16th January 2012
Dk.Slaa akiwa maeneo ya nyumbani kwao Regia Mtema
Dk.Slaa akiongea na Mama yake na Zitto Shida Salum na Muhonga Ruhwanya
Mzee Estalus Mtema baba wa marehemu Regia Mtema (katikati)
David Kafulila na Stephen Wassira
Picha ya Regia Mtema
Waimbaji
Waimbaji wa Karismatiki Katoliki wakiimba nyimbo za maombolezo
Mabere Marando na Mathias Chikawe
David Kafulila na Job Ndugai
Baadhi ya waombolezaji
Halima Mdee na Ester Bulahya
John Heche, Grace Kihwelu na Mh Rose Kamili
John Mnyika katika majadiliano kadhaa msibani
Bango likielekeza wageni njia kuelekea nyumbani kwao Regia Tabata CHANG'OMBE
Mwili wa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari, wilayani Kibaha, mkoani Pwani juzi, utaagwa katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam kesho.
Baba mkubwa wa marehemu, Canutte Mtema, alisema jana kuwa baada ya kuagwa, mwili wa marehemu utasafirishwa kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika katika makaburi ya mjini Ifakara, wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, keshokutwa.
Mtema alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa familia ya marehemu Tabata Chang'ombe, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema shughuli hizo zitatanguliwa na misa ya kumuombea marehemu itakayofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Segerea, jijini Dar es Salaam, leo saa 9:00 alasiri.
Mtema alisema baada ya misa hiyo, ndugu, jamaa, marafiki na majirani, watapata fursa ya kuuaga mwili wa marehemu na kutoa heshima zao za mwisho kanisani hapo leo.
Mtema alisema kesho itakuwa ni zamu ya wabunge, maofisa wa serikali na watu na wengine, ambao hawakupata fursa leo, kuuaga mwili wa marehemu katika viwanja vya Karimjee.
JK, PINDA WATOA POLE
Katika hatua nyingine, viongozi wa vyama vya siasa, serikali, taasisi za umma na binafsi, wabunge pamoja na ndugu, jamaa, marafiki na majirani, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, jana walimiminika nyumbani kwa familia ya marehemu kwa ajili ya kuwafariji wafiwa.
Miongoni mwa viongozi wakuu waliofika, ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye aliongozana na mkewe, Tunu Pinda, na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Wengine ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama hicho (Bavicha), John Heche.
SPIKA AMMWAGIA SIFA
Spika Makinda akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwafariji wafiwa, alisema leo Kamati ya Uongozi na Huduma za Bunge itakutana na kupanga atayeliwakilisha Bunge katika mazishi.
Alisema Regia amefariki dunia akiwa bado kijana, ambaye alionyesha uwezo mkubwa wa kufikiri na kujenga hoja, pia alikuwa hodari na kwamba alipenda kuwa wa kwanza kuuliza maswali katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni.
Pia alisema marehemu alikuwa akipenda kujifunza mambo na alikuwa akijisahihisha kama atakosea na alikuwa rafiki wa kweli na makini sana.
VIGOGO WOTE CHADEMA KUSHIRIKI MAZISHI
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema chama pamoja na Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa Chadema, wamepitisha maamuzi kwamba wabunge pamoja na viongozi wakuu wote wa chama hicho watashiriki katika hatua zote za mazishi.
KILOMBERO WAMLILIA
Wakati huo huo, mamia ya wananchi wa wilaya ya Kilombero wamepatwa na simanzi kubwa, huku wakiwa wamekusanyika katika makundi wakiomboleza kifo cha Regia.
Baadhi ya wafuasi wa Chadema walipita katika maeneo mbalimbali wakizunguka na pikipiki huku wakipeperusha bendera za chama hicho nusu mlingoti huku kundi la viongozi wa serikali wakiongozwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, walikusanyika nyumbani kwa marehemu Ifakara mjini.
Dk. Mponda aliongozana na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Francis Miti; Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abdu Mteketa; Mwenyekiti wa Halmashauri, Ramadhani Kiombile na mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Abdallah Kambangwa, pamoja na viongozi mbalimbali.
Katika ofisi ya mbunge huyo, kulikuwepo na shughuli mbalimbali za maandalizi ya mazishi ambapo viongozi wa Chadema na wanachama wa chama hicho walikusanyika ili kuunda kamati maalum itakayoshughulikia mazishi.
Waziri Mponda alisema kuwa alizipata habari za msiba huo akiwa njiani kutoka katika jimbo lake la Ulanga Magharibi kueleza kuwa marehemu alikuwa mchapakazi na alikuwa na uchungu wa kulitetea jimbo lake bila kujali itikadi ya vyama.
Naye Mteketa alisema baada ya kupata taarifa ya kifo hicho alishituka kutokana na alivyomzoea marehemu licha ya upinzani mkali wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kwa upande wake Kiombile alisema kifo cha Regia ni pengo kubwa katika wilaya ya Kilombero na kwamba marehemu alikuwa akimpigia simu ili kumpa ushauri.
Naye Kambangwa alisema hakuamini aliposikia habari za msiba wa Regia hadi aliposikia kupitia vyombo vya habari na kueleza kuwa Mungu amemchukua mwanasiasa kijana aliyekuwa akijali zaidi maslahi ya wananchi anaowaongoza na sio itikadi za chama chake pekee.
Mmoja wa mtu aliyekuwa karibu ya marehemu, Amina Simbamkuti, alisema ameathirika kwa kiasi kikubwa na kifo hicho kwani kwa kushirikiana naye walikuwa wakitatua kero mbalimbali za wananchi.
Uongozi wa Chadema katika Kata ya Ifakara kupitia kwa Katibu Mwenezi, Antony Kamonalelo, ulisema taratibu za mazishi zinaendelea na wameunda kamati ya watu watano.
NCCR YATUMA RAMBIRAMBI
Chama cha NCCR-Mageuzi kimetuma salaam za rambirambi kwa Chadema kwa kufuatia kifo cha Regia.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, katika salamu hizo jana kwa Mbowe, alisema kuwa wamepokea taarifa ya kifo hicho kwa mshtuko.
Mbatia alisema familia, ukoo, ndugu, jamaa na Watanzania kwa ujumla wamepokea kifo hicho kilichotokea juzi kwa mshtuko mkubwa.
No comments:
Post a Comment