KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday, 9 August 2012

Serikali inavifungia vyombo vya habari, lakini haitazuia midomo kujadili - Dkt. Slaa
09/08/2012

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, amefufua upya sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dkt. Steven Ulimboka, akitaka serikali ithibitishe hadharani mtu anayetajwa kuhusika na tukio hilo.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Ifakara, Morogoro jana, ikiwa ni sehemu ya Operesheni Sangara awamu ya pili, Dkt. Slaa aliyeambatana na viongozi wakuu wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, alisema kuwa Serikali ya CCM imekuwa na kiburi cha kuwatisha wanaotaka kutetea maslahi ya wananchi.

Alisema kuwa imefikia hata hatua ya wengine kutishiwa vifo, huku akitolea mfano wa kutekwa, kupigwa na kisha kuumizwa Dkt. Ulimboka, aliyetendewa unyama huo usiku wa kuamkia Juni 26 katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

“Serikali ina nguvu ya kuvifungia vyombo vya habari kwa sheria dhalimu ya magazeti ya mwaka 1977, lakini haitaweza kuzuia midomo ya watu kujadili suala zima la kutekwa huko kwa Dkt. Ulimboka,” alisema.

Dkt. Slaa ambaye alikuwa akishangiliwa kwa nguvu, aliongeza kuwa, kuanzia sasa CHADEMA itaanzisha mapambano kwa ajili ya kutaka kupata ukweli juu ya aliyemteka Dkt. Ulimboka.

Alisema kuwa miongoni mwa simu zilizowasiliana na Dkt. Ulimboka ni Ramadhan Ingondu, aliyetajwa kama mtu wa mwisho kabla ya kutekwa pamoja na namba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Mabwepande, aliyemtaja kwa jina la Abdallah Punja.

“Serikali na Usalama wa Taifa wanapaswa kusimama hadharani na kuuambia umma Ramadhan ni nani na kwanini anahusika na Idara ya Usalama wa Taifa.

“Mimi ni muumini wa Usalama wa Taifa na wala siwaondolei hadhi, lakini kwa mwendo huu ni wao wenyewe ndio wanajiondolea hadhi yao, na sasa wamekaa kufuatilia mikutano ya vyama vya siasa, hususan CHADEMA,” alisema Dkt. Slaa.

Endelea kusoma: TanzaniaDaima

No comments:

Post a Comment