KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 22 December 2011

CHADEMA WATOA TAMKO KUHUSU MAFURIKO JIJINI DAR ES SALAA



CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SALAAM ZA RAMBIRAMBI NA POLE KWA WANAFAMILIA NA WANANCHI KUHUSIANA NA
JANGA LA MAFURIKO YALIYOKUMBA JIJI LA DAR ES SALAAM, MBEYA NA DODOMA .
Usiku wa kuamkia tarehe 20.12.2011 Maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es
Salaam, Mbeya na Dodoma yamekumbwa na maafa makubwa ya mafuriko ambayo
yamesababishwa na mvua kubwa ambazo zimeendelea kunyesha mfululizo
katika maeneo hayo.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kutoa pole za
dhati kwa wanafamilia na wananchi wote ambao wamekumbwa na janga hili
kubwa , kwani limesababisha maafa makubwa sana ya vifo, kupoteza mali
na miundombinu mbalimbali kuharibiwa vibaya kwenye maeneo husika.
Tunapenda kuwahakikishia wananchi hawa kuwa tutakuwa nao pamoja katika
kipindi hiki kigumu katika maisha yao kutokana na madhara waliyopata
yaliyosababishwa na maafa haya.

Kutokana na janga hili limetukumbusha jambo moja kuwa kama Taifa
hatujajiandaa kikamilifu kuweza kukabiliana na majanga kama haya pindi
yanapotokea na hata vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeonyesha
dhahiri kuwa havijaandaliwa kimfumo na kinyenzo katika kuweza
kukabiliana na majanga kama haya na huu ni udhaifu mkubwa sana kwa
taifa lenye miaka 50 baada ya uhuru wake .

Mathalani mpaka sasa hatujaona jitihada zozote ambazo zimechukuliwa na
Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa katika kuonyesha juhudi za
kukabiliana na janga hili kubwa kwa taifa letu,hii inaonyesha wazi
kuwa kitengo hiki hakijaandaliwa kuweza kukabiliana na maafa kama
ambavyo majukumu yake yanavyopaswa kuwa . Na hii ni hatari kwani kama
chombo cha kukabiliana na maafa hakiwezi kufanya hivyo kwa wakati ni
kuendelea kuwaacha wananchi waendelee kupata madhara makubwa zaidi. Na
haswa ikizingatiwa kuwa idara ya hali ya hewa ilishatahadharisha
kuhusiana na mvua hizi.

CHADEMA tunapenda kuikumbusha serikali kuhusiana na ilani yetu ya
uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo ilieleza wazi kuhusiana na kukosekana
kwa mifumo thabiti ya kujulisha umma kuhusiana na majanga mbalimbali
katika miji yetu (Early Warning Systems) kama ambavyo ipo katika nchi
nyingi , mfumo huu ni muhimu sana katika kuweza kuufanya umma uwe na
elimu ya jinsi ya kuweza kujikinga na majanga haya kwa lengo la
kupunguza madhara yasiwe makubwa kama ambavyo taifa hivi sasa
linashuhudia.

CHADEMA inapendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa haraka na
serikali ili kuweza kukabiliana na majanga/maafa mbalimbali hapa
nchini yanapojitokeza;

I) Kuandaa mfumo wa awali wa kutahadharisha umma juu ya ujio wa
majanga (Early Warning Systems) kwa kutumia vyombo na nyenzo
mbalimbali ili kuepusha madhara makubwa kwa watu na mali zao.

II) Kutunga sheria mpya ya ujenzi na kuweka viwango vya ujenzi viwe
vyenye hadhi ya kimataifa na haswa ujenzi wa kuta mbalimbali na
majengo marefu na kuhakikisha kuwa ujenzi holela haujitokezi kwenye
miji na majiji yetu hapa nchini.

III) Kuhakikisha kuwa kwenye miji yote mikubwa mtandao wa mabomba ya
maji ya dharura unawekwa ili kuweza kukabiliana na majanga ya moto
pindi yanapotokea.

IV) Serikali ijiandae mara moja kukabiliana na magonjwa ya milipuko
kama vile kuhara ,kipindupindu na mengineyo ambayo yatajitokeza
kutokana na mafuriko haya kuharibu miundombinu ya kusambaza maji,
makazi ya watu n.k.

V) Kitengo cha maafa kiwe na vifaa wakati wote , na haswa vifaa kwa
ajili ya uokoaji na wawe na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma jinsi ya
kuweza kutumia vifaa hivyo kuweza kujiokoa na sio kuacha hali iwe kama
ambavyo imejionyesha Dar Es Salaam jana baada ya baadhi ya majaketi
okozi kufikishwa kwa wahanga na kushindwa kuyatumia kikamilifu.

VI) Serikali itoe elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa ya milipuko
kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko haya ili kuepusha wananchi wengi
kukumbwa na magonjwa hayo pindi yakijitokeza.

Mwisho tunapenda kuendelea kutoa pole kwa wanafamilia wote na wananchi
kwa ujumla kutokana na madhara makubwa waliyoyapata , Mungu awajaze
nguvu katika kipindi hiki kigumu.
Tamko hili limetolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu CHADEMA .

……………….

DR. Willbroad P. Slaa.

Katibu Mkuu –CHADEMA.


22/12/2011.

No comments:

Post a Comment