KAMBI INAYOHUSISHWA NA LOWASSA YAIBUKA KIDEDEA UCHAGUZI MKUU CCM ARUSHA MJINI.
Waziri mkuu mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli Mh. Edward Lowassa akipongezwa mara baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu ya Wilaya ya Monduli uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha ualimu Monduli, Mh Lowassa ameshinda kwa kishindo kwa kuwabwaga wapinzani wake kwa idadi ya kura 709, mpinzani mwingine amepata kura 44 na mshindi mwingine aliibuka na kura 7.
Mahmoud Ahmad,Arusha
Katika kile kinachoonekana ni kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu wa urais mwaka 2015 kambi inayohusishwa na Waziri Mkuu aliyejizulu Bw. Edward Lowasa imeibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa CCM wilaya ya Arusha mjini.
Katika uchaguzi huo uliokuwa na kila aina ya vituko, Mwenyekiti wa zamani wa CCM wilaya ya Arusha Jubilate Kileo aliangushwa vibaya na mpinzani wake Dkt. Wilfred Ole Soilel ambaye ni daktari wa hospitali ya St. Elizabeth kwa tofauti ya kura 70 .
Kinyanganyiro kingine kilikuwa kwenye nafasi ya mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM taifa (NEC) ambapo Godrey Mwalusamba ambaye ni mwenyekiti wa UVCCM wilaya alifanikiwa kupata kura 449 na kuwaangusha vibaya wapinzani wake Loota Laiser aliyepata kura 79 na Dkt. Harold Adamson aliyeambulia kura 7.
Kitendo cha wajumbe wa mkutano mkuu kumchagua Dkt. Ole Soilel anayehusishwa na kambi ya Lowasa kuliibua simanzi kwa kambi nyingine ambapo katika hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo sanjari na katibu wa CCM Arusha Mary Chatanda walionekana kuwa wanyonge muda wote kitendo kilichoibua maswali mengi kwa baadhi ya wajumbe waliohudhuria uchaguzi huo.
Hata hivyo, kijana mmoja ambaye ametajwa kuwa ni mfuasi wa kundi la Kileo alipewa kichapo nje ya ukumbi wa uchaguzi ndani ya hoteli ya Naura jijini Arusha kwa kile kinachodaiwa ni kutoa lugha chafu kwa wafuasi wa Musa Mkanga ambaye naye alikuwa akiwania nafasi ya uenyekiti wa CCM wilaya.
Awali kabla ya uchaguzi huo taarifa zilizolifikia blog hii zimedai ya kwamba ndani ya ukumbi wa uchaguzi Kileo aliulizwa maswali na wajumbe wa mkutano huo, kwamba aeleze sababu za yeye kushindwa kusimamia jimbo la Arusha mjini lililoangukia upinzani pamoja na kata yake ya Kaloleni hali iliyompa wakati mgumu kujibu maswali hayo.
No comments:
Post a Comment