtuma, Sitta aliwatelekeza tena akidai kwamba hatajiunga na chama hicho mpaka pale atakapokwenda jimboni kwake Urambo na kutangaza rasmi kujiondoa CCM.

Alisema Sitta aliyekuwa akitaka msaada wa viongozi wa CHADEMA ili afanikiwe kujiunga na chama hicho na hatimaye kupewa nafasi ya kuwania nyadhifa alizokuwa akitaka, ameanza kuwatusi hadharani viongozi hao akiwemo Menyekiti wake Mbowe.
Kwamba Mbowe ni mchezesha disco, Dkt. Slaa alisema kauli inayotolewa na Sitta inadhihirisha jinsi asivyo makini jambo linalowafanya waanze kuitilia shaka elimu na uzoefu alionao katika kuendesha shughuli za Serikali, “Sita anataka kutuambia kwamba watu wanaocheza disco wakiwemo Mawaziri wengi tu wanaokutwa kwenye kumbi za burudani wanatenda dhambi na ni uhalifu kufanya hivyo?” alihoji na kuendeleea, "...kama biashara ya Mbowe inafanywa kinyume na sheria za nchi, serikali inasubiri nini kufuta leseni yake?"

Kuhusu uongozi na namna ya kupata viongozi ndani ya chama hicho, Dkt. Slaa alisema sio kazi ya Sitta akuwapangia utaratibu,
“Sitta hajui kwamba duniani hakuna chuo cha kusomea Uwaziri, Ukatibu Mkuu na hajui kwamba Mwalimu Julius Nyerere hakuwa na uzoefu wakati akipewa madaraka ya kuongoza taifa hili na kwamba hata wasaidizi wake nao walipata uzoefu baada ya kupata madaraka,” alisema.

Alisema Sitta ni kiongozi mnafiki na atakumbukwa zaidi alipokuwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu kuna hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Wabunge wa upinzani kuhusu ufisadi alizizima. Alitolea mfano wa Sitta kuzuia muswada uliopelekwa Bungeni na Mh. Zito Kabwe (Mb, Kigoma Kaskazini - CHADEMA) unaohusu Ufisadi katika Makampuni ya umma, wakamfukuza Mh. Zitto kutoka Bungeni kwa kipindi cha miezi sita na kisha kumrudisha kimyakimya.

Alisema kuzimwa kwa hoja hizo ikiwemo ya Mkataba uliogubikwa na utata wa Kampuni za Meremeta, Buzwagi, unadhihirisha jinsi naye alivyotumia madaraka yake vibaya kwa kujenga ofisi ndogo ya Spika ambayo yeye aliita ya mbunge jimbo kwake Urambo.

Alisema wakati Serikali imeridhia Ofisi za Wabunge zijengwe kwa kiasi cha fedha kisichozidi Shilingi Milioni 40 kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha, ofisi hiyo ya Urambo ilijengwa kwa Shilingi Milioni 350, “Kauli zinazotolewa na Sitta kuhusu chama chetu zinadhihirisha jinsi alivyomnafiki na asivyofaa jambo lililosababisha hata CCM wamemnyima nafasi ya kuwania kugombea kwa mara nyingine tena nafasi ya Uspika,” alisema.
---

Picha na sehemu kubwa ya taarifa via Francis Godwin,
FrancisGodwin blog.


No comments:

Post a Comment