KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Wednesday 16 May 2012

CHADEMA wamvaa Shibuda

•  Wajiandaa kumkabili, hata ikibidi kumrudisha CCM


na Waandishi wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeanza kukunjua makucha yake dhidi ya Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda, ambaye amekuwa na uhusiano tete na chama chake hicho, huku akikishambulia hadharani na kujipendekeza kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bila kificho.
Baada ya kuwa anatoa kauli za kukishambulia chama hicho hadharani bila kuchukuliwa hatua, juzi Shibuda aliibukia katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, Dodoma akavishambulia vyama vya upinzani na kukisifia CCM, akisema ndicho chenye uwezo wa kutawala, kwani vingine vyote bado havijastahili kukabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi.
Hata hivyo, alijikanganya mwenyewe alipotamka kuwa anatarajia kugombea urais kupitia CHADEMA; na akamwomba Rais Jakaya Kikwete awe meneja wake wa kampeni mwaka 2015.
Baada ya kauli hizo kuvuja na nyingine kuandikwa na vyombo vya habari, jana Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) lilitoa tamko kali likisema: “Vijana wote wa CHADEMA sasa tujiandae kikamilifu katika kukabiliana na mtu yeyote yule ambaye ataonekana kuwa kikwazo kwa chama chetu, matumaini na masilahi ya Watanzania kwa ujumla wake katika kuelekea kuchukua dola mwaka 2015.”
Katika tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche, CHADEMA kinasema kimeshtushwa na kauli ya Shibuda kusema kuwa vyama vya upinzani havina uwezo wa kutawala, huku akitaka kugombea urais kupitia chama hicho.
Vile vile, vijana hao wa CHADEMA walishangazwa na mbunge huyo kutangaza nia yake kupitia vikao vya CCM na kuomba msaada kwa Rais Kikwete, huku akijua kuwa CHADEMA kina vikao na taratibu zake katika masuala kama hayo.
Kwa msisitizo, BAVICHA ilisema: “Tunapenda kumwambia kuwa kama anaona kuwa yeye haendani na utamaduni wa chama chetu na anakiona kuwa hakina uwezo wa kuongoza dola anafanya nini kwenye chama ambacho anaona kuwa hakiwezi kuongoza dola? Kwanini atafute urais kwenye chama ambacho anaona hakiwezi kuongoza dola? Anawatania Watanzania?
“Ni heri akaenda kwenye hicho ambacho anaamini kuwa kinaweza kuongoza dola, kwani lengo la chama chochote kile ni kuchukua dola na si vinginevyo. “Tunapenda kuwahakikishia vijana wote wa Tanzania na wananchi kwa ujumla kuwa tayari CHADEMA kimejiandaa kikamilifu kuongoza dola na wasiwe na hofu na maneno yaliyotamkwa na mbunge huyu.”
Kwa sababu hiyo, Heche alisema BAVICHA itaitisha kikao cha Baraza lao kujadili kauli ya Shibuda na kuwasilisha mapendekezo kwenye vikao halali vya chama, ili hatua mwafaka zichukuliwe dhidi yake.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya kikao cha CCM tangu juzi zinasema Shibuda, ambaye alihama CCM na kujiunga CHADEMA mwaka 2010, alivishambulia vyama vya upinzani, kiasi cha kuwaacha midomo wazi Wana CCM wenyewe.
Mmoja wa vigogo wa CCM waliozungumza na gazeti hili juzi usiku alisema kwamba baadhi ya maneno aliyotumia Shibuda dhidi ya CHADEMA yalikuwa makali kiasi kwamba hata katika mikanda yao ya video wanazotumia kwa matangazo ya vyombo vyao vya habari, ilibidi wayahariri au kuyakata.
Baadhi ya Wana CCM wanaomfahamu vema Shibuda walisema kwa vyovyote vile Shibuda bado ni Mwana CCM aliyetafuta hifadhi CHADEMA kwa ajili ya kupata ubunge baada ya kuenguliwa na CCM.
Wengine walikwenda mbali na kusema hata kuenguliwa kwake na CCM ulikuwa mkakati mahususi wa Rais Kikwete kupenyeza watu wake katika CHADEMA, hasa ikizingatiwa historia ya mbunge huyo mwenye kuhusishwa na ukachero wa kisiasa.
Mmoja wa Wana CCM hao ambaye hayumo kwenye kambi ya Rais Kikwete ndani ya makundi hasimu ya CCM, alisema si kazi ngumu kwa serikali ya Kikwete kutumia pesa za walipa kodi kwa “kazi chafu kama hiyo.”
Baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa na harakati za Shibuda wanadai kwamba uhai wa mbunge huyo ndani ya CHADEMA ulidumu hadi siku ya kutangaza matokeo ya ubunge wake. Baada ya hapo amekuwa akiwashutumu viongozi wenzake hadharani hata katika kuchangia hoja za bungeni.
Katika matukio kadhaa, Shibuda amenukuliwa akisema viongozi wa CHADEMA ni “wachanga na wanaharakati” na kwamba wanapaswa kuvuna uzoefu wa kisiasa kutoka kwake kwa sababu ni “mzee, mkongwe na mzoefu.”
Hata hivyo, baadhi ya wabunge vijana, ambao yeye amezoea kuwaita “watoto” waliwahi kumweleza kuwa uzoefu anaojidai nao Shibuda ni wa siasa za CCM, si wa siasa za upinzani; wakasema kama ni kujifunza yeye ndiye alipaswa kujifunza kwao waliofanya siasa za mageuzi kwa zaidi ya miaka 18.
Amefika mahali pa kutofautiana na chama chake katika masuala muhimu ya kisera, likiwamo suala la posho nono za watendaji wa serikali na wabunge. Wakati CHADEMA kikisema posho hizo ama zifutwe au ziingizwe rasmi kwenye mfumo wa malipo ya wafanyakazi wote, Shibuda amekaririwa mara kadhaa akisema posho ni ujira wa mwira, ambao ni halali kwao, na kwamba hazitoshi.
Baadhi ya Wana CHADEMA wamekuwa wakisitiza kuwa Shibuda alitumwa kukisambaratisha chama chao, lakini kwa utamaduni na mkakati wa kiuongozi ndani ya CHADEMA, hawezi kufurukuta, maana walitambua nia yake hata kabla hajaanza kuwashambulia.
Hata hivyo wapo wanaotaka afukuzwe chama ili kutoa funzo kwa viongozi wengine wa chama hicho wanaotaka kuleta chokochoko, huku wengine wakisema apewe muda anaweza kujirekebisha. Wapo pia wanaodhani kwamba Shibuda “si lolote, si chochote” ndani ya CHADEMA, na kwamba haki anayostahili ni kupuuzwa tu, maana wananchi walishamtambua.
Hata katika jimbo lake, aliwahi kususa baadhi ya matukio ya chama kilipokuwa kinafanya ‘Operesheni Sangara’ katika mikoa ya Kanda ya Ziwa mapema mwaka jana, lakini wananchi waliitikia vema na kuendelea bila Shibuda; jambo ambalo linasemekana kumshtua.
Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya wabunge wa CHADEMA walidai kuwa Shibuda ameanza kujirekebisha, maana anashiriki katika baadhi ya mipango na mbinu zao dhidi ya CCM. Wanadai kwamba Shibuda alianza kushtuka walipofukuzwa madiwani watano wa CHADEMA Arusha kwa utovu wa nidhamu.
Sababu halisi za Shibuda kuwabeza viongozi wa chama chake hazijawekwa hadharani, lakini wachunguzi wa mambo wanasema uhusiano mbaya kati yake na chama ulianza mwaka 2010 kabla ya uchaguzi alipoomba apewe fedha za kampeni akanyimwa.
“Nasikia alimwendea mwenyekiti (Freeman Mbowe) akamwomba msaada wa pesa kwa ajili ya uchaguzi. Mbowe alichomwambia Shibuda ni kwamba chama hakina pesa za kuwapa wagombea waliokuwa wabunge kama yeye, na kwamba kama zingekuwapo wangeombwa kusaidia vijana na wengine waliojitokeza kugombea ubunge.
“Wakati huo, chama kilikuwa kinahaha kupata fedha za kampeni za urais, na Mbowe mwenywe alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Hai. Shibuda alipoambiwa kwamba hakuna pesa, aliondoka akisema maneno mabaya dhidi ya viongozi; na hajawasamehe hadi leo,” alisema ofisa mmoja wa CHADEMA ambaye alidai kujua siri hiyo.
Ofisa huyo alisisitiza kwamba kama si uvumilivu binafsi wa Mbowe na wazee wengine, Shibuda angekuwa amefukuzwa chama miezi kadhaa iliyopita kwa sababu hana mchango wowote wa maana anaokipa chama chake.
Badala yake, baadhi ya wanachama na viongozi wenzake wanasema amegeuka mzigo, na “kashfa” kwenye chama.
Iwapo hatua hii ya Bavicha itazingatiwa na vikao vya juu, na iwapo Shibuda hatabadilika, upo uwezekano mkubwa kwake kufukuzwa uanachama na ubunge kabla ya mwaka 2015.
Baadhi ya Wana CHADEMA wanadai asipojihadhari hata huo urais anaouota hatapata fursa ya kuugombea akiwa CHADEMA, kwani anaweza kuwa amefukuzwa chama.

No comments:

Post a Comment