KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Monday, 1 October 2012



Nagu ambwaga Sumaye



 *Mwandosya apeta
  *Waliotoka Chadema wang'ara
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk. Mery Nagu, na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.

Baada ya malumbano ya muda mrefu kuhusiana na uchaguzi wa ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia Wilaya ya Hanan’g, mkoani Manyara, hatimaye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk. Mery Nagu, amembwaga Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.

Dk. Nagu, mbaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hanan’g, aliibuka kidedea kwa kumshinda Sumaye kwa kura 167 katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa Wilaya ya Hanan’g usiku wa kuamkia jana.

Dk. Nagu alishinda kwa kupata kura 648 dhidi ya kura 481 alizopata Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005.

Jumla ya wanachama wa CCM 1,129 walishiriki kupiga kura na kufanya uamuzi huo ambao ulipokelewa kwa shangwe.

Akizungumza baada ya matokeo kutangazwa, Sumaye alisema amekubali matokeo hayo kwani uamuzi huo umefanywa na wanachama wa CCM.

Aliongeza kuwa ameridhishwa na matokeo hayo na uchaguzi ulikuwa huru, haki na uliendeshwa kwa kufuata taratibu.

Kwa upande wake, Dk. Nagu aliwashukuru wanachama wa CCM na wananchi wote wa Wilaya ya Hanan’g kwa kumuona bado anafaa kuwaongoza na aliwaahidi kuendelea kuwaletea maendeleo.

Kushindwa kwa Sumaye katika wilaya yake kunaweza kuathiri harakati zake za kisiasa katika siku zijazo kwa kuzingatia kuwa ni miongoni mwa wanasiasa ambao hivi sasa wanatajwa kuwa wana nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Sumaye hajawahi kuthibitisha ama kukanusha kama atagombea ama la licha ya kutajwa tajwa mara kwa mara.

MWANDOSYA, WALIOTOKA  CHADEMA WANG’ARA 

Chama tawala katika Mkoa wa Mbeya, kimekamilisha uchaguzi zake katika wilaya zake huku viongozi waliohamia chama hicho wakitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waking’ara.

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyothibitishwa na makatibu wa CCM wilaya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Mbeya, Sambwee Shitambala, ameibuka kidedea baada ya kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Mbeya Mjini.

Shitambala aliibuka kidedea kwa kupata kura 653 na kumshinda kwa mbali Kamanda wa Vijana wa CCM mkoa wa Mbeya, Stephen Mwakajumilo, aliyeambulia kura 278.

Katika uchaguzi huo, Diwani mstaafu wa Kata ya Ruanda jijini Mbeya, Ephrem Mwaitenda, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mbeya Mjini kwa kupata kura 552 na kumshinda Deo Mwasanga aliyepata kura 308 na Emil Mwaituka 155.

Wilayani Rungwe, Diwani mstaafu wa Kata Bulyaga, Ally Mwakalindile, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo na kuwashinda Samweli Mwakyambiki na Anthon Mwanjevele huku nafasi ya mjumbe wa NEC ikichukuliwa na Prof. Mark Mwandosya.

Katika wilaya ya Mbeya Vijijini, aliyekuwa Katibu wa Chadema Mbeya vijijini, Ipyana Seme, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo kwa kupata kura 869 na kumbwaga  William Simwali aliyekuwa akitetea nafasi hiyo.

Nafasi ya mjumbe wa NEC ilichukuliwana Fredy Towanga aliyepata kura 651 na kumshinda Amani Kajuna aliyepata kura 604.

Kwa upande wa Wilaya ya Kyela, Diwani wa Kata ya Ipinda, Hunter Mwakifuna, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya na kumshinda Mwenyekiti wa Wazazi wilaya hiyo, Vicks Mahenge.

Wilaya mpya ya Momba Mwenyekiti wa CCM aliyechaguliwa ni Juma Rashid.

Katika Wilaya ya Mbarali, Mwenyekiti wa CCM wilaya aliyechaguliwa ni Mathayo Mwangomo kwa kura 541 na kumshinda Ignas Mgawo aliyepata kura 429. 

Mgawo alikuwa akitetea nafasi hiyo wakati nafasi ya mjumbe wa NEC ilichukuliwa na Geofrey Mwangulumbi.

Kwa upande wa Wilaya ya Chunya, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, ameibuka mshindi wa ujumbe wa NEC huku nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ikichukuliwa na Katala Makerere.

MARGARET  SITTA, KAPUYA WASHINDA

Mbunge wa Viti Maalum, Margaret Sitta, ameshinda nafasi ya ujumbe wa NEC kwa kura 460, katika uchaguzi uliofanyika wilayani Urambo, mkoani Tabora juzi.

Katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Wilaya, Martha Faustine Susu alishinda kwa kupata jumla ya kura 472.

Katika Uchaguzi wa Wilaya ya Kaliua, Elias Kaseko, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti kwa kura 587, huku akiwaacha nyuma Hamis Madili, aliyepata kura 328 na kura nne kuharibika.

Mbunge wa Urambo Magharibi,  Profesa Juma Kapuya, ameshinda nafasi ya ujumbe wa NEC kwa kupata kura 565 baada ya kuwashinda Gulamhussein Dewji, aliyepata kura 265 na Mussa Kisheri kura 65. 

Aliyeshinda nafasi ya Uchumi na Mipango ni Francis Kassanga na nafasi ya Uenezi ya Wilaya imechukuliwa na Paul Shija.

NKAMIA, MALECELA WASHINDA NEC

Mbunge  wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia, ameibuka mshindi wa ujumbe wa NEC kupitia Wilaya Nchemba.

Akizungumza na jana na NIPASHE, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo, Felister Bura, alisema Nkamia alishinda baada ya kupata kura 602 kati ya kura zote 878 zilizopigwa baada ya kuwabwaga wagombea wenzake, Fedrick Duma na Said Omar Sambala.

Kwa upande wa nafasi ya uenyekiti, aliyeshinda ni Alhaj Shabani Issa Kilalo kwa kupita bila kupingwa.

Katika Wilaya ya Chamwino, Charles Ulanga, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wakati nafasi ya ujumbe wa NEC ulikwenda kwa Samuel Malecela.

Katika wilaya ya Kongwa, nafasi ya uenyekiti imechukuliwa na  Mussa Abdi Mutari na aliyeshinda ujumbe wa NEC ni Godwin Mkanwa.

Katika Wilaya ya Mpwapwa, walioshinda nafasi ya uenyekiti ni George Chigwiye wakati nafasi ya ujumbe wa NEC aliyeshinda ni aliyewahi kuwa Mbunge wa Mpwapwa, George Lebeleje.

Katika Wilaya ya  Kondoa, nafasi ya uenyekiti ilikwenda kwa Othuman Juma Gora na nafasi ya ujumbe wa NEC mshindi ni Mohamed Lujuo Moni.

Katika wilaya mbili ambao uchaguzi ulifanyika jana ambazo ni wilaya za Dodoma Mjini na Bahi, uchaguzi hadi jana jioni kura bado zilikuwa zikiendelea kuhesabiwa.

BUKOBA MJINI, MISENYI  ZAPATA VIONGOZI

Uchaguzi ngazi ya wilaya katika CCM mkoani Kagera,umefanyika jana kwa wilaya tano huku wilaya nyingine tatu zikitarajia kufanya uchaguzi huo leo.

Wilaya zilizofanya uchaguzi ni Bukoba Mjini, Kyerwa, Missenyi, Ngara na Biharamulo huku Wilaya za Bukoba Vijijini na Karagwe zikitarajia kufanya uchaguzi huo leo. Wilaya ya Muleba inatarajia kufanya uchaguzi Ijumaa ijayo.

Kwa upande wa Wilaya ya Bukoba Mjini, Yusuph Ngaiza, alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kuwashinda wapinzani wake akiwemo Mwenyekiti aliyekuwa anatetea nafasi hiyo, Robert Bahati na Murungi Kichwabuta.

Nafasi ya ujumbe wa NEC kutoka Wilaya ya Bukoba Mjini imechukuliwa na Abdul Kagasheki, baada ya kuwashinda Filbert Katabazi huku nafasi ya Katibu Uchumi na Fedha ikichukuliwa na George Rubahyura na nafasi ya Uenezi ikichukuliwa na Ramadhani Kambuga. 

Wilayani  Missenyi, Fidelis Kibarabala, ameibuka mshindi wa kiti cha Uenyekiti na huku nafasi ya NEC ikichukuliwa na  Deptson Balyagati. Nafasi ya Itikadi na Uenezi imechukuliwa na Cronery Kamuzora huku nafasi ya Uchumi na Fedha ikichukuliwa na Rutwaza Kalisa.

Matokeo ya Biharamulo, Ngara na Kyerwa, yatatolewa baada ya uchaguzi wa mkoa mzima kumalizika.

ABOOD ANG’ARA MOROGORO

Mbunge wa Morogoro Mjini, Abduaziz Abood, amefanikiwa kutetea nafasi yake ya ujumbe wa NEC baada ya kuwaacha kwa mbali wapinzani wake.

Abood aliwashinda wapinzani wake wawili Amina Mhina na Kevin Njunwa. Abood alijipatia kura 784, Mhina kura 54 wakati Njunwa kura 14 wakati Fikiri Juma  akifanikiwa kutetea nafasi ya mwenyekiti wa wilaya kwa kipindi kingine cha tatu baada kupata kura 535 huku wapinzani wake, Pascal Kianga akipata kura  355 na Latifa Ganzel kura 14.

Katika  Uchaguzi wa wilaya ya Mvomero, Naibu wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, alianguka kuwania ujumbe wa NEC baada ya kushindwa na mpinzani wake, Suleman Sadiq Murad.

Murad alipata kura 648 dhidi ya 371 alizopata Makalla na nafasi ya pili ilishikwa na Hellen Mbezi, aliyepata kura 10 huku kura tatu zikiharibika kati ya wajumbe 1,030 waliopiga kura.

Katika nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, wajumbe walimchagua Abdallah Mtiga, aliyemshinda mgombea mtetezi Pololeti Mgema kwa kura 674 dhidi ya Mgema aliyepata kura 374 huku kura tisa zikiharibika.

Katika uchaguzi Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka alichaguliwa kuwa miungoni mwa wajumbe watano wa mkutano mkuu wa Taifa kupitia wilaya hiyo kati ya wagombea 15 waliojitosa,huku Yusuf Kingu, akitetea nafasi ya katibu mwenezi wa wilaya.

Katika Wilaya ya Ulanga, Mwenyekiti wa Halamashauri ya Wilaya hiyo, Furaha Lilongeri, alichaguliwa kuwa mjumbe wa NEC na kuwashinda Henry Barua, Clalence Mgoano na Agustino Matefu.

Katika nafasi ya Mwenyekiti, Khalid Nalioto aliwashinda Maximiliun Kidaula na Fadhili Liguguda.

Katika wilaya ya Kilosa, nafasi ya mwenyekiti imechukuliwa na Nassoro Udelele aliyemshinda  mwenyekiti wa zamani, Christoper Wegga.

Katika nafasi ya ujumbe wa NEC, Chisuligwe Khadudu alifanikiwa  kunyakua nafasi hiyo kwa kuwashinda Hamad Hila na Theofhil Nangusu.

Wilaya ya Kilombero, viongozi watatu wa juu wa chama hicho wametetea nafasi zao akiwemo Mwenyekiti, Abdallah Kambangwa; Katibu wa Siasa na Uenezi Pelegrin Kifyoga na Katibu wa Uchumi, Rajabu Kiwanga. Harun Kondo amefanikiwa kushinda nafasi ya NEC.

GACHUMA AIBUKA NEC

Katika uchaguzi wa Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Christopher Mwita Gachuma, alishinda kuwa mjumbe wa NEC kwa kupata kura 1,091 dhidi ya Maira Marwa aliyepata 181 wakati nafasi ya uenyekiti wilayani Tarime ilichukuliwa na mwenyekiti wa zamani, Rashid Bugombi kwa kupata kura 1,081 dhidi Nurandi Chacha aliyepata kura 166.

Katika Wilaya ya Rorya, Samwel Kibohe, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wakati Thobias Rayar, alichaguliwa kuwa mjumbe wa NEC.

Katika wilaya ya Butiama, Christophr Marwa Siagi, alichaguliwa kuwa mjumbe wa NEC huku Yohana Marwa Mirumbe akichaguliwa kuwa Mwenyekiti kwa kumuangusha Mwenyeki wa zamani, Bwire Nyabukika.

WALIOSHINDA TEMEKE

Uchaguzi wa nafasi mbalimbali ndani ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam ulifanyika mwishoni mwa wiki, ambapo kwenye Wilaya ya Temeke, nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya imenyakuliwa na Yahaya Sikunjema.

 Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumamosi mpaka usiku wa manane na matokeo yake kutangazwa alfajiri ya jana, Phares Magese, ameshinda nafasi ya ujumbe wa NEC kwa kupata kura 623 na kumbwaga Issa Mangungu, aliyepata kura 580.

Walioshinda nafasi tano za ujumbe wa Mkutano Mkuu ni Asha Mlawa, Lucy Kanyopa, Hadija Maganga na Issa Zahoro.

NIPASHE ilipomtafuta Katibu wa Mkoa wa Chama hicho Abilahi Mihewa alikiri kutangazwa kwa matokeo hayo, lakini alisema hakuwepo ofisini kwa muda huo, kwani alikuwa anasimamia uchaguzi wa wilaya za Ilala na Kinondoni na angetoa matokeo hayo baadaye.

Hata hivyo, uchaguzi wa Wilaya za Ilala na Kinondoni ulitazamiwa kuendelea mpaka usiku na matokeo yake yanatarajiwa kutangazwa mapema alfajiri ya leo. 

K'NJARO YATANGAZA TAREHE ZA UCHAGUZI

Chama tawala mkoani Kilimanjaro, kimetangaza tarehe za mikutano mikuu ngazi ya mkoa na wilaya, ambayo itachagua viongozi wa ngazi mbalimbali za chama hicho kiwilaya, kimkoa na kitaifa.

Katibu wa CCM mkoani humo, Steven Kazidi, jana aliliambia NIPASHE kuwa Oktoba 3, mwaka huu, uchaguzi utafanyika katika wilaya za Same, Mwanga na Rombo.

Alisema Oktoba 4, mwaka huu Wilaya ya Hai, Oktoba 5, wilaya ya Moshi Mjini na Oktoba 12, Wilaya za Siha na Moshi Vijijini huku ngazi ya mkoa ni Oktoba 15, mwaka huu.

"Utaratibu wa chama ni kuwa kampeni zitafanyika kwenye ukumbi, haturuhusu na hatuna utaratibu wa watu kuzunguka, ni chanzo cha rushwa na Chama kimezuia rushwa. Wagombea wote wanatakiwa kuomba kura kwenye ukumbi badala ya kuwafuata nyumbani, ni marufuku kwenda kuwafuata kuomba kura,” alisema.

Alisema kwenye mikutano hiyo, wagombea watapewa nafasi ya kujieleza na mgombea yeyote wa CCM anayegombea nafasi yoyote ndani ya CCM akifanya kampeni hasa ikihusisha na rushwa na ikabainika, ataadhibiwa kwa kuzuiwa kushiriki kugombea na hata kama ameshinda kwa rushwa atanyang’anywa ushindi.

WILAYA ZA ARUSHA LEO  

Uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Mkoa wa Arusha,  unaanza leo kwa wagombea wa nafasi za ngazi ya wilaya.

Katibu wa Siasa na  Uenezi wa Mkoa, Loota Sanare Mollel, alithibitisha kwamba uchaguzi kwa ngazi ya wilaya zote unafanyika leo na kwa mkoa ni Septemba 11.

KIKAO CHAVUNJIKA, FFU WAINGILIA

Kikao cha maandalizi ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Wilaya ya Korogwe kililazimika kuvunjwa baada ya kutokea vurugu zilizosababishwa na baadhi ya wagombea  wanaowania nafasi mbalimbali.

Hali hiyo ilikilazimu kikao hicho kuvunjika bila kumalizika kwa ajenda zilizokusudiwa kujadiliwa na Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walizingira eneo hilo kwa lengo la kuimarisha usalama.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia NIPASHE, kikao hicho kilianza juzi asubuhi na ajenda kuu ilikuwa ni wajumbe kusomewa majina yaliyorudi baada ya kupitishwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM Taifa pamoja na kupewa taratibu za uchaguzi.

Hali ya hewa ilichafuka baada ya Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe, Elli Minja, alipowaarifu wajumbe kuwa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Tanga imeagiza kutofanyika kwa kampeni ya aina yoyote kwa wagombea na kwamba wanatakiwa kutulia na kusubiri siku ya uchaguzi.

“Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa, iliagizwa kuwa ni marufuku kwa wagombea kufanya kampeni, ikiwemo kutengeneza vipeperushi wala kulisha watu pilau,” alisema.

Kwa mujibu wa chanzo  chetu, baada ya wajumbe kupewa taarifa hiyo, ndipo  walipoanza kutupiana maneno na kushutumiana, hali iliyozua mtafaruku mkubwa na baadhi yao wakitaka kupigana.

Miongoni mwa wagombea ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini, Said Kallaghe anayewania nafasi ya Katibu wa Fedha na Uchumi na Edmund Mndolwa anayewania nafasi ya ujumbe NEC kupitia Wilaya ya Korogwe.

Wagombea wengine ni Stephen Ngonyani ambaye pia anawania nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Korogwe na Hussein Mngazija ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilayani humo aliingia katika mgogoro huo baada ya kutupiwa maneno ya shutuma na kashfa.

Akizungumza na NIPASHE, Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe, Elli Minja, alithibitisha kutokea kwa tafrani hiyo.

“Ni kweli kulikuwa na vurugu kwa wagombea kutoleana maneno, lakini sasa kilichobaki ni kungoja uchaguzi,” alisema.

Naye Ngonyani alisema alilazimika kutoka nje ya kikao alipoona tafrani zimeanza.

“Ni kweli hali ya hewa juzi katika kikao ilichafuka, lakini mimi baada ya kuona hivyo, nilitoka nje na sikupenda kuwApo katika malumbano hayo. Mimi ni kiongozi na si vema kujiingiza katika migogoro hiyo na kutupiana maneno ya kejeli kwa kuwa siyo busara,” alisisitiza Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini.

Akizungumzia tuhuma alizobebeshwa, Mngazija alisema baadhi ya wagombea wanachafua jina lake na kudai kuwa hata nafasi aliyonayo sasa aliipata kwa kuiba kura.

“Wanataka kunichafua, yote hiyo ni baada ya kuona kuwa Katibu na Mwenyekiti wamewaambia agizo la mkoa la kutofanya kampeni, wanajiona wamechelewa na sasa wanataka kubebesha watu lawama,” alisema na kuongeza:

“Kusema kweli maneno waliyoyatoa yaliniuma na ndiyo maana nikataka kurusha ngumi. Hayana ukweli wowote hadi kikao kikavunjwa.”

Akithibitisha kuwepo kwa agizo la kutofanya kampeni katika chaguzi hizo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Tanga, Mrisho Gambo, alisema agizo hilo wanalisimamia kikamilifu.

“Ni kweli agizo lipo kwamba hakuna wagombea kufanya kampeni chafu na wanatakiwa kutulia kusubiri siku ya uchaguzi na sisi kwa upande wangu Korogwe nalisimamia agizo hilo kikamilifu," alisema Gambo.

Imeandikwea na Woinde Shizza na John Ngunge, Arusha; Thobias Mwanakatwe, Samson Fridolin na Mashaka Mgeta, Dar;  Kibuka Prudence, Kagera; Augusta Njoji, Dodoma; Salome Kitomari, Moshi;  na Lulu George, Tanga na George Marato, Samson Chacha, Mara.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment