Kwa nini tuamini kauli ya Nape Nnauye?
by Juvenalis Ngowi
MAMBO mengine kwenye hii kaya yetu unabaki ukishangaa tu. Ni jambo lililoko bayana kabisa kwamba mimi siwezi kupata afya njema kwa kuomba mtu mwingine augue.
Kama ninataka mimi kupata afya bora, kazi yangu na juhudi zangu zinapaswa kujitunza na kufuata mashauri ya wataalam.
Katika hali ya kushangaza, unapomsikia kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi, akisema kwamba CHADEMA wanapokea fedha kutoka nje kwa siri kutoka kwa wafadhili ili hao “wafadhili” waje kuifaidi Tanzania ni kiwango cha juu kabisa cha kushindwa kujua tatizo lililopo.
Kabla ya kujadili hiyo kauli na kuangalia matege yake, kwanza tujiulize kama bado kuna sababu yoyote ya kuamini kauli inayotoka Chama Cha Mapinduzi, hasa kwa wakati huu. Nitakumbusha kauli chache tu halafu tuone kama kwa kauli hizo, hii kauli dhidi ya CHADEMA inafaa kuaminika japo kidogo.
Wakati Chama Cha Wananchi (CUF) kilipokuwa na upinzani uliokuwa unafanya CCM watoke macho mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango, walizushiwa kila aina ya uchafu ikiwemo udini na hali ilipokuwa tete kabisa, propaganda kali zikapigwa kwamba kuna kontena la visu vyenye nembo ya chama hicho limeingizwa nchini.
Bila shaka, habari hii ililenga kuwaambia watanzania kwamba CUF sio chama makini wala watu wasijaribu hata kidogo kukiingiza madarakani.
Hadi leo, sijawahi kusikia huyo mwana-CUF aliyeingiza visu hivyo kwa nia ovu akikamatwa, akishtakiwa na kuhukumiwa.
Yawezekana porojo zile ziliyumbisha mwelekeo wa CUF, lakini ukweli ambao hauna mjadala ni kwamba, kuyumba kwa CUF hakukuifanya CCM iwe imara.
Badala ya kutumia muda mwingi kushambulia wapinzani wao, wangetumia muda kujijenga na kukijenga chama chao labda mambo yangekuwa afadhali.
Kama hadi leo hatujaoneshwa ushahidi wa hawa CUF na visu vyao, kwa nini tuamini haya yanayosemwa dhidi ya CHADEMA? Kalaghabao!
Ni Chama hiki cha Mapinduzi (CCM) kilichojiapiza kwamba kinawapa mafisadi miezi inayohesabika kwenye vidole vya kiganja cha mkono ili wajiondoe wenyewe, vinginevyo wangetimuliwa.
Tukaanza kusikia hadithi ya tunawapa mwezi mmoja, miezi miwili mara tunarudisha hili kwa wanachama.
Kauli yao wenyewe ya kuwaondoa mafisadi ndani ya chama, imedhihirika kwamba haitekelezeki na walichokisema kwamba wana nia ya kusafisha chama, kumbe ilikuwa porojo. Kwa nini tuwaamini sasa kwamba wanayosema dhidi ya CHADEMA yana ukweli?
Ni CCM hii hii ndiyo iliyokula yamini ya kutuletea maisha bora kwa kila mtanzania. Hivi hadi sasa tukichukulia katika wingi wetu, ni nani ameyaona hayo maisha bora?
Labda tuwaulize walimu na madaktari. Hivi hawa watanzania wanaokufa kwa ajali zinazoepukika, ndio wanaoishi maisha bora kwa kila mtanzania?
Hivi ni hawa watanzania wanaofanya kazi kwa amri za mahakama ndio wanaotekeleza sera za ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi (ANGUKA)? Kama utekelezaji wa ahadi za chama umekuwa na kigugumizi hivi, kwa nini tuamini haya mengine wanayoyasema? Mwenye macho haambiwi tazama.
Ni CCM hii hii katika kujaribu kughilibu umma, wakati wa mazishi ya mwasisi wa CHADEMA Bob Makani ilijaribu kuleta mzaha ndani ya kilio kwa kutaka kuwalisha watu uongo mchana wa jua la utosi eti Bob Makani ndiye alikuwa muasisi pekee wa CHADEMA asiyetoka Kaskazini. Mola mkubwa, waliokuwa wakifahamu historia wakatoa majibu pale pale, yakawashuka waliotaka kuleta siasa ndani ya kilio!
Kama waliweza kujaribu kupotosha umma kwa kiwango hicho cha kutisha, kwa nini leo hii tuwaamini wakizungumza mambo hasi dhidi ya CHADEMA?
Ni kada wa CCM aliyejaribu kusimama na kutaka kuwalaghai watanzania kwamba eti Dk. Wilbroad Slaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA, aliiba kanisani. Mungu wakati mwingine hujibu hapa hapa duniani. Maaskofu wakafungua mdomo na kusema huo wizi unaosemwa na kada wa CCM, haupo.
Uongo mwingine wa wazi wazi kabisa. Kimya kilichofuata hapo ni zaidi ya kile cha makaburini usiku wa manane.
Na mara nyingi tunashuhudia CCM wanavyodanda na kujidanganya wenyewe kuhusu kupendwa kwake. Wanapoitisha mkutano wa hadhara, hawana uthubutu wa kuwataka wanachama waende wenyewe kwa usafiri wao wenyewe.
Sikiliza, ukisikia kuna mkutano wa hadhara, tafuta wafanyabiashara wenye daladala wakueleze namna wanavyopata tenda ya kusomba watu na kuwapeleka mkutanoni.
Mitaani pia tunasikia tetesi kwamba kuna kuwepo pia posho za alfu moja moja kwa wahudhuriaji. Ndipo walipofika, na bado mnataka tuwaamini wakituambia wanayosema leo?
Tangu tusikie kwamba eti wanaachana na mpango wa kununua magari ya kifahari maarufu kama mashangingi, huu ni mwaka wa ngapi? Tunapishana nayo huku na kule utadhani kauli ile ya kutotumia magari hayo au ilitolewa nchi jirani, au wewe ndiye uko nchi jirani. Kimojawapo kati ya hivyo, maana kauli haziendani na macho yanayoshudia.
Hayo ni machache sana kati ya mengi ambayo yamesemwa, lakini hayakutekelezwa.
Kwa maana nyingine, ni kwamba CCM haina kauli thabiti na kwa mtazamo huo na historia yao, inakuwa mashaka sasa kuyaamini wayasemayo hasa dhidi ya wapinzania wao wakubwa.
Tukirudi kwenye hoja ya Nape Nnauye kwamba hawa CHADEMA wanapata ufadhili ili hao wakubwa kutoka nje, waje wafaidi rasilimali zetu, tuna maswali zaidi ya elfu moja na moja ya kuuliza. Hivi hadi sasa watu wa nje hawafaidi rasilimali za Tanzania?
Wale twiga waliosafirishwa kwenda nje walikuwa wanasafirishwa wakati wa utawala wa chama kipi? Ile ripoti ya wataalam kuhusu kodi tunayopoteza kwenye madini imesomwa na ndugu yetu Nape? Wanaofaidi unono wa misamaha na vivutio vya uwekezaji ni watu gani? Katika utwawala wa chama gani?
Walioleta wageni kuja kukusanya Ankara za umeme ni serikali ya wakina nani? Nadhani dada yangu Stella Manyanya atakuwa anakumbuka sana hilo sakata wakati ilibidi nguvu itumike kuruhusu wageni wachukue menejimenti ya shirika la umeme.
Ajabu ya Tanzania ni kwamba, mambo yanaenda kinyume nyume.
Yaani wakati ule tuliona hatuwezi kuwa na wataalamu wa kuendesha shirika, lakini tuna wataalamu wa kuendesha wizara!
Sijui kipi ni kigumu kuliko kingine. Tuna haja ya kuzungumza kwamba Tanzania sio muuzaji anayeongoza kwa kuuza tanzanite duniani? Tunahitaji kuzungumzia chochote kuhusu dhahabu? Tuna haja ya kuuliza mikataba tata ya kuzalisha na kuuzia TANESCO umeme?
Labda Nape aanze kutuambia CCM ililipwa kiasi gani hadi ikaua na kuzika Azimio la Arusha na kuumba Azimio lisilo rasmi la Zanzibar.
Tumalizie kwa kuhoji kidogo. Hivi inawezekana vipi, CCM kama chama kikafahamu mipango thabiti ya CHADEMA kupatiwa fedha kutoka nje kwa makusudi ya kuja kuwafaidisha wageni rasilimali zetu (utadhani sasa hivi hawazifaidi) halafu serikali ya chama hicho hicho ikashidnwa kujua mipango hiyo na kuizuia?
Hakuna sheria inayoelezea uchangiaji wa fedha kwa vyama vya siasa? Nani anapaswa kuisimamia? Lakini, hawa maasimu wetu wanaotaka kuja kufaidi maliasili zetu ni akina nani?
Bila majibu ya maswali haya, ni ngumu kuupokea ujumbe wa CCM kwamba CHADEMA wanapewa hela kwa hila ili maliasili zetu zije kufaidiwa na wageni.
Badala ya kusambaza propaganda ingekuwa vyema kujenga chama maana hata kama CHADEMA watachafuka na kuanguka, wananchi wamechoka, watatafuta mdabala mwingine.
via Tamzania daima
juvengowi@yahoo.com
No comments:
Post a Comment