KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Tuesday 22 May 2012




Matajiri G8 kumwaga trilioni 1/- Tanzania



KUNDI la nchi nane tajiri duniani-G8 limeahidi kuipa Tanzania dola milioni 897 za Marekani (sawa na zaidi ya Sh trilioni 1.3) chini ya mpango maalumu wa kuimarisha kilimo na usalama wa chakula barani Afrika. 

Kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete aliyehudhuria mazungumzo ya wakuu wa nchi hizo uliofanyika katika Ikulu ya Camp David iliyoko Maryland kuhusu kilimo katika Afrika, Ijumaa Rais Barack Obama alitangaza uamuzi huo wa G8. 

Kikwete ambaye alihudhuria mazungumzo hayo, alitangaza jijini hapa juzi alipozungumza na mwandishi wa habari hizi, akisema Marekani ndiyo iliyoahidi kutoa kiasi kikubwa ambacho ni dola milioni 315 (zaidi ya Sh milioni 470). 

Nchi zingine zilizoahidi ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Japan, halikadhalika Umoja wa Ulaya (EU), ambapo katika tangazo lake, Obama alisema nchi 45 za Afrika na kampuni binafsi za kimataifa ziliahidi kutoa dola bilioni tatu kwa ajili ya miradi kadhaa ya kilimo katika bara hilo. 

Miradi ya Tanzania inayotarajiwa kunufaika na msaada huo ni iliyo chini ya Mpango wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP) pamoja na mpango wa maendeleo katika ukanda wa Kusini. 

Kilimo ndiyo shughuli kuu ya uzalishaji katika Afrika na msukumo huu mpya unaoongozwa na Marekani, unalenga kuunganisha nguvu na raslimali kutoka sekta binafsi na kuziunganisha na sekta ya umma hasa juhudi za Serikali katika kuboresha kilimo na kukifanya cha kisasa zaidi, ili kuvuna zaidi katika hekta moja. 

Uwekezaji binafsi unasisitizwa katika kilimo cha mazao ya chakula na ugavi wa mbolea, viuatilifu na mbegu bora pamoja na uongezaji thamani kwenye mazao ya kilimo kwa kuyasindika. 

Rais Kikwete alisema msaada wa G8 utaanza kwa kuzinufaisha Tanzania, Ethiopia na Ghana, ambazo zimesifiwa kwa kuwa na mipango bora katika maendeleo ya kilimo. “Wameamua kuanza na nchi tatu na kupanua wigo kidogo kidogo,” alifafanua. 

Mpango huo mpya ulizinduliwa huku kukiwa na matatizo ya kifedha na kiuchumi Ulaya, lakini Rais Obama alisema Afrika lazima iangaliwe kwa umakini. 

Mkutano huo wa Camp David pia ulipitia ahadi zilizotolewa na G8 katika mkutano wake wa Italia miaka mitatu iliyopita, za kutoa dola bilioni 20 za Marekani kwa ajili ya maendeleo ya kilimo Afrika na nchi zingine zinazoendelea, ambazo baadhi yao hazijatekelezwa. 

Tanzania bado haijapokea dola milioni 30 kutokana na ahadi hizo. Wakati huo huo, Rais Kikwete alisema Serikali imeanza mawasiliano na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani ili kuihuisha tena akaunti ya Tanzania ya Changamoto za Milenia. 

“Tumewadokeza na wameonesha nia ya kusikiliza,” alisema. Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) lilitoa dola milioni 698 katika awamu ya kwanza kwa ajili ya kufadhili ujenzi wa barabara za Tunduma-Sumbawanga, Namtumbo-Mbeya, Tanga-Horohoro na Pemba. 

Pia zinafadhili skimu za ufungaji umeme katika mikoa sita na Zanzibar na uboreshaji wa ugavi wa maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro. Awamu ya pili nayo inatarajiwa kujielekeza katika barabara na ugavi wa maji. 

Katika mahojiano hayo, Rais Kikwete pia alieleza kwamba wawekezaji wa kigeni katika kilimo wametengewa ardhi kwa maelekezo ya mamlaka za mikoa husika kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), akipinga tuhuma kwamba wamekuwa wakipora ardhi kutoka kwa wakulima. 

“Wakulima binafsi wakubwa wanakuja kusaidia wadogo, na si kuwaondoa,” alieleza, akiongeza kuwa miradi iliyoanzishwa imekuwa pia ikitoa huduma za ugani na masoko kwa wakulima wadogo wanaoizunguka. 

Baadhi ya vyombo vya habari vya kigeni vimekuwa vikitangaza madai kwamba wakulima wakubwa wamepora mamilioni ya hekta za ardhi kutoka kwa wakulima wa Tanzania

No comments:

Post a Comment