KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Tuesday 25 September 2012


Kamati Ya Maafa Ya Mkoa Wa Dsm Yakutana

Mkuu wa wilaya ya Temeke Bi. Sophia Mjema (kushoto) na mkuu wa wilaya ya Kinondoni Bw. Jordan Lugimbana wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikiwasilishwa kuhusu namna ya kukabiliana na maafa katika jiji la Dar es salaam leo wakati kamati ya maafa ya mkoa wa Dar es salaam ilipokutana
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki akiongea na na wajumbe wa kamati ya maafa ya mkoa wa Dar es salaam waliokutana leo  jijini Dar es salaam kujadili namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali yanayoweza kutokea na kusababisha  maafa katika jiji la Dar es salaam
Wajumbe wa kamati ya Maafa ya mkoa wa Dar es salaam 


Na: Aron Msigwa.
Serikali imewataka wananchi kutopuuza taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kuhusu athari za mvua kubwa zinazotarajia kunyesha nchini kuanzia mwezi Oktoba mpaka Desemba 2012 na kuwataka  wanaoishi mabondeni kuhama ili kuepuka madhara ya kukumbwa na mafuriko.
Hatua hiyo imekuja kufuatia baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni hususani  jijini  Dar es salaam kuupuuza taarifa za wataalam na kukaidi maagizo yanayotolewa na viongozi wa serikali ya kuwataka kuhama katika maeneo yenye mikondo ya maji na yale yaliyoainishwa kuwa hatari kwa maisha ya binadamu.
Akizungumza wakati wa kufungua  kikao cha kamati ya maafa ya mkoa wa Dar es salaam kilichowahusisha  wakuu wa wilaya za Temeke, Ilala, Kinondoni pamoja na wataalam wa sekta ya Afya, Jeshi la Polisi,  Kikosi cha Zimamoto na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na usalama ya mkoa leo jijini Dar es salaam mwenyekiti wa kikao hicho na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki amesema mkoa wa Dar es salaam unaendelea kujipanga kuhakisha kuwa wananchi wanapewa elimu ya namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali.
Amesema kamati ya maafa ya mkoa wa Dar es salaam imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa shughuli za uokoaji pindi majanga yanapotokea zinafanyika kwa ufanisi  na kuweka nguvu kubwa katika kuwasaidia wananchi kabla ya tatizo kutokea badala ya kujikita katika kuokoa wakati wa maafa.
Mwenyekiti  amezitaka manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni  kuhakikisha kuwa zinatenga maeneo mbadala kwa ajili ya kupeleka na kuhifadhi watu yanapotokea mafuriko na kuwataka kutotumia maeneo ya shule kwa ajili ya kuwahifadhi waathirika.
“Natoa agizo kwa viongozi wa manispaa kutenga maeneo mbadala ya kuhifadhi waathirika wa majanga mbalimbali ili shule ziendelee kutumika kama mahali pa watoto kujifunza, hata kama shule zimefungwa lazima tutafute maeneo mbadala haiwezekani tufunge shule wakati maeneo yapo ya kutosha”
Amesema kuna tabia ya  baadhi ya waathirika wanapopewa msaada wa kuhifadhia katika maeneo ya shule huyatumia kinyume cha utaratibu na wakati mwingine kuharibu miundombinu na wakati mwingine kugoma kuondoka na kukwamisha shughuli za uendeshaji wa shule.
Aidha ameitaka kamati ya maafa ya mkoa wa Dar es salaam kufuatilia mahitaji muhimu ya misaada yatakayokua yakitolewa wakati wa majanga ili kuwa na akiba na kuepuka usumbufu unaojitokeza wakati wa tatizo na kuziagiza halmashauri kupitia kwa wakurugenzi kutenga fedha kwa ajili ya kununulia vifaa vya uokoaji vitakavyotumika pindi yanapotokea majanga.  
‘’Lazima tuwe na ufahamu kutambua yatakayotokea kwa maana ya kujenga uwezo wa madawa, vifaa vya vya kisasa vya kuokolea yanapotokea mafuriko,kutenga maeneo maalum na vyumba vya kuuguzia wagonjwa waliopata madhara mbalimbali” amesema.
 Bw. Sadiki amewataka viongozi wote kuanzia ngazi ya mtaa kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kufanya usafi na kuzibua mifereji na kuepuka kutupa taka ovyo ili kurahisisha maji kutiririka kutoka eneo moja hadi jingine bila kikwazo chochote.
Kwa upande wake wake Dkt. Meshack Shimwela kutoka hospitali ya manispaa ya Ilala amefafanua kuwa kufuatia kuongezeka kwa majanga mbalimbali yanayotokana na vitu vya asili na vile vya kutengeneza imeundwa timu maalum ya kukabiliana na dharula (DAR MAERT).
Amesema utoaji wa huduma kwa waathirika wa majanga mbalimbali umekua ukikabiliwa na changamoto za ukosefu wa fedha, wataalam na vifaa vya kutosha hasa pale yanapotokea maafa makubwa.
Naye mganga mkuu wa hospitali ya Amana Dkt. Christopher Mzava akieleza kwa wajumbe kuhusu mkakati wa kukabiliana na mafuriko amesema kuwa suala la utupaji wa taka na uchafuzi wa mazingira limekua chanzo cha kuchangia kuziba kwa mifereji inayosafirisha maji kuelekea baharini hasa katika jiji la Dar es salaam.

Amesema licha ya changamoto za kukosekana kwa vifaa vya kutosha vya uokoaji zikiwemo ndege maalum (Helikopta) jamii inahitaji kuelimishwa kuhusu namna bora ya kukabiliana na kukwepa majanga.

Kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo mkoa wa Dar es salaam umeshuhudia majanga mbalimbali yakiwemo milipuko ya mabomu ya Mbagala iliyotokea mwaka 2009, milipuko ya mabomu ya Gongolamboto 2012 na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2011 na kusababisha upotevu wa maisha, mali na uharibifu wa miundombinu.

No comments:

Post a Comment