KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Monday, 19 December 2011

Zambia, Chipolopolo; Yaenda Gabon na kumbukumbu ya vifo 1993

TIMU ya taifa ya Zambia, ni kati ya mataifa yatakayokuwa kwenye Fainali za Afrika 2012.

Lakini safari ya Zambia kwenda kwenye fainali hizo zinazoandaliwa kwa pamoja kati ya Gabon/Guinea ya Ikweta zitakuwa na kumbukumbu nyingi hasa kwa kikosi cha Zambia kilichopotea wakiwa njiani kwenda kulitumikia taifa lao.

Itakumbukwa wachezaji wa Zambia walianguka na ndege kwenye ufukwe wa Gabon mwaka 1993. Zambia ilikuwa ikienda Senegal kucheza mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, fainali zilizofanyika Marekani 1994.

Wachezaji na maofisa wa timu ya Zambia walifariki kwa ajali hiyo ya ndege April 28, 1993 ambayo hadi leo hakuna uhakika wa nini kimesababisha. Katika ajali hiyo, wachezaji 18, watumishi 12 wa ndege na walifariki.

Mwaka 2003, serikali ilitoa taarifa tata kuhusiana na ajali hiyo na kuongeza hasira kwa familia za wafiwa.

Wachezaji waliofariki kwenye ajali hiyo ni Richard Mwanza na David Chabala (makipa) Samuel Chomba, Winter Mumba, Kenan Simambe, John Soko, Whiteson Changwe na Robert Watiyakeni ambao ni mabeki

Viungo ni Eston Mulenga, Godfrey Kangwa, Derby Makinka, Moses Chikwalakwala na Wisdom Chansa wakati mshambuajili walikuwa  Kelvin Mutale, Timothy Mwitwa, Numba Mwila, Moses Masuwa na Patrick Banda.

Muda mfupi Zambia ilisimama kwa kuwa kulikuwa na mipango ya kutengeneza wachezaji. Ilifanya vizuri katika fainali za Afrika 1994, iliingia fainali lakini ikaishia kuwa ya pili.

Fainali za mwakani, tayari Zambia imekwishaanza maandalizi kwa mujibu wa Chama cha Soka Zambia (FAZ), kwamba Desemba 6 ilikuwa siku ya kwanza kwa wachezaji kukutana na kuanza kambi.

Ikiwa katika sehemu ya maandalizi hayo, Zambia itacheza na Angola Desemba 18 mjini Dundo, kaskazini mwa Angola.

Baadaye Chipolopolo itakwenda Afrika Kusini kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ambayo yatakuwa makini kuanzia Desemba 27 hadi Januari 18, 2012.

Itakapokuwa Afrika Kusini, itacheza na Bafana Bafana Januari 11 lakini bado haijapangwa siku na mahali. Chipolopolo iko Kundi A pamoja na Equatorial Guinea, Libya na Senegal.

*Rekodi ya Zambia

Zambia haikushiriki Michuano ya Afrika kati ya 1957 hadi 1968 lakini ilianza kushiriki 1970 na hadi 1972 haikufuzu. 1974, 1994 ilishika nafasi ya pili wakati nafasi ya tatu ilikuwa 1982, 1990 na 1996.

Chipolopolo iliyokuwa ikiitwa Kenneth Kaunda Eleven (KK Eleven) jina la Rais wa Kwanza wa Zambia haikufuzu mwaka 1976, 1980, 1984 na 2004 lakini iliishia raundi ya kwanza mwaka 1978, 1986 lakini 1988 ilijitoa.

1992 na 2010 iliishia robo fainali 2010. Raundi ya kwanza pia ilikuwa mwaka
1998, 2000, 2002, 2006 na 2008.

Zambia itaingia kwenye michuano ya 2012 chini ya kocha wake, Herve Renard ambaye tayari amewataka wachezaji watakaochaguliwa kuunda timu itakayocheza Fainali za Afrika 2012 kukaza buti kwani mashindano ni magumu na vinginevyo watakuwa wasindikizaji.

Timu hiyo ambayo bado haijatajwa rasmi, itawategemea zaidi mastaa wake wanaocheza soka nje wakiwemo makipa Kennedy Mweene anayechezea Free State Stars ya Afrika Kusini pamoja na Kalililo Kakonje anayekipiga TP Mazembe.

Pia wamo mabeki Joseph Musonda wa Golden Arrows (Afrika Kusini), Emmanuel Mbola na Stophira Sunzu (TP Mazembe) na  Davies Nkausu wa  SuperSport.

Viungo wa nje ni Rainford Kalaba (TP Mazembe), Felix Katongo (Ashdod) na William Njovu (Ironi Kiryat Shmona) za Lesotho,  Isaac Chansa (Orlando Pirates), Noah Chivuta (Free State Stars) na Clifford Mulenga wa  Bloemfontein Celtic zote za Afrika Kusini.

Washambuliaji ni Fwayo Tembo Basel (Uswisi) na  Justine Zulu anayechezea  Ironi Rishon leZion ya Lesotho.

Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani ni  Francis Kasonde (Power Dynamos), Thomas Nyrienda (Zanaco)  Nyambe Mulenga (Zesco United) na Jimmy Chisenga (Red Arrows), Bruce Musukunya (Red Arrows),  Ronald Kampamba na Evans Kangwa wote wa Nkana FC

No comments:

Post a Comment