KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 22 December 2011

Ang’ang’ania mkia wa ng’ombe kujiokoa



Pamela Chilongola
SHARIFU Said mkazi wa Tabata Segerea wilayani Ilala, jana alitumia kila aina ya mbinu ikiwamo ya kushikilia mkia wa ng’ombe kwa ajili ya kunusuru maisha yake baada ya kusombwa na maji ya mto Msimbazi kutoka Segerea hadi Matumbi.Kufuatia kuchelewa kwa juhudi za  uokoaji, Said alilazimika kutumia kila aina ya mbinu kujiokoa ikiwamo mkia huo wa ng’ombe baada ya kusombwa na maji na kukaa zaidi ya saa tano.

Akisimulia tukio hilo, Said alisema mvua ilianza kunyesha mnamo  saa 11:00 asubuhi mara akaona maji yakiingia ndani ya nyumba yake, ndipo alipoanza kutoa baadhi ya vitu nje.
Said alisimulia kwamba, alipotoa baadhi ya vyombo alienda kwenye banda la ng’ombe na kukuta maji yameingia ndipo alipoamua kuwaokoa ng’ombe wake kwa kuwatoa ndani ya banda hilo.
“Nipo ndani mara nikaona maji yanaanza kuingia ndani ndipo nilianza kutoa baadhi ya vitu, wakati natoa mara nikasikia ng’ombe wangu wanalia nikaelekea kwenye banda nikakuta maji yameingia ndipo nikaanza kuwaokoa ng’ombe wangu,”alisema.

Wakati akiwa anawaokoa ng’ombe wake, alisema mara aliona  maji yakiwa mengi kama mto ndipo maji hayo yalipomsomba yeye mwenyewe, ng’ombe na baadhi ya vitu vyake.Said alisema alipelekwa na maji kusikojulikana ghafla yalimtupa eneo ambalo alikuwapo ng’ombe wake ndipo alipoukamata mkia wa ng’ombe.
“Nilimuomba Mungu anisaidie baadaye nilipoona maji yameshanishinda nilimuachia Mungu yeye ndiye muweza wa kila kitu, kama siku zangu zilikuwa zimewadia au kama zilikuwa bado yeye ndiye anayejua,”alisema na kuongeza:

“Nikiwa namuomba Mungu mara nikatupwa na maji kwa nguvu karibu na ng’ombe wangu, ndipo nilifanikiwa kumshika katika mkia wake.”
Alisema akiwa yeye na ng’ombe wake, walipita kwenye maeneo ambayo hayatambui wakati huo alikutana na vitu mbalimbali kama magodoro, sofa na ndoo.

Akiwa amemshikilia ng’ombe mkia,  mara alijigonga kwenye mti na kujikuta amemwachia ng’ombe huyo na kutupwa upande wa mti ndipo aliukamata mti huo zaidi ya nusu saa.
“Nilipokuwa nimeshika ule mti maji yaliongezeka zaidi na kujikuta ninaondoka na ule mti, nilijua hapa ndio mwisho wa maisha yangu,”alisimulia zaidi Said
Alisema akiwa haelewi anakokwenda akiwa mbali kabla hajafikia daraja la matumbi aliona magari yamepanga foleni barabarani alitamani kunyoosha mkono lakini alishindwa kutokana na wingi wa maji yaliyokuwapo.

Akiwa anapelekwa na maji eneo la daraja la Matumbi, aliona mti wa muarobaini ndipo alipoweza kuushikilia hadi walipotokea wasamalia wema na kumuokoa.

Waliomuokoa
Mwokoaji Abed Abdalla, alisema said baada ya kukaa katika mti huo zaidi ya saa tatu bila msaada wowote,  alikusanya vijana na kutafuta kamba ili waweze kumuokoa.Alisema baada ya kutafuta kamba ndipo aliamua kujitosa kwenda kumuokoa huku wengine wakiwa wameshikilia kamba hiyo, aliyokuwa amejifunga kiunoni ili aweze kumuokoa.
“Sisi kama wananchi tuliamua kujitolea kumuokoa mwenzetu, na tulipiga simu polisi, zima moto lakini hadi sasa hawajafika hii inaleta taswira  gani hatuoni maana ya Serikali,’’alisema Abdalla.

Hata hivyo, wakati Said akijiokoa kwa shida helikopta ya  polisi ilipita mara mbili eneo hilo bila msaada wowote mara ndipo wananchi wakaanza kulaumu kwamba badala ya kuokoa majeruhi kazi yao wanapita na kuondoka.“Tunasikia kuwa kazi ya helikopta ya  polisi ni kuokoa majeruhi, lakini tunashanga wanazunguuka katika eneo hili bila ya msaada wowote, wameonekana mara mbili,”walisema wananchi.

No comments:

Post a Comment