KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday, 15 November 2012


Taarifa Kwa Umma:- Tanzania Kutangaza Utalii Urusi

                                  JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
                                     WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

       Waziri Kagasheki akizungumza na Balozi wa Urusi Alexandr Rannikh


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Kagasheki amesema kuwa Tanzania imeandaa Mkakati wa kutangaza Utalii nchini Urusi.
Mhe. Kagasheki aliyasema hayo alipokutana na Balozi wa Urusi Bw. Alexandr Rannikh ofisini kwake leo.  Nia kubwa ya mkutano huo ilikuwa ni kuzungumzia namna ya kukuza Utalii nchini.

Waziri Kagasheki alisema Wizara imeandaa mkakati madhubuti wa kutangaza Utalii kwa nguvu zaidi ndani na nje ya nchi kwa lengo la kupata masoko mapya kama vile Urusi, China na Korea.  

Mkakati huo ambao umeandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) utazinduliwa leo katika Hoteli Serena Dar es Salaam.

Waziri Kagasheki alisema kuwa anayo hakika kuwa mkakati huo utafanikiwa kutokana na Tanzania kuwa na vivutio vya kutosha na kusisitiza kuwa ulimwenguni nchi inashika nafasi ya pili kwa kuwa na vivutio vingi na vizuri.

Waziri alisema kuwa kabla ya Kipindi cha Awamu ya Nne kumalizika atahakikisha kuwa anachukua hatua za kufanikisha Sekta ya Utalii nchini. 

Alisema, baadhi ya mambo atakayohakikisha kuwa yanafanyika ni kuongeza idadi ya vitanda vya kulala watalii, pamoja na kufanya mazungumzo na Mashirika ya ndege ili yaweze kufanya safari zao Tanzania.

Mhe. Kagasheki alisisitiza kuwa kuanzia sasa wawekezaji halali ambao watakuwa wanataka kujenga Hoteli katika maeneo ya Hifadhi, maombi yao yatashughulikiwa haraka iwezekanavyo kwa usimamizi wake mwenyewe.

Naye Balozi wa Urusi nchini Mhe. Alexandr Rannikh alisema kuwa amevutiwa na Tanzania inavyokuza demokrasia yake na kuwa Urusi itaendelea kushirikiana nayo katika masuala ya kukuza uchumi.

Kuhusu Utalii, Balozi Rannikh alisema amevipenda vivutio vya Utalii vilivyoko nchini na kusema kuwa kinachotakiwa sasa ni kuboresha utangazaji ili Warusi wavijue vivutio hivyo.
Kuhusu usafiri wa ndege, Balozi huyo alisema kuwa Tanzania inatakiwa ianzishe mazungumzo na mashirika ya ndege ya Urusi, kama vile Aeroflot, ili mashirika hayo yaandae safari ambapo ndege zao zitatua Tanzania. 

Aidha aliahidi kuisaidia Tanzania kuzungumza na wafanyabiashara wa Urusi ili waweze kuja Tanzania kuwekeza katika Sekta ya Utalii.

Balozi Rannikh alisema pia kuwa yuko tayari kuandaa mazungumzo kati ya Mawaziri husika wa Tanzania ili wazungumze na Mawaziri wenzao wa Urusi kuzungumzia uwekezaji.

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

No comments:

Post a Comment