KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 30 June 2011

ZITTO AFICHUA UFISADI MADINI

1st July 2011
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ameshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua mapato katika sekta ya madini ya miaka 10 iliyopita, kutokana na jumla ya mapato yaliyolipwa na makampuni ya madini kwa serikali kubainika yalikuwa na tofauti ya Sh. bilioni 20.
Zitto alisema kuwa kiasi ambacho wawekezaji walidai kuwa walilipa kama kodi kilikuwa pungufu ya Sh. bilioni 20 kulinganisha na kiasi kilichoelezwa na serikali.
Alitoa ushauri huo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, bungeni, mjini hapa jana.
Alisema tofauti hiyo ilitokana na ripoti iliyotolewa na Taasisi iitwayo Extractive Industries Transparency Initiative (EITI) baada ya kukagua malipo yaliyofanywa na makampuni ya madini kwa serikali mwaka huo.
Zitto alisema ushauri huo ni muhimu kutekelezwa kwani utasaidia kuepuka ugonjwa unaoikumba nchi ya Nigeria, ambako fedha zinalipwa kama mapato ya serikali, lakini zinaishia kuingia mifukoni mwa watu binafsi.
Alisema mamlaka husika ya serikali ilipoulizwa na Kamati ya

Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC, ambayo yeye (Zitto) ni mwenyekiti wake, ilidai kuwa nyaraka zinazohusiana na suala hilo zimechomwa moto.
Alisema baada ya ushuru wa mafuta ya taa kuongezwa kutoka Sh. 52 hadi 400.30, serikali inapaswa sasa kutoa agizo ushuru huo upelekwe kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili ukasaidia umeme vijijini.
Alisema wakati wa bajeti kulikuwa na malalamiko mengi yaliyotolewa na baadhi ya wabunge kuhusu misamaha ya kodi, lakini serikali ilishikilia msimamo wake kwamba, lazima misamaha hiyo iendelee.
Hata hivyo, alisema kuna msamaha wa kodi uliotolewa na serikali, ambao anadhani serikali haikufikiria vizuri katika kuutoa.
Alisema jambo hilo alilijadili vizuri kwenye Kamati ya Fedha na Uchumi na kwamba, alitarajia kuwa lingebadilishwa kwenye Bunge lilipokaa kama kamati ya matumizi, lakini haikufanyika.
Alisema Waziri Mkuu alikutana na makampuni ya kutafuta mafuta nchini wakamuomba kwamba, waondolewe kodi katika mafuta wanayotumia katika kutafuta mafuta kwa madai kwamba, jambo hilo litasaidia uwekezaji zaidi.
Hata hivyo, alisema kwa sasa hivi kwenye eneo la utafutaji mafuta na gesi hakuna wa kushindana na Tanzania na pia serikali haiwezi kutoa vivutio kama ambavyo Kenya wanatoa, kwani wana makampuni manne yanayotafuta mafuta wakati Tanzania ina makampuni zaidi ya 22.
Alisema pia Tanzania haiwezi kutoa vivutio kama Msumbiji wanavyotoa, kwani faida pekee waliyonayo (Msumbiji) ni gesi waliyoigundua, ambayo iko kusini mwa Mkoa wa Mtwara. Zitto alisema kitu, ambacho serikali inatakiwa kukifanya ni kuhakikisha kiwanda cha gesi (LNG plant) kinajengwa haraka iwezekanavyo kabla Msumbiji hawajafanya hivyo.
Alisema Tanzania haitakuwa na faida ya kutoa vivutio kwa mafuta ya makampuni, ambayo yanatafuta madini, kwani itapoteza fedha bila sababu ya msingi.
"Na jambo hili ni la kuangalia kwa sababu kwenye mikataba yetu ya mafuta tuna vitu viwili; kuna kitu kinaitwa profit oil na coast oil. Coast oil maana yake ni kwamba kampuni ya mafuta ikishapata mafuta inatoa gharama zake zote, wanajilipa. Wakishajilipa zile gharama za mafuta yaliyoabaki ya ziada ndio tunayogawana,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema-Morogoro), Suzan Kiwanga, aliitaka serikali kubadili utaratibu wa chai ofisi zake ili fedha zilizotengwa kwa ajili hiyo zipelekwe kugharamia miradi ya maendeleo.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema-Mbeya), Naomi Kaihula, aliitaka serikali kutumia rasilimali zilizopo kuanzisha mfuko wa kuwatunza watoto nchini.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema-Pemba), Raya Ibrahim Khamis, alisema anasikitishwa kuona Wazanzibari wakisahaulika kwenye kitabu cha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment