KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday, 5 October 2012


Haruna Moshi Aomba Radhi Kwa Kumchezea Rafu Beki Wa Yanga

 

Na: Majuto Omary, MWANANCHI

 KIUNGO wa Simba, Haruna Moshi ameomba radhi kwa kumchezea rafu beki wa Yanga, Kelvin Yondani itakayomfanya akae nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki mbili. Moshi alimkanyaga Yondani juu ya goti kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliozikutanisha Yanga na Simba Jumatano usiku na kumalizika kwa sare 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Akizungumza na Mwananchi, Moshi maarufu kwa jina la 'Boban' alisema kuwa anajisikia vibaya sana kwani hakudhamiria na kilichotokea ni bahati mbaya. Boban alisema kuwa Yondani ni rafiki yake wa karibu sana na kilichotokea hata yeye hakujua matokeo yake. ìMimi nimekosea, lakini sikujua kwani ule mpira ulikuwa fifty fiftyí, nilikuwa nauwahi na Yondani alikuwa anauwahi ili kuokoa, matokeo yake ndiyo hayo, nilivyoosha mguu ili kuuchukua mpira, bahati mbaya Yondani naye akawa amefika, nasikitika sana kwa yale yaliyotokea,î alisema Moshi. 

Alisema kuwa baada ya Yondani kutolewa nje na kushindwa kuendelea na mchezo, alijutia kile kilichotokea na hasa ukaribu wake na mchezaji huyo kwa miaka mingi, tangu akiwa Simba na sasa baada ya kuhamia Yanga. ìNaomba radhi kwa Yondani, familia yake, wachezaji wa Yanga, viongozi wa timu hiyo, benchi la ufundi na wadau wa soka kwa ujumla, sikujua nilichokifanya kwani nilikuwa katika majukumu ya klabu wala sikutegemea kitu kama kile kutokea,î alisema Moshi kwa masikitiko makubwa. Alisema kuwa atajitahidi kukutana na Yondani ili kumjulia hali yake kwani mbali ya upinzani wa uwanjani, wao ni marafiki wa siku nyingi sana. Boban aliwaomba mashabiki wa Yanga wasichukulie tofauti suala hilo kwani hata yeye mpaka sasa linamuumiza sana. 

Naye Daktari wa Yanga, Juma Sufiani alisema kuwa Yondani amepata ufa (fracture) katika mfupa wake wa mguu wa kulia na kuchana ligament, hali ambayo imemfanya awe katika hali mbaya na atakaa nje kwa muda wa wiki mbili bila ya kufanya mazoezi. Sufiani alisema kuwa muda wa wiki mbili ni wa muda wa awali tu, lakini kwa hali ilivyo, inawezekana kabisa akaongezewa muda kutokana na kasi yake ya kupata nafuu. Alisema kuwa pamoja na kukaa nje, pia anahitaji kupata uangalizi wa karibu sana na ushauri huo umetolewa na madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 

Ni pigo na anahitaji uangalizi wa karibu sana, kwa sababu rafu ilikuwa mbaya, lakini ni hali ya kawaida kwa wachezaji, hajavunjika ila maumivu yake ni sawa na mtu aliyevunjika, kupata fracture na kuchana ëligamentí ni kati ya magonjwa makubwa sana katika mpira wa miguu,î alisema Sufiani. Wakati huohuo; Jumla ya mashabiki 50,455 walishuhudia pambano hilo na kuingiza sh 390,568,000, huku Yanga na Simba kila moja ikiambulia sh 93.3 milioni.

 Watazamaji 50,455 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa usiku kwa viingilio vya sh 5,000, sh 7,000, sh 10,000, sh 15,000, sh 20,000 na sh 30,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh 93,345,549.15 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh 59,578,169.49. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh 240,000, kamishna wa mechi sh 250,000, waamuzi sh 591,000, mwamuzi wa akiba (reserve referee) sh 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh 2,000,000. Umeme sh 750,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh 400,000, ulinzi wa mechi sh 5,860,000 wakati tiketi ni sh 7,327,000. Gharama za mchezo sh 31,115,183.05, uwanja sh 31,115,183.05, Kamati ya Ligi sh 31,115,183.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh 18,669,109.83 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh 12,446,073.22.

 Wakati huo huo, mechi ya ligi hiyo kati ya African Lyon na Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ilishuhudiwa na mashabiki tisa kwa kiingilio cha sh 3,000 na kuingiza sh 27,000. Mgawo wa mechi hiyo ulikuwa VAT sh 4,118.6 wakati kila timu ilipata sh 6,864.3. Uwanja sh 2,288.1, gharama za mchezo sh 2,288.1, Kamati ya Ligi sh 2,288.1, FDF sh 1,372.8 na DRFA sh 915.2.

No comments:

Post a Comment