KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Saturday 21 July 2012

WABUNGE WASUSIA KIKAO NA KUTOKA NJE


BAADHI ya Wabunge wa upinzani bungeni wametoka nje ya kikao cha Bunge baada ya kutokea malumbano ya kikanuni ndani ya bunge kati ya Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema huku Mbunge huyo akidai kuwa ametukanwa.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya Lissu kuomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya 47(1) pamoja na kanuni ya 47 (3) za Kanuni za kudumu za Bunge akitaka kuomba idhini ya kuomba kutoa hoja kwamba bunge liahirishe shughuli kama zilivyoorodheshwa kwenye shughuli za Julai 20 ili kujadili jambo la dharura linalohusu ajali ya meli ya Mv Skagit. “Mheshimiwa Naibu Spika huu ni muda muafaka kujadili jambo hili kubwa badala ya kulipa likizo bunge ajali inatokea, alisema Lissu. Kwa kutumia kanuni ya 47(3) niliomba idhini yako Mheshimiwa Naibu Spika ili nitoe hoja,” alisema Lissu.

Lakini muda mfupi baadaye Mwanasheria mkuu wa serikali alisema Mbunge huyo wa Singida alitoa hoja ambayo haikuungwa mkono na wabunge kwa sababu hakuomba idhini, “Mheshimiwa Naibu Spika, sisi binadamu tuna vichwa na tunatumia vichwa hivyo kufikiri sio kufuga nywele. Sasa kuwa na nywele kichwani hakumaanishi kwamba unaweza kufikiri, alisema Werema. Kufuatia kali hiyo ya Mwanasheria mkuu wa serikali Lissu alisimama tena na kuomba utaratibu kutoka kwa Spika kuhusu matumizi ya lugha zisizo faa bungeni. Kanuni ya 64(1)f; mbunge hatamsema vibaya au kutoa lugha ya matusi kwa mbunge mwingine yeyote. Mheshimiwa Spika Mwanasheria Mkuu wa serikali anasema kwamba kuwa na nywele sio kuwa na uwezo wa kufikiri.

Lissu alisema kwa kauli hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina maana kwamba kuna wabunge ndani ya bunge ambao hawana uwezo wa kufikiri, “Mheshimiwa Naibu Spika haya ni matusi na ni mbaya matusi yanapotoka kwenye kinywa cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hoja halali ambayo imetolewa.Mimi nimeomba idhini ili nitoe hoja. Mwanasheria wa Serikali anasema nina nywele lakini sina uwezo wa kufikiri. Haya ni matusi Mheshimiwa Naibu Spika, alisisitiza Lissu.

Mapema pia Mbunge wa Ludewa(CCM) Deo filikunjombe akitumia kanuni ya 68(7) inayohusu jambo lililojiri wakati bunge likiendelea alisema tume zimekuwa zikundwa kila mara kuchunguza matukio ya ajali hususan za meli lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Kuhusu suala la Mv Spice Islander. Tumefika mahala sasa Mheshimiwa Naibu Spika Tanzania tunaunda tume nyingi, tume tunaunda na matokeo yake hatupewi na ukitazama wanaokufa wale ni watanzania wenzetu bila kujali meli ni ya Zanzibar au ni ya Bara,” alisema. Alisema hali imekuwa ikijirudia rudia tangu kutokea kwa ajali ya Mv Bukoba kisha Mv Spice Islander na sasa ajali ya Julai 18 ya Mv Skagit katika bahari ya Hindi. Tanzania tumekuwa ni taifa la kuombeleza, tunashusha bendera nusu mlingoti kila siku na mimi nasema, hata tukishusha bendera mpaka chini kabisa bila kuchukua hatua stahiki watanzania tutaendelea kufa", alisisiza Mbunge huyo.

Aidha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi alitaka bunge liache kujadili suala la ajali ya Mv Skagit kwa sababu kazi inayotiliwa mkazo sasa ni uokoaji, “Tusubiri tumalize kazi ile ya msingi ya ukozi na mazishi, tusubiri tume itakayoundwa na viongozi viongozi wakuu ambao kwa mujibu wa sheria ndio itatakiwa kufanya hivyo, badala ya ya kujadili hapa mjadala wetu ambao mimi nafikiri hautaweza kuwa na tija kwa sasa, alisema Lukuvi.

Akitoa maamuzi kuhusu mongozo aliioumba Mbunge, Lissu Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema mbunge huyo hakuomba idhini hivyo asingeweza kutoa hoja kabla ya idhini, “Kosa la Mheshimiwa hapa ni la kikanuni tu. Alichopaswa kufanya ni kuomba idhini ya kuomba kutoa hoja na hoja hiyo iungwe mkono na wabunge, alisema Ndugai.

Hadi sasa zaidi ya watu 62 wamethibitika kuwa wamekufa katika ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokewa karibu na Kisiwa cha Chumbe katika bahari ya Hindi wakati ikitoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar.


No comments:

Post a Comment