KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Sunday, 29 January 2012

Ban Ki Moon; " Migiro Ameomba Kupumzika"


NEWYORK, Marekani
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amesema Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo,  Asha Rose Migiro ameomba mwenyewe kustaafu.Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijiji New York, Marekani, Ki Moon alisema hata hivyo Dk Migiro ataendelea kuwapo kwenye ofisi za umoja huo, akiratibu shughuli mbalimbali hadi Juni mwaka huu.

 Alisema mbali na Dk Migiro, mwingine aliyeomba kuacha kuutumikia umoja huo ni Vijar Nambiar ambaye ni Mkuu wa  Ofisi yake.

 “ Kama mlivyotangaziwa mwishoni mwa mwaka jana kuhusu mabadiliko  yanayotarajiwa kufanyika katika nafasi za  watendaji waandamizi. Ningependa kuongezea na kuwajulisha kwamba, Naibu Katibu Mkuu,  Dk Migiro  na Vijar Nambiar wamewasilisha   kwangu maombi  yao ya kutaka kuachia nafasi zao  ili kuniruhusu  kuunda timu mpya ya  maofisa waandamizi nitakaofanya nao kazi katika  awamu  ya pili ya  uongozi wangu,” alisema Ki Moon.

 “Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati  kabisa kwa  Naibu Katibu Mkuu, Dk Asha- Rozi Migiro,  kwa uamuzi wake huo, na kwa kazi nzuri na ushirikiano mkubwa na usio na shaka wala doa  alionipatia katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita akiwa msaidizi wangu wa karibu,” alisisitiza.  
Alisema Dk Migiro alimpa  ushirikiano mzuri mno na kumshauri kwa busara huku akijituma kwa uadilifu mkubwa katika kukabiliana na changamoto nyingi  zinazoukabili Umoja wa Mataifa.


Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, aliyasema hayo baada ya  kuainisha mpango kazi na vipaumbele vyake katika miaka mitano ya muhula wa mwisho ya uongozi wake Kwa mujibu wa Ki Moon watendaji wengine watakaondoka ni wa Idara za Utawala, Maendeleo, Huduma za Mikutano,  Habari,  Ofisi ya Upokonyaji wa silaha,  na Mshauri wa Masuala ya Afrika.
 Wengine ni   wasimamizi  wa  Idara za Uchumi za Afrika na Ulaya,   waratibu wa  mifuko ya maendeleo na Idadi ya watu  UNDP na UNFPA.  Chanzo: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment