KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday, 7 September 2012


Wavamia CBA, waiba mil. 300/-

na Betty Kangonga
WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi jana walivamia benki ya Commercial Bank of Afrika (CBA) iliyopo barabara ya Nyerere, Dar es Salaam na kuiba zaidi ya sh milioni 300.
Akizungumza na Tanzania Daima mmoja wa mashuhuda ambaye si msemaji wa benki hiyo, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 1:30 asubuhi bila ya kuwepo kwa purukushani za aina yoyote.
Alisema watu hao walifika katika eneo hilo wakiwa na magari na kuingia ndani ya benki hiyo.
“Inaonekana hawa watu walikuwa na mchoro kamili wa benki hii maana hawakufanya fujo zaidi ya kuingia ndani na kumkuta meneja na kisha kumtaja jina,” alisema.
Alisema baada ya kumwita walimwelekezea bastola kichwani na kutaka aoneshe zilipowekwa fedha.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kabla ya watu hao kufanya uhalifu huo waliharibu mfumo wa CCTV.
“Yaani hii ni kama picha, baada ya kumaliza shughuli hiyo waliingia katika magari yao na kutokomea… hata polisi walipofika na kuwasha CCTV hawakuambulia,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova, alisema kuwa jeshi hilo lilipata taarifa juu ya kutokea kwa tukio hilo majira ya saa 2:30.
Alisema kuwa, wapita njia hawakujua tukio lililokuwa likiendelea ndani ya benki hiyo kutokana na kutokea kimya kimya.
“Watu hao walimuita meneja wa tawi hilo ambaye alikuwa akiingia kazini kwa jina la Vick na kuingia… kumbe hatimaye meneja akawagundua kuwa ni wahalifu,” alisema.
Alisema kuwa, majambazi hao walimlazimisha meneja huyo, Victoria Munishi (47) pamoja na msaidizi wake, Baraka Sheshambo (40), kufungua mlango wa kuhifadhia fedha na chumba maalumu (strong room) kinachodhibiti mitambo maalumu ya kuzuia wizi.
Kamanda Kova, alisema kuwa mpaka sasa Jeshi la Polisi na makao makuu ya CBA wanashirikiana kujua kiasi kamili cha fedha zilizoibiwa ambazo ni shilingi za Kitanzania na fedha za kigeni.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa wahalifu hao walikaa kwenye benki hiyo kwa saa mbili bila taarifa hizo kufika Jeshi la Polisi wala makao makuu jambo ambalo sio la kawaida.
“Zipo dalili za kutosha kuwa kuna njama pamoja na ushirikiano kati ya wahalifu hao na baadhi ya watumishi wa benki hiyo, hivyo tunawashikilia meneja tawi, msaidizi na mlinzi wa zamu ya asubuhi,” alisema.
Kova alisema kuwa, mlinzi wa Security Group anashikiliwa kutokana na kutochukua hatua zozote pale alipogundua kuna mmoja wa wahalifu hao alivaa kitambulisho cha CBA wakati sio mtumishi wa benki hiyo.

No comments:

Post a Comment