KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday, 7 September 2012



Tendwa ababuliwa

NA MWANDISHI WETU

Makundi mbalimbali ya jamii yamesema kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, hana ubavu wa kukifuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwamba kauli aliyoitoa juzi ilikuwa ya jazba na ya kisiasa.

Wamesema kauli hiyo haina mashiko kwa sababu makosa ya jinai hayafanywi na taasisi bali watu binafsi.

Walisema suala hilo ni gumu kwa kuwa anapaswa kuangalia sera za chama na kwamba hadi sasa hakuna chama ambacho kina sera za mauaji ama uvunjifu wa amani.

DK. BANA: TENDWA ANATAKA KUWASHA MOTO 

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema si rahisi Tendwa kufuta Chadema, kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuzua moto mkubwa, ambao ni vigumu kuuzima.

Alisema kauli ya Tendwa ni ya kijazba na pia ni ya kisiasa, kwani ofisi yake haina uwezo wa kukifuta chama chochote cha siasa, kwa kuwa suala hilo ni la kisheria.

“Sijawahi kuona msajili anafuta chama chochote japo baadhi ya vyama vimekuwa vikikiuka sheria. Kwa hiyo, si rahisi msajili kufuta Chadema. Anataka kuzua moto, ambao huwezi kuuzima,” alisema Dk. Bana.

Alisema kwa mujibu wa sheria, chama kinatakiwa kifutwe iwapo kitakiuka sheria na kwamba, hatua hiyo itachukuliwa hadi hapo vyombo vya sheria vitakapothibitisha ukiukwaji wa sheria uliofanyika.

Hata hivyo, alivitaka vyama vya siasa kujenga maadili mema, ikiwa ni pamoja na kuheshimu mamlaka halali iliyopo.

DK. LWAITAMA: TENDWA ANACHEZA KARATA YA HATARI

Mhadhiri mstaafu wa UDSM, Dk. Azaveli Lwaitama, alisema kinachofanywa na Tendwa ni kucheza na karata, ambayo ni ya hatari.

Alisema kauli hiyo ya Tendwa haikuanza kutolewa naye, bali ilishatolewa kwa nyakati tofauti na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCC), Martin Shigela, na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Alisema kinachofanywa na Tendwa ni kurejea tu kauli za makada hao wa CCM na kufumbia macho matukio ya mauaji yaliyokwishafanywa hadharani katika mikoa ya Morogoro na Iringa na polisi na kuelekeza hasira zake kwa Chadema.

PROFESA SAFFAR: KAULI YA TENDWA NI NDOTO

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Abdallah Saffar, alisema kwa hali ilivyo hivi sasa nchini, utekelezaji wa kauli ya Tendwa ni ndoto.

Alisema Tendwa anapaswa kujifunza katika nchi kama Uingereza, ambako alisema hakuna mwenye ubavu kukifuta mfano Chama cha Labour cha na chama kingine chochote cha nchini humo na kusema anamshangaa sana Tendwa kuona akiitisha Chadema.

MREMA: TENDWA AMECHELEWA KUIFUTA CCM

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, alisema Tendwa amechelewa kutoa kauli kama hizo kwa kuwa chokochoko za uvunjifu wa amani nchini hazikuanza leo.

Alisema chokochoko hizo zilianza muda mrefu wakati baadhi ya viongozi wa CCM walipokuwa wakiwafanyia mabaya wapinzani, akiwamo yeye (Mrema).

“Mbona hakusema atafuta CCM? Tendwa ni mwongo, anabagua, hana lolote. Ni kweli ana ujasiri wa kufuta CCM aua anatishia nyau? Angeanza zamani. Lakini anakumbuka shuka asubuhi wakati kumekucha,” alisema Mrema.

WAKILI: NI VIGUMU KUFUTA VYAMA

Wakili Elias Machibya wa mjini Dodoma alisema kwa vyama, ambavyo vimekuwa na nafasi kubwa katika jamii, ni vigumu kuvifuta, kwani hata sheria yenyewe haimpi mamlaka ya moja kwa moja ya kufuta chama cha siasa.

“Jana (juzi) Tendwa ametoa kauli ya vitisho ambavyo ukiisikiliza sana hakusema chama fulani ndicho kinahusika na mauaji kwa kuwa suala la nani ni muuaji ni la kisheria zaidi na yeye si Mahakama,” alisema.

Alisema chama ni taasisi na kisheria hakiwezi kutenda kosa la jinai na ndiyo maana hata kama kushtaki hushtakiwa mtu na si chama.

Machibya alisema baada ya msajili kupokea majibu kutoka chama husika kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, kifungu namba 19, anatakiwa kumuandikia Waziri Mkuu ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kukifuta chama husika.

“Kama kuna mtu anavunja amani au anaua, huyo anapaswa kushughulikiwa kwa jina lake na siyo chama cha siasa,” alisema Machibya.

MHADHIRI: TENDWA HAJITENDEI HAKI

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Loisulie, alisema kauli iliyotolewa na Tendwa haimtendei haki yeye mwenyewe kama mwanasheria.

“Ukweli wa matukio ya mauaji anaufahamu mwenyewe, kwanini anazungukazunguka? Kinachotakiwa ni kutengeneza mazingira ya kukabiliana na matatizo na si kukifuta chama,” alisema na kuongeza:

“Kwanini kila tukio linapotokea wanapenda kukilaumu Chadema, kwanini isiwe CCM, mbona wao huwa wanaitisha mihadhara kipindi ambacho inakatazwa kufanywa hivyo mbona polisi hawaendi kuwazingira?”

ASKOFU: TENDWA ANACHOCHEA

Askofu wa Kanisa wa International Evangelism Sinai lililopo Ipagala Dodoma, Sylivester Thadei, alisema kauli ya Tendwa inaleta uchochezi kati ya wanachama na serikali.

“Ukizingatia huko nyuma mauaji yalishatokea, lakini hakutoa kauli kama hiyo kwanini leo atoe?” alihoji.

Mchungaji Samweli Maduma wa Kanisa la Anglikaana, alisema kauli aliyoitoa Tendwa ni vitisho na kinachotakiwa ni kulionya Jeshi la Polisi juu ya matumizi ya nguvu za dola.

SHEIKH WA MKOA: NI VITISHO

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajabu, alisema kauli ya Tendwa ni vitisho, ambavyo kwa hisia zake anaweza kupunguza matatizo yaliyopo hapa nchini.

“Nadhani Tendwa anaongea kwa ukali na hisia akiwa na mategemeo kuwa hiyo itakuwa suluhu ya kukomesha suluhu katika mikutano, lakini kumbe hali inaweza kuwa tofauti na vile anavyodhani,” alisema na kuongeza:

“Kwa mtazamo wangu sidhani kama polisi sheria inawaruhusu kutumia silaha za moto kumwajibisha mtu ambaye yuko mikono mitupu, hata vitabu vya dini mbalimbali haviruhusu mtu kutumia kitu chenye madhara makubwa kwa mwenzie.”

MENEJA: TENDWA AMEKURUPUKA

Meneja wa kampuni ya Faidika ya Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya, John Shashula, alisema Tendwa amekurupuka kutoa kauli hiyo, ambayo inajaribu kuufanya umma uamini kwamba Chadema ndiyo iliyohusika na mauaji ya watu kwenye mikutano yake, wakati tume zilizoundwa kuchunguza mauaji hayo mkoani Morogoro na Iringa zikiwa bado hazijatoa ripoti zake.

Alisema kutishia kufuta vyama vya siasa siyo suluhisho la tatizo hilo kwa kuwa hali halisi inaonyesha kwamba, mauaji kwenye mikutano ya vyama vya siasa hayafanywi na wafuasi wa vyama hivyo, bali ni askari wa Jeshi la Polisi ndio wanaonekana kuhusika.

Shashula alisema Tendwa ni sawa na baba wa vyama vya siasa, ambaye kama chama kimefanya makosa anapaswa kuwaita viongozi wake na kukishauri njia sahihi ya kupita badala ya kutoa vitisho vya kukifuta.

Alisema kwa msajili kufuta chama cha siasa ni sawa na kukwepa majukumu yake kwa kuwa ndiye mlezi anayepaswa kuzungumza na vyama na kuvielekeza njia sahihi ya kufanya mikutano na kuepuka mauaji kwenye shughuli za vyama.

‘TENDWA AMEJITUMBUKIZA KWENYE SIASA’

Mwanafunzi wa sheria wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu Huria Tanzania tawi la Mbeya, Eddo Mwamalala, alisema amesikitishwa na kauli ya Tendwa, ambayo inaonyesha wazi kuwa badala ya kuwa mlezi wa vyama vya siasa amejitumbukiza kushiriki siasa akitaka kuaminisha umma kuwa Chadema ndiyo inayoua watu kwenye mikutano yake.

Mwenyekiti wa Mtandao wa wasomi Mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo, alisema Tendwa alichokifanya ni kutoa vitisho, ambavyo haviwezi kusaidia kuboresha demokrasia nchini.

Alisema Tendwa alipaswa kutulia na kufanya uchunguzi wa chanzo cha mauaji kwenye mikutano ya vyama vya siasa ili apate fursa nzuri ya kuvishauri vyama cha kufanya badala ya kukimbilia kutoa vitisho vya kufuta vyama.

‘KAULI YA TENDWA INAWEZA KUTUMIWA VIBAYA’

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara na wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, alisema kauli ya Tendwa inaweza kutumiwa vibaya kwa kufutia vyama vingine usajili kwa maslahi ya kisiasa.

Alisema vyama vya siasa vinaundwa na vinaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu zinazofahamika, hivyo kauli hiyo inatia shaka kuwa ni kipimo gani kitatumika kujua kama chama ndicho kilihusika katika mauaji.

Alisema ili kupata ukweli wa tukio la mauaji, ni lazima kuwe na uchunguzi wa kina utakaohusisha vyombo mbalimbali na uchunguzi huo ndio utabainisha kama chama ndicho kilichoua au muhusika ni nani.

MCHUNGAJI: TENDWA HAJAFANYA UTAFITI

Mchungaji Julius Makorali, alisema kauli hiyo imetolewa bila kufanya utafiti kwani hakuna chama, ambacho kinaita mikutano na maandamano kwa ajili ya kupenda mauaji yatokee, bali huwa ni matokeo ya mikutano husika.

Wakili Method Kimomogoro wa jijini Arusha alisema anamshangaa Tendwa kwa kutoa kauli kama hiyo kwa kuwa chama hakiwezi kufanya vurugu, isipokuwa na viongozi maofisa, wanachama au wafuasi wake.

“Namkumbusha Tendwa ile kesi ya mauaji ya Shinyanga ya 1976 iliyomfanya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, (sasa Rais Mstaafu) alijiuzulu, walioshtakiwa kwa kusababisha mauaji ya watu wawili ni maofisa waandamizi wa Polisi na Usalama wa Taifa waliohusika katika utesaji na mauaji hayo,” alisema na kuongeza:

“Hivyo kama zinatokea vurugu kwenye mikutano ya siasa, lazima tume huru ichunguze kiini cha vurugu hizo badala ya Tendwa kuibuka na madai ya kufuta vyama, hata kama angekuwa na madaraka angewajibika kwanza kupata taarifa ya uchunguzi ijulikane kama chama hicho kimehusikaje.”

“Kwanza namshangaa sana Tendwa, akisoma sheria yake ataona kwamba hana mamlaka ya kufuta chama…Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258, kifungu cha 19 ndiyo inayompa mamlaka ya kufuta usajili wa chama, lakini imetoa sababu mbili.”

“Moja ni chama hicho kiwe kimekiuka masharti ya sheria hiyo au; kiwe kimepoteza sifa ya usajili ambazo zimetajwa kwenye sheria hiyo.”

Alisema suala la mauaji kutokea kwenye mikutano ya vyama au maandamano yaliyokatazwa na polisi hayo ni makosa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu au Sheria za Polisi za kushughulikia masuala mbalimbali na yanachunguzwa kuwa ni makosa ya jinai, hivyo ni lazima washtakiwe na kutiwa hatiani.

Alisema kwa mfano, haki ya kuandamano/kukusanyika ni ya Kikatiba, hivyo haiwezi kuminywa kivepesi kwa kisingizio cha sheria zingine na ndio maana viongozi wa mihimili yote wanaapa kulinda Katiba pamoja na haki za binadamu zilizoorodheshwa.

Wakili kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), mkoani Arusha, Shilinde Ngalula, alisema kauli ya Tendwa ni vitisho vyenye lengo la kuua demokrasia.

“Suala la kuwa na vyama vingi ni la Kikatiba na Tendwa hana mamlaka ya kufuta chama chochote…amethibitishaje Chadema inaleta vurugu?” alihoji.

Mwanasheria Mshauri wa Masuala ya Haki za Binadamu mkoani Morogoro, Aman Mwaipaja, alisema Tendwa anatoa kauli hiyo, huku akijisahau kuwa nchi hii hivi sasa inaendeshwa kwa mfuko wa vyama vingi vya kisiasa na kwamba, vyama hivyo ni lazima vifanye shughuli zake kila siku za kisiasa pasipo kuwekewa vikwazo na vyombo vya usalama.

Alisema shughuli hizo za kisiasa pia zimekuwa zikifanywa na chama tawala, lakini vyombo vya usalama kama Jeshi la Polisi halikiwekei kikwazo cha aina yoyote bali vikwazo hivyo vinawekewa vyama vya upinzani na kusababisha mauaji.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Viziwi Tanzania Mkoa wa Morogoro, Henry Mtasiwa, alisema kauli ya Tendwa ni ya uonevu na yenye lengo la kuvunja haki na uhuru wa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Naye Maliki Malupo, kutoka Chuo Kikuu cha Waislam mjini Morogoro, alisema kuwa anaunga mkono kauli ya Tendwa, lakini hofu yake ni utekelezaji iwapo itatokea chama tawala kimefanya mikutano na kutokea mauaji hayo.

DK. KITIMA:  TENDWA ANAVITISHA VYAMA

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk. Charles Kitima, alisema kauli ya Tendwa inalenga kuvitisha vyama vya upinzani ili vishindwe kuendesha shughuli zao kidemokrasia. 

Hivyo, akamtaka kufahamu kuwa anafanya kazi ya kulea vyama vya siasa kwa niaba ya wananchi na sio kwa niaba yake mwenyewe, hivyo hatua yoyote, ambayo itakuwa kinyume cha matakwa ya wananchi inaweza kusababisha machafuko.
 
MWANASHERIA: TENDWA ANATAKA KUBOMOA DEMOKRASIA

Mwanasheria na wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya Right Mark Attorneys ya Jijini Mwanza, Gasper Mwanalelya, alisema kauli ya Tendwa inalenga kubomoa zaidi misingi ya demokrasia. 

Mwanaharakati, Jimmy Luhende, alisema kauli hiyo ya Tendwa ni sawa na kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu.

Imeandikwa na Sharon Sauwa, Jacqueline Massano, Peter Mkwavila, Paul Mabeja, Dodoma; Ashton Balaigwa, Morogoro; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Salome Kitomari, Moshi; John Ngunge, Arusha; George Ramadhani, Mwanza na Muhibu Said, Dar.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment