Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi mradi wa umeme unaotumia nishati ya upepo katika Chuo cha Ualimu Rukwa (Rukwa Teachers Collage). Mradi huo wa Umeme umebuniwa na mjasiriamali kutoka Rukwa wa Kampuni ya Ulaya Hydro and Windmill Technology.
Mradi huu wa umeme utatumika katika chuo hicho cha ualimu kwa shughuli mbalimbali ikiwemo chumba cha kompyuta, mabwenini na madarasani. Mkuu huyo wa Mkoa alifarijika na kutoa ushauri kwa wajasiriamali kuonyesha uwezo wao kwa kubuni miradi mbalimbali ambayo ina manufaa ya moja kwa moja kwa jamii.
Sehemu ya mtambo huo wa kuzalishia umeme. Mtambo huu una uwezo wa kuzalisha umeme wenye kilowatts tatu (3)
Chuo cha Ualimu Rukwa kinamilikiwa na Asasi isiyo ya kiserikali ya wanawake kutoka Rukwa iitwayo RUWAA (Rukwa Women Advancement Association); Taasisi ya Kuwaendeleza Wanawake Rukwa. Mwaka 2010 taasisi hii ilipewa Zawadi ya kuwa asasi bora kitaifa katika kuonyesha mchango wake wa maendeleo nchini. Picha juu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya akionyesha kikombe asasi hiyo ilichopewa katika ushindi wao huo, Mkuu huyo wa Mkoa aliguswa na maendeleo ya Kikundi hicho na kusema kuwa ni mfano wa kuigwa na kuwaasa wanawake wengine kuwa na umoja kwa kujijenga kijasiriamali na kuwekeza katika miradi inayotoa faida kwao na jamii kwa ujumla.
Mhe. Injinia Manyanya akihutubia wahitimu, waalimu na wageni waalikwa katika ukumbi wa chuo hicho. Katika hotuba yake hiyo alizitaka Asasi za Rukwa zijikite zaidi katika kutatua matatizo ya kijamii hasa tatizo la ajira, na isiwe kama asasi nyingine nyingi zinazojihusisha na mitazamo ya kinadharia. Alizitaka pia asasi hizo kuanzisha programu zinazoendana na mazingira na mahitaji ya jamii zetu.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo alijumuika na wahitimu kufurahi kwa kucheza muziki
Burudani ya Ngoma za asili pia zilikuwepo kutumbuiza. Kikundi cha sanaa cha Kanondo kutoka Wilayani Sumbawanga kikifanya kazi yake
Mhe. Mkuu wa Mkoa alichangisha fedha kwa ajili ya kumalizia miradi mbalimbali chuoni hapo. Alifanikiwa kuchangisha jumla ya Shilingi Millioni 1.18 ikiwa ni Fedha taslim pamoja na ahadi. Kati ya fedha hizo mwenyewe binafsi alitoa ahadi ya Shillingi Laki tano ambazo ameahidi kuzilipa ifikapo Ijumaa ya wiki hii.
Risala ya wahitimu kwa Mgeni rasmi. Kilio chao kikubwa ilikuwa ni ajira juu yao kuondoa tatizo la uhaba wa waalimu nchini.
Mgeni rasmi alikabidhi pia vyeti kwa wahitimu. Jumla ya wahitimu 109 wamehitimu mafunzo ya Ualimu wa Elimu ya Awali katika Chuo cha Ualimu Rukwa. Chuo cha Ualimu Rukwa kinatoa mafunzo ya ualimu katika ngazi ya Elimu ya Awali, Grade A na Certificate. Dira ya Chuo hicho ni kuwa Chuo Kikuu siku za usoni.
No comments:
Post a Comment