KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Wednesday 18 July 2012


Meli STAR GET ya Kampuni ya SEAGULL iliyokuwa na abiria 248 imezama leo eneo la Chumbe.
18/07/2012

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema meli ya STAR GET mali ya kampuni ya SEAGULL Transport Company imezama leo, katika kisiwa cha Chumbe, Zanzibar ilikuwa na abiria 248 wakiwemo watoto 31 na watalii 10.

Taarifa ya mamlaka hiyo hiyo imesema, meli hiyo, MV SKY GET iliondoka katika Bandari ya Dar es Salaam leo saa sita mchana, ikiwa na mabaharia tisa.

Taarifa nyingine (si za SUMATRA) zinasema sababu ya kupinduka kwa meli hiyo inadhaniwa kuwa ni kutokana na upepo mkali uliosababisha mawimbi kuipiga nakupindukia upande mmoja.

Inaelezwa kuwa abiria wengi wameokolewa kutokana na jitihada mbali mbali kupitia msaada wa boti za Mv Kilimanjaro, Tug ya Bandari na vyombo vingine. Waliojeruhiwa wanatibiwa katika Hospitali ya Mnazimmoja.

Kwa mujibu wa SUMATRA meli hiyo imesajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na kwamba, Cheti cha Ubora kimeanza tarehe 24 Agosti, 2011 na kinamalizika 23 Agosti, 2012. Imesema, meli hiyo ilikuwa imeruhusiwa kubeba abiria wanaoruhusiwa 300 na tani 26 za mizigo.

“SUMATRA kupitia Kituo cha Utafutaji na Uokoaji (MRCC) ilipata taarifa kuwa meli ya MV SKY GET iliyokuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar ilikuwa inazama katika eneo la karibu na kisiwa cha Chumbe, Zanzibar, eneo ambalo lipo umbali wa Kilomita za Bahari 13.8 kutoka Bandari ya Zanzibar” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Sumatra, baada ya kupata taarifa hizo, kituo cha MRCC kilitoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vyombo vya usafiri wa majini vilivyokuwa karibu na eneo la tukio.

“ Zoezi la uokoaji linaendelea katika eneo la tukio kwa msaada wa vyombo vifuatavyo: Mv Flying Horse, Mv Kilimanjaro III, Tug Bandari ya Zanzibar, KMKM, Mv Zanzibar I, Police Patrol Boat, Navy” imesema taarifa hiyo.

Inaripotiwa kuwa hadi sasa, watu zaidi ya 145 wameokolewa na miili ya maiti 16 imeopolewa.

Waziri wa Ulinzi Dkt. Emmanuel Nchimbi alisitisha kusoma hotuba ya Wizara yake kwa kutumia kanuni ya 58 kifungu cha 5 kuomba kutoa hoja iliyokuwa inaendelea, ili kujadili jambo jingine muhimu.

---
Taarifa via ZanziNews blog na gazeti la HabariLeo










Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, wa pili kulia) akiwa na Viongozi Wakuu wa Serikali alipofika katika Ofisi za Shirika la Bandari, Malindi Unguja kupata taarifa sahihi ya ajali ya kuzama kwa Meli hiyo. [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]



Askari Polisi Wanamaji wakiandaa kwenda kwenye ajali hiyo leo katika Bandari ya Dar es Salaam


Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Mwinyihaji Makame akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari.

Wananchi mbalimbali wakishuhudia tukio la kuokolewa watu waliozama na meli ya Star Gate.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiwa katika Eneo la Bandari akishuhudia kuletwa kwa majeruhi mbalimbali waliookolewa.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Amer Kificho pamoja na mawaziri mbalimbali wakiwa katika eneo la Bandari wakishuhudia kuletwa kwa majeruhi mbalimbali waliookolewa.

Mmoja wa majeruhi waliookolewa.

Majeruhi wakipatiwa Mablanketi kwa ajili ya kujihifadhi baada ya kuokolewa.


Watalii na raia wa kigeni pia walikuwemo katika meli iliyozama hawa ni baadhi ya waliosalimika



Abiria waliookolewa kutoka katika meli iliozama ya Star Gate katika bahari ya Chumbe Zanzibar

Abiria aliyeokoka kutoka katika meli iliyozama

Abiria aliyookoka katika Meli iliozama ya Star Gate akifarijiwa na Jamaa zake Baada ya kuteremka katika Meli iliowaokoa hapo Bandarini



Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamad akiwa katika hali ya huzuni Baada ya kushiriki katika uokoaji na kuwaona Majeruhiwaliookolewa katika Meli iliozama ya Star Gate wakiteremka hapo Bandarini Zanzibar.
Askari wa Vikosi mbalimbali wakiwa katika kazi ya Uokozi kwa Abiria waliokuwa katika Meli ya Star Gate ambayo iliozama katika ikiwa imebeba abiria 250 huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar
[Picha: Yussuf Simai - Maelezo]


TAARIFA YA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

KUHUSU

MAAFA YA KUZAMA KWA MELI ZANZIBAR


Meli ya Mv. Star Gate imezama karibu na Kisiwa cha Chumbe ambapo watu 12 wamefariki hadi muda huu na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Akitoa taarifa fupi kwa waandishi wa habari,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Mwinyihaji Makame Mwadini alisema taarifa za kuzama kwa meli hiyo ilitolewa na Boti iendayo kasi ya Kilimanjaro III iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar ndipo ilipoiona meli hiyo ikizama.

“Tulipata taarifa kutoka Boti ya abiria ya Kilimanjaro III saa 7:50 mchana waliporipoti kuona meli ikizama karibu na Kisiwa cha Chumbe” Alisema Waziri Mwinyihaji.

Waziri huyo alisema Meli hiyo imezama maili sita kuelekea Kisiwa cha Yasin Kusini mwa Kisiwa cha Chumbe kilichopo Unguja maili kadhaa kutoka Bandari ya Malindi.

Waziri Mwinyihaji alisema idadi ya abiria walikuwa 250 ambao ni watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6. “Tumepeleka waokoaji, kuna boti tano zipo eneo la tukio kushirikiana na waokoaji wengine” Alisema Waziri Mwinyihaji.

Alisema maiti zote zitapelekwa viwanja vya Maisara Zanzibar kwa ajili ya ndugu na jamaa kuzitambua maiti za ndugu zao ambapo majeruhiwa wote watatibiwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.

Katika Bandari ya Malindi mwandishi wetu ameshuhudia maiti kadhaa zikiwemo za watoto zikishushwa, Miongoni mwa abiria waliookolewa ni raia 13 wa Mataifa mbalimbali ya nje huku raia mmoja ambaye hakuweza kutambuliwa utaifa wake amepoteza maisha.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alifika eneo la Bandari ya Malindi Zanzibar pamoja viongozi wengine akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Mawaziri na baadhi ya Wajumbe a Baraza la Wawakilishi walikuwepo kutoa msaada unaohitajika.

Katika eneo la pembezoni mwa bandari ya Malindi, makundi ya wananchi yalikuwa yamekusanyika wakisubiri taarifa za tukio hilo tangu saa 8:30 mchana.

Vikosi vya ulinzi na usalama, msalaba mwekundu na watoaji wengine wa misaada ya dharura walifika kwa haraka eneo la tukio.

Hadi sasa kazi ya uokoaji inaendelea karibu na Kisiwa cha Yasin ilikozama meli hiyo.

Meli ya Mv. Star Gate inamilikiwa na kampuni ya kizalendo ya Sea Gull Sea Transport Ltd ambayo mwaka 2009 Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilipinduka na kuzama katika Bandari ya Malindi Zanzibar na kua watu sita.

Mwaka jana Zanzibar ilikumbwa na maafa baada ya Meli ya Mv. Spice Islanders kuzama katika bahari ya Hindi eneo la Nungwi katika Kisiwa cha Unguja ikielekea Kisiwani Pemba ambapo taarifa rasmi ya Serikali ilisema watu 197 walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.

Taarifa zaidi zitatolewa hapo baadaye.

Imetolewa na:

Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzíbar
Julai 18, 2012

Zanzíbar,Tanzania.


Baadhi ya abiria ambayo wameokolewa katika meli inayomilikiwa na Seagull iliyobiruka katika eneo la bahari karibu na Chumbe (picha via ZanzibarYetu.wordpress.com

Mmoja wa Majeruhi akipata huduma ya kwanza baada ya kuokolewa

Daktari akitowa huduma ya kwanza kwa mmoja wa majeruhi










Majeruhi wa ajali ya Meli wakiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja wakipata huduma baada ya kuokolewa

Majeruhi wakiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja








Mwokoaji akiwa na mmoja wa maiti wa ajali hiyo

Waokoaji wakiokoa moja ya maiti wakiwa katika boti ya Kilimanjaro.

Majeruhi wakiwa katika mgongo wa boti hiyo wakisubiri kuokolewa

Baadhi ya Abiria wakiwa katika moja ya combo cha kuokolea wakielea baharini wakisubiri kuokolewa.

Boti ya KMKM ikiwa katika zoezi la kuokowa majeruhi.

Helikopta ya Jeshi la Polisi ikiwa eneo la tukio.

Boti iliyozama ni kama hii, ni ni pacha wake.

Boti ya Fly ikiondoka katika bandari ya Zanzibar kueleke kutowa msaada wa uokozi.


Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu Hamad Masoud akiwa katika boti ya Kilimanjaro akiwa sehemu ya tukio ilikozama boti.

Tagi la Shirika la Bandari likiwa katika sehemu ya tukio.







No comments:

Post a Comment