Mafuriko yaua 1watu 2 Dar, Mara
Madaraja yakatika, usafiri balaa
Madaraja yakatika, usafiri balaa
Madaraja yakatika, usafiri balaa
Madaraja yakatika, usafiri balaa
Aidha, watu wanne wengine wanne wamekufa maji wilayani Bunda, Mkoa wa Mara kwa kusombwa na mafuriko.
Licha ya madaraja kukatika na kusababisha wananchi kushindwa kuvuka kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini pia maeneo mbalimbali ya jiji yalijaa maji na kusababisha barabara kufungwa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliliambia NIPASHE kuwa vifo vya watu hao vilitokana na kusombwa na maji na kunaswa na umeme.
Kova alisema wananchi walipoteza mali zao, kujeruhiwa na magari kushindwa kutembea katika barabara kutokana na msongamano.
“Watu wanane wamepoteza maisha yao kutokana na mvua hizi na tulishirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), vikosi vya zima moto na uokoaji, wananchi na Polisi katika kazi ya kuokoa,” alisema.
Kutokana na vifo hivyo, idadi ya watu waliokufa kutokana na athari za mvua hizo jijini Dar es Salaam imefikia watu 13, baada ya juzi watano kuripotiwa kufa maji katika mafuriko yaliyosabbaishwa na mvua kubwa zilizonyesha kuamkia juzi.
MAENEO YALIYOATHIRIKA
Baadhi ya maeneo ya jiji yaliyoathirika zaidi kutokanan na mvua hizo ni pamoja na Tandale, Tabata Matumbi, Tabata Camp, Tabata Segerea, Buguruni, Kinondoni Mkwajuni, Jangwani, Kigogo eneo la Mto Msimbazi na Mikocheni jirani na Hospitali ya TMJ.
MADARAJA YAKATIKA
Madaraja yaliyokatika jana kufuatia mvua hizo ni pamoja na Mbezi Tangibovu, Goba kupitia Makongo na baadhi ya sehemu za barabara zilijaa majina kuziba kingo za madaraja.
Mengine ni Msewe, Kimara Golani, Ubungo Kisiwani, Mbezi Luis kuunganisha na eneo la Goba, Kimara Kilungule na Kinyerezi.
Baadhi ya madaraja yaliyosombwa ni mapya ambayo yalianza kutumika hivi karibuni likiwemo linalounganisha Goba na Makongo wilayani Kinondoni.
Barabara zilizofungwa kutokana na kujaa maji ni Kawawa eneo la Kigogo Mto Msimbazi, Morogoro eneo la Jangwani, Mandela sehemu za Tabata Matumbi hadi Buguruni sheli.
Maeneo ya Sinza Kamanyola nako magari yaliyokuwa yameegeshwa pembezoni mwa barabara yalisombwa na maji na kuangushwa darajani.
Wananchi katika baadhi ya maeneo jijini walijikuta wakipanda juu ya paa za nyumba zao ili kujiokoa wao pamoja na familia zao kufuatia makazi yao kumezwa na mafuriko.
Mvua hizo ambazo zilinyesha kuanzia juzi usiku ziliendelea hadi jana mchana na hivyo kusababisha baadhi ya shughuli kusimama hususani kwa wafanyabisha wanaouza bidhaa nje na daladala kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mgeni Yusuph mkazi wa Kinondoni Mkwanjuni, aliliambia NIPASHE kuwa mvua za mwaka huu ni kubwa ikilingaishwa na za miaka iliyopita.
“Hapa huwa maji yanajaa lakini mvua hizi za juzi usiku zimevunja rekodi kwani nyumba zetu zimejaa maji na maeneo ya jirani ambayo tulikuwa tunapita nayo yamejaa maji,” alisema.
Wakazi wa maeneo ya Jangwani walionekana kusimama juu ya paa huku wakilia na kuomba msaada ili waweze kuokolewa na Helikopta la Polisi iliyokuwa ikizunguka katika sehemu mbalimbali za jiji.
Eneo la Kigogo bonde la Msimbazi baadhi ya wananchi waliokolewa na Helkopta na Tabata Matumbi na kupelekwa katika sehemu za nchi kavu.
Aidha, katika eneo la Tabata Kisukuru Mto wa Maji Chumvi ulifurika na kusababisha kukatika mawasiliano kati ya sehemu hiyo na Makoka.
Kutokana na kukatika kwa madaraja, wakazi wengi wa jiji walishindwa kwenda katika maeneo ya kazi na biashara huku baadhi wakiamu kurejea nyumbani baada ya kukumbwa na adha hiyo.
Daraja la Bondeni karibu na Lugalo katika barabara ya Bayamoyo, baada ya kupata nyufa, lilifungwa na magari yote yaliyokuwa yakitokea Bagamoyo, Bunju, Mbweni, Boko, Tegeta, Mbezi, Goba, Kawe, Mwenge, Ubungo kulazimika kushusha abiria na kulazimika kupanda magari yaliyokuwa ng’ambo yake.
Wanajeshi wengi, wakiwemo askari wa Polisi wa Jeshi walikuwa katika daraja hilo kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Waendesha pikipiki na bajaj waliitumia vizuri fursa hiyo kujipatia kipato kutokana na wananchi wengi kuhitaji usafiri huo kuunganisha safari.
MNYIKA:SERIKALI ISAIDIE WANANCHI
Akizungumzia athari za mvua hizo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alitaka serikali kutumia fedha za Maafa kuwasaidia wananchi waliokumbwa na mafuriko na kupotelewa na mali zao.
Mnyika alisema Bunge kila mwaka linapitisha fedha hizo na lengo lake ni kusaidia wananchi wanapokumbwa na maafa ya aina yoyote.
Alisema katika jimbo lake, madaraja kadhaa yamesombwa na mafuriko ya mvua hizo zilizonyesha juzi usiku na kwamba serikali inatakiwa kuchukua hatua za dharura ili kuwasaidia wananchi wake.
Mnyika alitaka ufanyike uchunguzi wa kina ili kubaini watalaam waliosimamia ujenzi wa madaraja hayo ambayo alisema yamekatika kutokana na mvua ya siku mbili.
“Lazima uchunguzi wa kina ufanyike kwa kuwa inaonekana haya madaraja yalijengwa chini ya kiwango ndiyo maana yamekatika kwa haraka,” alisema.
Aidha, alitaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusiana na athari za kiuchumi zilizotokea baada ya kunyesha mvua hizo kwani hivi sasa kuna baadhi ya watu wameathirika kwa namna moja ama nyingine.
Alisema ametoa taarifa katika kitengo cha maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kwani idadi ya watu wa waliothirika na mvua hizo ni kubwa.
Alisisitiza kuwa kama serikali haina fedha iwatangazie wananchi ili juhudi za kuwachangisha wananchi wenye uwezo ziweze kufanyika kwa haraka.
FAMILIA 181 ZAHIFADHIWA SHULENI
Familia 181 ambazo nyumba zao ziko Bonde la Msimbazi katika eneo liitwalo Spenco, zimehifadhiwa katika Shule ya Msingi Mtakuja iliyipo Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Familia hizo zimehifadhiwa kwenye madarasa manne ya shule hiyo baada ya nyumba zao; baadhi kujaa maji na nyingine kubomoka kutokana na mafuriko ya mvua hizo
Vilevile daraja la Salender Bridge lililoko eneo la Upanga limeanguka, pamoja na bomba kubwa la kupitishia maji lililoko eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo, eneo hilo limezuiwa, huku askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiweka ulinzi.
Pia baadhi ya wakazi wa maeneo ya Kiwalani; ikiwamo Yombo Reli, Kwa Gude na Migombani, pia wamekosa makazi baada ya nyumba zao kujaa maji na vyombo vyao kuelea juu.
Kadhalika kuta za viwanda vilivyoko eno la Tabata Matumbi, zimeanguka kutokana na mvua hizo.
RC DAR: HALI NI MBAYA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, aliwambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa hali ni mbaya tofauti na matarajio.
Sadick alisema watu walioathirika na mvua hizo, wamehifadhiwa katika Shule ya Msingi Mchikichini, wengine Germanus Rutihinda, Mzambarauni, Kibasila na Shule ya Sekondari Msimbazi.
Sadiki alisema jana vifaa vya kuwasitiri waathirika, yakiwamo majaketi havikutosha kutokana na idadi yao kuwa kubwa na eneo waliko kutofikika kirahisi.
Hata hivyo, alisema helikopta itaendelea kudondosha vifaa hivyo kwa waathirika kwa vile haziwezi kutua katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua.
Alisema miongoni mwa vyombo vilivyotumika kuokoa waathirika ni pamoja na boti.
Eneo la Jangwani, baadhi ya watu walijitolea kuokoa waathirika na mafuriko, huku wengine wakitumia mwanya huo kujinufaisha kwa kuwatoza waathirika kati ya Sh. 5,000 na Sh. 10,000 kama malipo ya kuwaokoa.
Eneo la Kiwalani hali ilikuwa mbaya kwa wakazi maeneo hayo kutokana na mafuriko kuingia kwenye majumba na kuharibu mali zao.
Akizungumza NIPASHE, mkazi wa eneo hilo, Ally Muhogo, alisema mvua hizo zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali na kwamba walipojaribu kuyachota maji yalikuwa yakiongezeka.
Alisema walishindwa kufanya shughuli zao za kuwaingizia kipato kutokana na hali hiyo na kuwalazimisha kusubiri mvua ikatike.
“Tumechota maji mpaka tumechoka na tukikaa nje ndipo tunazidi kulowa huku ndani kukizidi kujaa maji hivyo tumeamua kukatisha shughuli zetu za leo na kuamua kwa sasa tukae kitandani mpaka hapo mvua itakapoisha,” alisema.
Naye Mkazi wa Yombo Kilakala, Elizabeth Nchimbi, alisema mafuriko hayo yalisababisha kukosekana kwa usafiri kwa kuwa daraja ambalo linatumiwa na magari lilijaa maji na kusababisha daladala kukatisha safari.
Katika bonde la Mto Mzinga, nyumba nyingi zilizingirwa na maji na baadhi ya watu walikwama na kuonekana wakiwa wamekaa juu ya paa za nyumba zao wakiomba msaada na pia malori matatu ambayo yalikuwa yanaoshwa yalizama.
Maeneo mengine ambayo yameathirika na mafuriko hayo ni Kijichi, Makuka, Mtoni, Kiburugwa, Mianzini, Nzasa, Kingugi, ambako nyumba 30 zilisombwa na maji.
Eneo la Azimio nyumba 30 zilizama na maji na wananchi walihifadhiwa kwa wajumbe.
Hata hivyo, Timu ya maofisa kutoka Kitengo cha Maafa cha Manispaa ya Temeke, ilikwenda kufanya tathmini na kujionea namna ya kutoa msaada na kutangaza kuwa Shule ya Msingi Kibasila itatumika kuhifadhia watu walioathirika.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Magreth Nyalile, alisema kuwa atatoa taarifa ya vifo kwa baadaye.
Hali ya usafiri kwa abiria waliokuwa wanatoka eneo la Mwenge kwenda Mbagala ilikuwa ni ya taabu baada ya daladala kuamua kupandisha nauli kutoka Sh. 500 hadi Sh. 1,000 na kila mmoja alitakiwa kulipia mlangoni kisha kupanda katika gari.
Mkuu huyo wa mkoa, ameziagiza Manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke kuchukua hatua za kuwasaidia waathirika hao na kuhakikisha kuwa wanapatiwa huduma muhimu za afya, chakula na sehemu za kulala.
KINONDONI YAUNDA KIKOSI KAZI
Akizungumza na NIPASHE jana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordani Rugimbana, alisema wamekwisha kupokea maagizo hayo na tayari wameunda kikosi kazi katika wilaya zote na kwamba wanafanya kazi ya kuangalia maeneo ambayo yameathirika na kutoa msaada kwa haraka.
Alisema vikosi hivyo vitakuwa vinafanya kazi ya uokoaji, kutenga maeneo kwa ajili ya kuwahifadhi waathirika na kuwapa huduma mbalimbali.
Rugimbana alisema mpaka sasa kazi ya uokoaji inaendelea vizuri katika maeneo yote ambayo wananchi walikuwa wamekwama pamoja na wale ambao walikuwa juu ya mapaa.
Alisema kazi hiyo ya uokoaji linafanyika chini ya Jeshi Polisi kwa kushirikiana na kikosi cha zima moto cha uokoaji.
Hata hivyo, Rugimbana alisema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Maafa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ilitoa msaada wa mablanketi, magodoro na chakula kwa waathirika.
Alisema hadi sasa wamewaomba wananchi wote wanaoishi mabondeni kuhama kwani wamejulishwa kuwa mvua hizo zitanyesha kwa siku moja au mbili.
TANROADS YATATHMINI
Kwa upande wake, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alipoulizwa kuhusiana na ujenzi wa madaraja yaliyokatika, alisema wahusika wa suala hilo ni Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ambao walikuwa wanazungukia maeneo yaliyoathirika na kwamba bado hajapatiwa taarifa juu ya suala hilo.
Alisema kwa kuwa wahusika wanafanyia tathmini athari hizo, watatoa taarifa kuhusu ujenzi wa madaraja ambayo yamekatika.
WANNE WAFA BUNDA
Watu wanne wamekufa maji katika matukio tofauti, wakiwemo watatu baada ya kusombwa na maji, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Bunda Mkoa wa Mara.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Robert Boaz, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo yaliyotokea katika vijiji vitatu tofauti wilayani hapa.
Boaz alisema tukio la kwanza lilitokea Desemba 17, mwaka huu majira ya asubuhi katika Kijiji cha Balili wilayani Bunda, ambako watu wawili waliokuwa wakichunga ng’ombe walikufa maji baada ya kusombwa na mafuriko wakati wakivuka Mto Rubana kwenda kutoa ng’ombe walioingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Ni kweli matukio yote ninayafahamu maana yametokea huko kwenu Bunda... miili ya watu hao ilipatikana na kufanyiwa mazishi,” alisema Boaz.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Marwa Maranya (25), Raia wa Kenya na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Enock.
Alisema mwili wa marehemu mmoja ulipatikana siku ya tukio na wa mwingine juzi.
Aliwataja wengine waliokufa maji kwa kusombwa na mafuriko kuwa ni Raphael Benkiko Mahuta (63), mkazi wa Kijiji cha Hunyari na Seta Masoro, mkazi wa Kijiji cha Sarawe.
ABIRIA 1,500 WA TRENI WAKWAMA
Zaidi ya abiria 1,500 wamekwama kwenye kituo cha reli cha mkoani Dodoma kutokana na kuharibika kwa njia ya reli kati ya Dodoma na Morogoro.
Abiria hao ambao waliwasili jana saa 7:00 mchana wakitokea Kigoma na Tabora walishindwa kuendelea na safari yao kufuatia kituo hicho cha Gurwe wilayani Mpwapwa kuharibika kutokana na mafuriko.
Mmoja wa maofisa waandamizi wa kituo hicho ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa madai kuwa si msemaji, alisema abiria hao waliwasili jana mchana, lakini walishindwa kuendelea na safari kutokana reli hiyo kuharibika vibaya.
“Reli hiyo imeharibika vibaya kutokana na mvua zilizoanza kunyesha tangu juzi…kwa hiyo abiria wameshindwa kuendelea na safari,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL)Mkoa wa Dodoma, imeamua kuwasafirisha abiria hao kwa mabasi ili kupunguza gharama ambazo zitajitokeza.
Alisema kampuni hiyo imekodisha mabasi 14 ya Kampuni ya mabasi ya Shabiby kwa ajili ya kuwasafirisha abiria hao ambapo hadi juzi usiku walisafirisha abiria 881.
“Abiria wengine tuliwasafirisha juzi usiku na hawa wengine waliobaki bado tunaendelea kuwasafirisha. Abiria wengi wanaelekea Morogoro,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, pia mamlaka hiyo imeamua kutoa posho kwa abiria wake kwa ajili ya kujikimu ikiwa ni pamoja na chakula.
Alisema pia abiria hao kwa sasa wanalala kwenye mabehewa ya treni huku wakiendelea kusubiri mabasi yaliyokodiwa kwa ajili ya kuwasafirisha.
Aidha, alisema mafundi bado wanaendelea kutengeneza njia hiyo ya treni usiku na mchana.
“Kwa sasa njia hiyo imefungwa kwa muda hadi hapo itakapotafutiwa ufumbuzi, na treni haziruhusiwa kupita,” alisema.
Hata hivyo, NIPASHE lilizungumza na mmoja wa abiria, Sebastian Mbavu, Mkazi wa Mpanda mkoani Rukwa, ambaye alisema hadi sasa hawajui hatma yako kwa sababu fedha zimewaishia.
Mbavu alisema jana asubuhi TRL ilitoa Sh. 3,000 kwa kila abiria kwa ajili ya kununulia chakula, lakini hawajui fedha hizo ni kwa ajili ya mlo wa siku nzima au vipi.
Alisema kinachomuumiza zaidi ni familia yake yenye watoto wadogo ambayo anahofia inaweza kupata maradhi ikiwa ni pamoja kuugua kifua kutokana na baridi.
“Sijui hii hali itaisha lini, nina familia tena yenye watoto wadogo. Na fedha zimeanza kuniishia kwani kuna vitu vingine ambavyo inabidi ninunue na havikuwa kwenye bajeti yangu,” alisema.
Aliitaka serikali iangalie kwa undani suala hili la njia za treni kwa sababu zinatumiwa na watu wengi hasa kutoka Kigoma, Tabora, Morogoro, Mwanza na Mpanda.
Abiria mwingine, Desdery Mwandike, alisema treni hiyo iliwasili jana saa 7:00 mchana na kutangaziwa kuwa hawataweza kuendelea na safari kutokana na reli kuharibika na mafuriko.
Alisema baada ya kutangaziwa hivyo waliambiwa wavute subira huku kampuni hiyo ikiendelea kutafuta njia nyingine ya kuwasafirisha.
“Huwezi amini, mimi nina watoto wadogo nimeshindwa kuwalaza kwenye mabehewa imebidi niwapeleke wakalale kwenye nyumba ya wageni,” alisema na kuongeza kuwa hali hiyo inawagharimu sana kwa sababu hawakupanga bajeti ya kulala nyumba ya wageni.
Alisema kuna baadhi ya abiria wenzao wameishiwa fedha na hawajui cha kufanya ingawa mamlaka hiyo imetoa Sh. 3,000 kwa kila abiria kwa ajili ya kununua chakula.
“Mimi hadi sasa sijui tutakaa hapa hadi lini, maana tunaambiwa tusubiri kuna mabasi yanakuja lakini hadi sasa sijayaona ingawa jana (juzi) usiku yalikuja na wengine waliondoka,” alisema.
DARAJA LASOMBWA, 5,000 WAKWAMA SAME
Zaidi ya mamia ya abiria waliokuwa wanasafiri kutoka eneo la Kisiwani kwenda maeneo mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, wamekwama kuendelea na safari, kutokana na daraja la eneo la Mzimbo katika kijiji cha Nkonga Ijunyi, Kata ya Kisiwani wilayani Same kusombwa na maji.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Kisiwani, Simba Jaffet, alisema mvua kubwa ambayo ilinyesha kwa usiku mzima, iliambatana na upepo mkali imesababisha madhara makubwa kwenye kata hiyo.
“Mvua iliyonyesha kwenye eneo letu hata wazee wa zamani wanasema hawajawahi kuona mvua kubwa kama hii. Imeharibu daraja, maji ya mafuriko yalikuwa mengi sana na sasa magari yameshindwa kusafiri na abiria waliotoka maeneo ya mlimani wameshindwa kuendelea na safari zao,” alisema.
Alisema pia mvua hizo, zimeharibu mashamba ya mpunga na mazao mengine na hivyo wananchi kuwa katika hatari ya kukosa chakula.
Diwani wa Kata hiyo, Salim Tenga, alisema mafuriko hayo yamesababisha magari kushindwa kuendelea na safari.
maeneo ya milima na kwmaba maji mengi yanateremka kutoka mlimani.
BARABARA KITONGA HATARINI
Sehemu ya Kitonga katika Barabara kuu ya TANZAM yenye urefu wa zaidi ya mita 200 iko katika hali mbaya kutokana na uharibifu wa mvua.
Hofu hiyo imeelezwa na Mhandisi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Iringa, Daniel Kindole, alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa wameanza kuchukua hatua za dharura za awali ambazo ni kuzuia uharibifu zaidi.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuzuia magari kupita eneo lililouthirika na madereva kutakiwa kufuata alama zilizowekwa kwa dharura.
Alisema kipande hicho cha barabara cha matengenezo hakitafunguliwa hadi hapo matengenezo makubwa yatakapo fanyika chini ya ujenzi wa Kampuni ya Ghana Building Contractor.
NIPASHE ilitembelea eneo la tukio na kushuhudia magari yakiwa yamesimama na kupita kwa zamu kutokana na barabara hiyo kufungwa upande mmoja ulioathirika.
Dereva aliyejitambulisha kwa jina moja la Sila, alisema serikali inatenga fedha kwa ajili ya barabara, lakini matokeo yake yanaweza kuwa ni malipo ya awamu na kufanya utekelezaji wake kuwa mgumu na wa kusuasua na matokeo yake ni hayo.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Iringa, Paul Lyakurwa, alisema kutokana na uharibifu huo, ofisi imejipanga kuhakikisha kunapatika njia sahihi ya kutatua tatizo hilo.
TMA: MVUA HAZIJAWAHI KUNYESHA TANGU MWAKA 1956
Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mvua zinazonyesha ni kubwa na hazijawahi kunyesha tangu mwaka 1956.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Kijazi alisema mvua zilizonyesha juzi zilikuwa ni milimita 60 na za jana zilikuwa ni milimita 156 na kufanya jumla ya mvua hizo kuwa milimita 216.
Alisema mvua hizo zimesababishwa na kuongezeka kwa msukumo wa hewa yenye unyevunyevu na makutano ya upepo katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na kisiwa cha Unguja ambapo hali hiyo itaendelea hadi leo.
Dk. Kijazi alisema mvua za kawaida ambazo hazitakuwa na madhara zitaendelea kunyesha kuanzia kesho.
Alisema maeneo mengine yatakayokumbwa na kiwango cha juu cha mvua ni pamoja na Nyanda za juu Kusini, inayohusisha Mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa, Kanda ya Kati, Dodoma na Singida na Kanda ya Magharibi, Kigoma na Tabora.
“Tunawasihi wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki kuelekea kipindi cha sikukuu ya krismas na mwaka mpya kwa kuwa mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuimarika kwa hali ya joto la Bahari ya Hindi sambamba na kuongezeka kwa msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)” alisema Dk. Kijazi.
Aliongeza: “Kulingana na viwango vya mvua zilizonyesha katika kipindi kifupi ongezeko kidogo la mvua katika mikoa hiyo linatarajia kuendelea kusababisha mafuriko na uharibifu wa Miundombinu… mamlaka inashauri tahadhali stahiki ziendelee kuzingatiwa.”
Alisema TMA itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na athari zake ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na tahadhari kila inapobidi.
Imeandikwa na Richard Makore, Hellen Mwango, Muhibu Said, Beatrice Shayo, Omar Fungo, Moshi Lusonzo, (Dar); Jacqueline Massano, (Dodoma); Ahmed Makongo, (Bunda); Salome Kitomari, (Same)
No comments:
Post a Comment