AJINYONGA KWA KUNYIMWA UNYUMBA
na Walter Mguluchuma, Mpanda
MKAZI wa Mtaa wa Mpanda Hotel, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, Nzego Vicent (33), amejiua kwa kujinyonga na kamba baada ya mkewe kumnyima tendo la ndoa.
Tukio hilo limetokea hapo juzi majira ya saa 7:30 usiku jirani na nyumba waliyokuwa wakiishi wanandoa hao.
Mke wa marehemu huyo aitwaye Agnes Nicodemu, alisema siku ya tukio mumewe ambaye alikuwa ametoka kwenye pombe za kienyeji, alifika nyumbani kwake majira ya saa 6:20 usiku na kumtaka ampe tendo la ndoa.
Alisema kutokana na shughuli alizokuwa amezifanya mchana, alimwomba mumewe avumilie hadi siku itakayofuata kwa kile alichomweleza kuwa hakuwa tayari kufanya tendo hilo kwa kuwa alikuwa amechoka.
Kwa mujibu wa mama huyo, baada ya kumjibu hivyo, mumewe hakuridhika na ndipo alipoanza kumshutumu kuwa huenda ana mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine.
“Baada ya hapo alianza kunishambulia kwa kunipiga huku akinitolea maneno ya kunitisha kuwa lazima ataniua kwa panga,” alisema mama huyo huku akitoka machozi.
Agnes baada ya kuona kipigo kimezidi, anasema aliamua kukimbia nje na mumewe nae aliamua kutoka huku akiwa na mashoka mawili, akaelekea kusikojulikana na kuacha nyumba ikiwa wazi.
“Ilipofika aubuhi, majira ya saa 12:30 asubuhi, majirani walinifuata na kunieleza kuwa mume wangu amejinyonga kwa katani, jirani na nyumba yetu,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho.
Wakati mkazi huyo akijinyonga kwa kunyimwa unyumba, jijini Dar es Salaam, mkazi wa Manzense, Mustafa Juma (23), amefariki dunia kwa kujinyonga na kamba ya manila.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema chanzo cha kifo hicho bado hakijafahamika na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment