Kada wa Chama cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro, Agrey Mareale (pichani) amechaguliwa kuwa Mjumbe wa CCM-NEC kutoka Wilaya ya Moshi Mjini.
Mareale amemwangusha mpinzani wake katika nafasi hiyo Buni Ramole. Aidha katika uchaguzi huo, Bi. Elizabeth Minde alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya ya Moshi Mjini.
Mkoani Mbeya, ndugu Amani Kajuna amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa kwa ushindi wa kura 465 dihidi ya kura 37 za Lusekelo Williard na 33 za Mary Mwaijumba.
Huko Iringa, mwanahabari Tumaini Msowoya anayewakilisha gazeti la Mwananchi mkoani Iringa amechaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wa mkoa wa Iringa.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Jumba la Maendeleo mjini humo, Msowoya ambaye pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya uandishi wa habari katika chuo Kikuu cha Tumaini Kampasi ya Iringa alishinda kiti hicho baada ya kuwabwaga wagombea wenzake wawili.
Uandishi wa habari ilikuwa sifa muhimu kwake katika uchaguzi huo na kumpa nafasi ya ziada ya kukitwaa kiti hicho dhidi ya wagombea wenzake kabla ya uchaguzi huo, “Tunahisi chama hakina mahusiano stahili na wanahabari, tukimpata mwanahabari huyu katika nafasi hii tunaamini atatusaidia kutuunganisha na sekta hiyo muhimu ya habari,” walisikika baadhi ya wajumbe wakisema kabla ya uchaguzi huo.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gelard Guninita aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi alisema jumla ya kura 302 zilipigwa. Alisema kati ya kura hizo, Msowoya alipata kura 188 akifuatiwa kwa mbali na Abba Ngilangwa aliyepata kura 76 huku Ramadhani Baraza akiambulia kura 36.
Alipopewa nafasi ya kuwashukuru wajumbe kwa kumpatia ushindi huo, Msowoya alisema anafahamu kazi ngumu aliyoanayo mbele yake ya kuwaangunisha vijana wa mkoa mzima wa Iringa ili kukiletea ushindi chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, “Uongozi unapimwa kwa mambo mengi lakini unapokuwa katika siasa sifa kubwa ni kukisaidia chama chako kupata ushindi,” alisema huku akiomba ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari.
Katika uchaguzi huo, wajumbe walimchagua Seki Kasuga kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la umoja huo.
Guninita alisema nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa ilikwenda kwa Cornel Malangalila aliyepata kura 130 dhidi ya David Banda aliyepata kura 76 na Malipula Chalamila aliyepata kura 90.
Nafasi ya Uwakilishi katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Irina ilikwenda kwa Janeht Innocent aliyepata kura 149 dhidi ya kura 137 alizopata Nuru Mwinukana na nafasi ya uwakilishi wa Mkutano Mkuu wa Wazazi Mkoa ilikwenda kwa Akimu Mwasambogo aliyepata kura 149 dhidi ya kura 145 alizopata Salvatory Ngelela.
Source: Wavuti