KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Tuesday 22 May 2012


Tunaiamini CHADEMA tunayoifahamu!

         na Samson Mwigamba

WASOMAJI wapendwa, nawashukuru wote walionipigia simu, walionitumia barua pepe na walionitumia ujumbe mfupi wa simu. Na natambua kuna wengi walitamani kuwasiliana nami ila basi hali ya kiuchumi ama ya kimazingira haikuruhusu. Nawashukuru wote hata wale ambao hatukuwasiliana. Lakini barua pepe niliyoipokea kutoka kwa Dk. Lupembe ilinishangaza sana! Dk. alinitumia kwanza ujumbe mfupi wa simu kunitaarifu kwamba atanitumia hiyo barua pepe na kweli baadaye akanitumia. Nilipofungua kuusoma nilikuta ameandika hivi:
“Ndugu Mwenyekiti-CHADEMA, Arusha: Mheshimiwa Samson Mwigamba. Kwanza nikushukuru kwa kuitumia sehemu kubwa ya e-mail yangu kama msingi mkuu wa "kalamu ya Mwigamba"-16.05.2012 (Tanzania Daima).
Nimeisoma makala nzima neno kwa neno, kifungu kwa kifungu, aya kwa aya. Mwenyekiti, niharakishe kusema kwamba, mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa, maoni yangu ambayo nimekuwa nikiyatoa mara kwa mara, ni mtazamo wangu binafsi kutokana na mapenzi mema kwa nchi yangu. Nirejee sasa katika makala yako-waraka maalum kwa vijana wa nchi hii (Tanzania): Kichwa cha makala yako ni "exclusive" , umewa-alert vijana pekee na si watanzania wote kwa ujumla wao, suala la kuleta mageuzi, mabadiliko na maendeleo ni jukumu la watanzania wote wa rika na jinsia zote. Mwenyekiti, siijui kabisa na hata baada ya kutafiti nimeshindwa kuielewa falsafa na itikadi ya CHADEMA, inaonekana ni chama kisichokuwa na itikadi wala falsafa inayoeleweka waziwazi!
Kitu pekee kinachoitambulisha CHADEMA mbele ya watanzania ni kampeni yake ya kufichua na kupinga ufisadi na mafisadi! Jambo kubwa na la msingi ambalo nilitarajia ungeli-highlight intesively, ni hii tendency ya watanzania ya kupuuzia kujiandikisha kupiga kura, kutunza shahada zao, na hatimaye kupiga kura wakati unapowadia.
Wengi wa watanzania hawajiandikishi kupiga kura, na mara baada ya uchaguzi kupita wanaanza kulalamika na kulia kama watoto wadogo! Hili ndilo suala ambalo nilidhani lingebeba makala nzima. Mwenyekiti, what matters most ni kuwa benet na wapiga kura! Na hapa ndipo CCM inapowapiga bao, CCM inawajua wapiga kura wa uhakika walipo na inakuwa nao benet muda wote.
Haina maana saana kuwa na watu waliotayari kunyeshewa mvua au hata kushinda na kukesha wakiwa na njaa, iwapo watu hao hawatajiandikisha kupiga kura! Na hapa ndipo ile assumption yangu ya "deception" ndipo inapodhihirika. Ndugu Mwigamba, bado siioni genuine desire ya CHADEMA kushika dola, ziko sababu chache zinazonifanya niwe na wasiwasi na dhamira yenu… Nimalizie kwa kusema kwamba, chama makini hujipanga na kujijenga vilivyo kama kweli kina nia ya dhati ya kushinda uchaguzi mkuu na kuongoza dola. CHADEMA bado mnafanya mchezo mchezo. Dk. Lupembe”.
Nawaomba radhi sana wasomaji wangu! Nimeshindwa kuvumilia maelezo haya ya Dk. Lupembe kiasi cha kuamua kutumia makala ya leo kama maelezo yangu ya mwisho kwa msomi huyu wa PhD na kama hatatuelewa basi. Kama atatuelewa, naamini kuna watu wengi ambao wako chini yake ama wanaomwamini ambao atawaelewesha pia na watajiunga kwenye mapambano.
Kwanza kabisa nimemshangaa! Kwa wasomaji waliosoma ujumbe wa Dk. Lupembe kwenye makala yangu iliyopita, watakubaliana nami kwamba Suala la msingi lilikuwa ni elimu na utayari wa Watanzania kubadilika na ndiyo nikatoa wito kwa vijana kupambana kueneza elimu ya uraia na wito wa mabadiliko kwa kila Mtanzania. Simwelewi leo anazungumza nini.
Halafu anahoji suala la kuwaandikia vijana. Hivi leo nikimuandikia mzee wa miaka 60 yale niliyoyaandika kwenye makala ile atayafanyia kazi kweli? Nimewaandikia vijana wa kike na wa kiume kwa sababu ile kazi ninayosema ifanyike inaweza kufanywa na vijana. Na historia ni shahidi kwamba mageuzi yoyote yawe ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni na hata kidini, huletwa na vijana.
Hakuna mahali ambapo utategemea mageuzi yaletwe na akina Dk. Lupembe (sijui kama wewe ni mzee Dk. lakini maneno yako yanafanana sana na ya wazee kama akina Kingunge, Malecela, Msekwa, na wengineo ambao bado wanaota kwamba CCM kuondoka madarakani ni miaka 50n ijayo).
Nitawaandikia hao wa nini? Nazungumza na vijana ili waeneze taratibu kila mtu kwa njia yake lakini hatimaye nuru ya mabadiliko iwafikie wazee wanaume kwa wanawake tufanye mabadiliko. Suala la kujiandikisha kupiga kura ni rahisi kwa mtu aliyekwishapata nuru ya mabadiliko lakini pia nilisema kwenye hizo makala mbili kwamba wakati wa kujiandikisha ukifika tutafanya kampeni kubwa kuwahimiza wajiandikishe na kutunza shahada za kupigia kura. Kwa mtu ambaye elimu ya uraia na nuru ya mabadiliko haijamwangazia utakuwa unampigia mbuzi gitaa kama utamsisitizia tu kujiandikisha na kupiga kura. Kwamba CCM iko karibu na wapiga kura kuliko CHADEMA na ndiyo maana inakipiku chama hicho. Mbona haijakipiku Arumeru mashariki. Mbona Igunga ambako tuliingia bila hata kura moja ya ubunge tulikaribia kuwaangusha?
Kilichoniuma zaidi kwenye email yako Dk. Lupembe ni kusema kwamba, “… hata baada ya kutafiti nimeshindwa kuielewa falsafa na itikadi ya CHADEMA, inaonekana ni chama kisichokuwa na itikadi wala falsafa inayoeleweka waziwazi”. Dk. hebu tujuze huo utafiti umefanya wapi? Soma maneno haya machache yaliyo kwenye tovuti ya CHADEMA (www.chadema.or.tz) kwenye sehemu inayosema: “Ijue CHADEMA” imeandikwa hivi:
“Agosti 13, 2006, Chama cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA kilifanya uzinduzi mpya wa chama, uzinduzi ambao ulikuwa na lengo la kubainisha mikakati na Programu mbalimbali za utekelezaji kuelekea uchaguzi wa mwaka 2010, kwa lengo la kujipanga na kujijenga upya ili kuwaletea Watanzania Matumaini, Imani na Mwelekeo katika medani za uchumi, siasa na kijamii.
CHADEMA kilijipanga upya kwa maana ya kubadilisha mfumo na muundo wake, kilifanya mabadiliko ya katiba na kanuni ili viende sambamba na mahitaji na mazingira ya sasa ambapo CHADEMA imedhamiria kujipanua zaidi kuanzia ngazi ya msingi mpaka taifa.
Kwa upande mwingine CHADEMA kimeendelea kujipanga kuwa sauti ya wasio na sauti kuwatetea, kuendeleza na kutekeleza Mabadiliko ya Kweli na Uhuru wa Kweli. Chama kimedhamiria kusimamia uwajibikaji wa serikali na kuishinikiza kutekeleza ahadi ilizozitoa. Kitaendelea kuwa chenye mtizamo chanya na wenye kujenga katika kuiwajibisha serikali. Na kitakuwa na watu wa fikra, wenye nafsi wazi (open mind) na nishati katika kuibua mawazo na kutengeneza sera tunazohitaji kukabiliana na changamoto hususan za muda mrefu ambazo nchi yetu inakabiliana nazo. CHADEMA kinaendelea kuwa moja ya vyanzo vya imani, matumaini na mwelekeo wa taifa letu.
Tunafanya hivi kujenga chama imara na makini zaidi ili kuongeza ufanisi katika ushindani wa demokrasia ya vyama vingi. Tulizindua mchakato wa kwanza unaohusisha zaidi mabadiliko ya kimuundo na zana na baadaye mchakato wa maboresho ya kisera na uongozi. Tulizindua alama na zana sita za CHADEMA. Ndani ya alama na zana hizi upo ujumbe mahususi kwa Wana CHADEMA na Watanzania. Alama na zana hizi ni ishara tu ya imani, matumaini na mwelekeo wetu kwa mustakabali wa chama na taifa letu. Tunatazama mbali, tukiwa na imani, matumaini na mwelekeo.
Miongoni mwa mambo yaliyozinduliwa ni pamoja na: Chama kuwa na bendera mpya na kadi mpya zenye rangi nne: bluu, nyekundu, nyeupe na Nyeusi; Uzinduzi rasmi wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa CHADEMA kuanzia mwaka 2006 mpaka 2010.
Mpango huo umedhamiria kukiendesha na kukijenga kama “chama taasisi” na si “chama uchaguzi”; Mfumo na muundo mpya wa chama uliojikita zaidi katika kuhakikisha na kutambua nguvu za makundi maalumu ya kijamii, kama vijana, wanawake, wazee na walemavu; Wimbo rasmi wa chama unaoimbwa kote nchini, ni sauti ya CHADEMA. Ni njia ya kutumia sanaa kuwasilisha hisia, misimamo, hamasa, matamanio na matarajio yetu; Kaulimbiu ya uzinduzi mpya wa CHADEMA ni CHADEMA; TUMAINI JIPYA! Hii ni kauli mbiu inayobeba dhana nzima ya “imani, matumaini na mwelekeo”. Tumaini jipya ni Imani, Ni matumaini, Ni mwelekeo!
CHADEMA tunaamini kuwa Watanzania wengi wamepoteza imani ya kupata maendeleo kupitia serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi CCM, Wamekata tamaa kwa sababu waliopo madarakani kwa takriban nusu karne wameshindwa kuleta mabadiliko ya kweli na mbaya zaidi wamedhamiria kubaki madarakani kwa gharama yoyote. Wamedhamiria kubaki madarakani kwa gharama ya umaskini wa Watanzania.
Falsafa ya chama
Falsafa ni fikra na mtazamo wa chama ambayo ni kuamini katika “Nguvu na Mamlaka ya Umma” (The People’s Power) katika kumiliki, kuendesha, kubuni, na kuendeleza maamuzi, mawazo, rasilimali, uchumi na siasa ya nchi yao.
Aidha falsafa ya “Nguvu na Mamlaka ya Umma” ndiyo msingi na chimbuko la kuundwa dola ya nchi, na kuwa, umma ndiyo wenye madaraka ya mwanzo na ya mwisho katika kuamua hatima ya nchi na taifa pasipo kuingiliwa, kudanganywa au kughilibiwa na viongozi, watawala au wageni.
Itikadi ya Chama
CHADEMA ni chama cha itikadi ya mrengo wa kati (center party). CHADEMA ni chama kinachoamini kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali za nchi yetu bila kuathiri uhuru wa taifa, na kuhakikisha kuwa umma kwa ujumla unanufaika na raslimali zao.
CHADEMA inaamini katika kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huru, utakaoheshimu na kulinda haki na mali za watu, biashara huru na sekta ya watu binafsi bila kupoka mamlaka ya umma katika maeneo nyeti hususani pale penye hitilafu ya soko au penye maeneo nyeti ya kiuchumi. Tunaamini katika soko huru si soko holela.
Madhumuni ya kisiasa ya chama
Kukuza, kulinda, kuelimisha na kutetea haki za binadamu katika misingi ya Tangazo la Ulimwengu la haki za Binadamu na mikataba yote ya kimataifa inayolinda haki hizo na inayofutilia mbali ukandamizaji wa watu katika misingi ya rangi, jinsia, ukanda, umri au itikadi. Kuhakikisha kila mtu ana haki na uhuru wa kuabudu kwa minajili ya dini, madhehebu au imani yoyote anayotaka, bila kuathiri amani na/au utulivu wa mwenzake na jamii. Kuendeleza na kudumisha demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, kujenga utamaduni wa demokrasia katika jamii kwa kutambua haki za wengi katika maamuzi na pia kutambua haki za wachache kusikilizwa, kuheshimiwa na kulindwa, sambamba na kukubali ushindani huru, wa haki na wa wazi katika uchaguzi.
Madhumuni ya kiuchumi
Kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali za nchi yetu bila kuathiri uhuru wa taifa, na kuhakikisha kuwa umma kwa ujumla unanufaika na rasilimali zao. Kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huru, utakaoheshimu na kulinda haki na mali za watu, biashara huru na sekta binafsi bila kupoka mamlaka ya umma katika maeneo nyeti. Kujenga na kuimarisha kilimo, hususan cha umwagiliaji, na ufugaji katika lengo la kutosheleza taifa kwa chakula na kwa ajiri ya masoko ya biashara ya ndani na ya nje ili kuboresha maisha ya wakulima na wafugaji na kuendeleza sera ya kulinda ardhi, maliasili na mazingira kwa manufaa ya kilimo na ufugaji endelevu.
Kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali asilia za nchi ili zichangie kikamilifu katika pato la taifa na hasa katika kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii zinazotumiwa na wananchi wote.
Madhumuni ya kijamii
Kuendeleza juhudi za kuhakikisha haki za wanawake, watoto na wenye ulemavu kwa kuelimisha umma ili kuondoa fikra na mila potofu za ukandamizaji wa kijinsia, kuwanyima watoto haki za malezi bora na za kupata elimu ya kutosha, umuhimu wa kuwajali wenye ulemavu na kuwatimizia mahitaji yote ya msingi, pamoja na kutekeleza makubaliano na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za watoto, wanawake na walemavu. Kuboresha, kutunza na kutoa huduma za jamii, kwa mfano afya, elimu, maji, makazi na usalama wa raia, kwa ajili ya kukuza hali ya maisha ya watu. Kuhifadhi na kuboresha utamaduni wa taifa ili kujenga hadhi na heshima ya Watanzania na kuendeleza nyanja zote za utamaduni, burudani, michezo, sanaa na historia ya nchi.
Nimejitahidi kuyafupisha nisiandike yote na bado nina shaka kama mhariri ataweza kuyatoa yote maana ukurasa hautoshi.
Lakini pia yamo kwenye katiba na kwenye majukwaa na vyombo vya habari yanaimbwa kila siku na viongozi.
Mtaani hata mama ntilie na machinga wanajua “Pipo Pawa”. Wewe uko wapi hujui hii falsafa Dk.? Jipe muda upitie tovuti ya CHADEMA, soma katiba ya chama hiki, fuatilia mikutano yake na hotuba za viongozi wake, utagundua kwamba tunaamini CHADEMA tunayoifahamu na wewe utajiunga nasi! Karibu katika mapambano

No comments:

Post a Comment