KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Tuesday, 26 July 2011

Kumekucha; CUF Na CHADEMA WAJIPANGA KUMRITHI ROSTAM IGUNGA!



LIPUMBA, SLAA WATAMBA KULINYAKUA JIMBO LA IGUNGA CCM BADO KIMYA
Waandishi wetu
SIKU chache baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kutangaza kuwa kiti cha Jimbo la Igunga liko wazi kufuatia kujiuzulu kwa Rostam Aziz, vyama vya siasa vimeanza mbio za kuwania jimbo hilo.Rostam alijiuzulu ubunge wa Igunga Julai 13 mwaka huu, kutokana na kile alichokiita siasa uchwara ndani ya CCM, na wiki iliyopita Spika Makinda, alitangaza kuindikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuieleza kuwa kiti hicho cha ubunge, sasa kiko wazi.  

Hatua ya Spika Makinda kuijulisha Nec kuhusu kujiuzulu kwa Rostam, ni mwanzo wa mchakato wa kukijaza kiti hicho cha ubunge kilichokuwa kikikaliwa na kada huyo wa CCM kwa miaka 18 iliyopita.Baada ya taarifa hiyo ya Spika Makinda, Nec sasa itatakiwa kutangaza uchaguzi mdogo kwenye jimbo hilo ndani ya siku 90 kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

Lakini katika kile kinachoonekana harakati za kukitwaa kiti hicho, vyama vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, TLP, UDP,  CCM na SAU, jana vililithibitishia gazeti hili kwamba vitasimamisha wagombea wao wa ubunge katika uchaguzi mdogo utakaotangazwa na Nec hivi karibuni.

CUF yataja wagombea wao
CUF kimetoa onyo kwa vyama vya upinzani kuwa ni bora vingeacha kugombea jimbo hilo kwa kuwa tayari chenyewe kimelitwaa.

Katika kuonyesha majigambo, chama hicho kilisema kina nafasi kubwa ya kuchukua ushindi katika jimbo hilo kutokana na mgombea wao, Leopard Mahana, kuombwa na wananchi kugombea tena ubunge baada ya kubwagwa na Rostam kwenye uchaguzi wa mwaka jana.Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, CUF haitafanya kosa la kuliacha jimbo hilo tena.

Alisema hayo muda mfupi baada ya kutoa rambirambi kwa Ubalozi wa Norway nchini kutokana tukio la vifo vya watu 93 vilivyotokana na milipuko ya mabomu nchini humo. “Vyama vya upinzani wasijidanganye kusimamisha mbunge katika jimbo hilo kutokana na chama chetu kuwa na nafasi kubwa ya kushinda kutokana na wananchi wa eneo hilo kumchagua kijana wetu kugombea jimbo hilo,” alitamba Lipumba na kuongeza:

“Katika uchaguzi wa mwaka jana chama chetu ndio pekee kilichosimamisha mgombea kati ya vyama vya upinzani kushindana na Rostam, hivyo vyama vya upinzani kwa sasa vinapaswa kuachia nafasi kama vilivyofanya kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana,”alisema Lipumba.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana, Jimbo la Igunga lillikuwa na wagombea wawili ambao ni Rostam  kupitia CCM pamoja na   Mahana kupitia CUF.

Chadema waja na Opesheni Chukua Igunga
Kwa upande wake,Chadema kimesema kitaweka mipango yake hadharani hivi karibuni ya namna kilivyojipanga kuingia kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.

Katibu Mkuu wa Chadema hicho, Dk Willibrod Slaa aliliambia Mwananchi jana kuwa chama kimedhamiria kuweka mgombea katika jimbo hilo na hata sasa vijana wako jimboni.“Mikakati ipo,na tutaiweka hadharani baadaye kwa sasa ni mapema mno, lakini  vijana wetu wapo kule,”alisema Dk Slaa.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema, John Heche aliliambia Mwananchi juzi kuwa wanakwenda Igunga kuzindua Opresheni ya Chukua Igunga.“Kama tulivyo na utaratibu wa kuwa na operesheni za kujenga chama ambazo mara nyingi zimejulikana kwa jina la Operesheni Sangara, safari hii katika moja ya mikakati ya kulichukua Jimbo la Igunga, Chadema imeandaa Operesheni Chukua Igunga,”alisema Heche.

Oparesheni hiyo ya siku ilianza juzi Jumapili na inaongozwa na vijana ambapo Mwenyekiti huyo alisema kazi ya kuchukua jimbo imekabidhiwa kwao.

NCCR-Mageuzi yapeleka ujumbe Igunga
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema chama hicho kitasimamisha mgombea katika Jimbo la Igunga na kusisitiza kuwa kwasasa kimetuma timu ya watu sita kwa ajili ya kutizama hali ya kisiasa ilivyo.

“Timu tuliyoituma itakapolejesha majibu ndio tutaweza kutanzaga watakaochuana kuwania nafasi ya kugombea katika jimbo hilo kwa tiketi ya NCCR,” alisema Ruhuza,

Hata hivyo, Ruhuza alisema kuna dalili za wazi kwamba  idadi kubwa ya vyama vya upinzani vitasimamishwa wagombea katika jimbo hilo, huku akionyesha wasiwasi hali hiyo inaweza kuipa CCM mwanya wa kushinda.

“Kuna dalili za wazi kila chama cha upinzani kitataka kuweka mgombea katika jimbo la Igunga. Ni vyema vyama vya upinzani kukubaliana na kusimamisha mgombea anayekubalika ili iwe rahisi kushinda, lakini waking’ang’ania wataishia kugawana kura tu,” alisema Ruhuza.

Sau nao wamo
Mwenyekiti wa Sau, Paul Kyara alithibitisha kuwa chama hicho pia kitaweka mgombea katika jimbo hilo huku akisisitiza kuwa katika uchaguzi huo mdogo jimbo hilo litachukuliwa na wapinzani.

“Tumetuma timu ya wajumbe watatu kwa ajili ya kutizama hali ya kisiasa wilayani Igunga, timu hiyo itarudi wiki hii na majibu kamili, pamoja na hayo mchakato wa kupata mgombea tayari umeshaanza kufanyika,” alisema Kyara.

UDP yavuta pumzi
Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alisita kuzungumzia uchaguzi huo huku akifafanua kwamba ni mapema mno.“Ndio kwanza imetangazwa kuwa jimbo liko wazi…, sasa ndio kila mtu aseme kuwa atasimamisha mgombea, ni mapema sana kuzungumzia suala hilo,” alisema Cheyo kwa ufupi.


CCM bado inavuta pumzi
Kwa upande wake, CCM kimesema bado hakijakaa kujadili namna kitakavyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Igunga.Akizungumza jana Katibu Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema CCM bado haijakaa vikao kujadili suala hilo.

“Chama chetu hufanya uamuzi wake kwa kupitia katika vikao, hadi sasa sisi hatujakutana kujadili suala hilo, ”alisema Nnauye.Jimbo la Igunga limeachwa wazi kufuatia aliyekuwa Rostam kujuuzulu nyazifa zake zote ndani ya CCM kwa kile kilichodaiwa ni kujivua gamba, ingawa mwenyewe alikataa.


Nec yapokea barua ya Spika
Kwa upande wa  NEC, imekiri kupokea barua ya kujiuzulu kwa Rostam baada ya Spika Makinda kuiandikia.Kaimu Mkurugenzi wa Tume hiyo, Sisti  Cariah, alisema barua hiyo imewasilishwa jana kutoka bungeni.“Ni kweli leo (jana) tumepokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kuhusu kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Rostam Aziz,” alisema Cariah
Kwa mujibu wa Cariah, uteuzi unafanyika kuanzia  siku ya 20 hadi 50 tangu Spika wa Bunge kupokea barua na kuiarifu Nec.

 Imeandikwa na Fidelis Butahe, Hadija Jumanne na Aziza Masoud, Geofrey Nyangóro . Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment