NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
22/12/2011
WAZIRI wa Ujenzi ,Dk. John Magufuli amewataka mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) wa mikoa nchini kutengeneza barabara ili ziweze kupitika na kuacha kisingizio cha sababu ya mvua.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri Magufuli katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri wa haraka wa mabasi jijini Dares Salaam wa awamu ya kwanza wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alitolea mfano wa mkoa wa Iringa. “Sitaki kuona barabara inayosimama kwa sababu ya kusingizio cha mvua. Ni wajibu wao kuona barabara zote zinapitika,” alisema Waziri Magufuli huku akisema fedha za mfuko wa barabara zipo wakandarasi na mainjia wapo. Waziri Magufuli alitolea mfano pia barabara ya Mwenge hadi Tegeta, Mandela eneo la Kitunda zilizopo katika jiji la Dares Salaam ambapo alisema alitaka wakandarasi husika wapewe maelekezo ili waweze kutengeneza barabara hizo kwa kuwa ni jukumu lao.
Wakati huohuo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Patrick Mfugale ambaye alitia saini katika mkataba huo na Meneja Mkazi wa kampuni ya Strabag kutoka Ujerumani, Heribert Schippers, ambayo ndiyo mkandarasi mradi huo alisema ujenzi wa awamu ya kwanza utagharimu sh. 240. 87 unahusisha ujenzi wa barabara wa kilometa 20.9 katika barabara ya Morogoro , kutoka Kimara hadi Kivukoni Feri. Eneo jingine ni barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi Morocco na barabara ya Msimbazi kutoka Fire hadi Makutano ya barabara ya Nyerere. Aliongeza kuwa ujenzi huo utachukua kipindi cha miaka mitatu.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka(DART) , Cosmas Takule alizitaja changamoto zinazoukabili mradi huo kuwa ni kesi ya wakazi wa Gerezani ya tangu mwaka 2008 ambayo imekwamisha ujenzi wa fungu la tano na ujenzi wa miundombinu, hivyo kukwama wa eneo hilo kunatishia uhai wa mradi kwa kuwa linakutanisha awamu tatu muhimu. Alizitaja Changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wananchi kufungua kesi kwa madai ya kutaka nyongeza ya fidia na ufinyu wa bajeti ya wakala ambao unakwamisha utekelezaji wa masuala mengine ya msingi katika kufanikisha mradi huo.
Katika hatua nyingine Waziri wa Uchukuzi ,Omari Nundu , Waziri wa Miundombinu wa Uganda Dk. Chebrot Stephen na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya China Civil Engineering Constraction Corporation (CCECC EAST AFRICA LIMITED), Wang Xiang dog leo(jana) wametia saini mkataba ya utafiti wa kina wa mradi wa ujenzi wa reli na bandari mpya.
Utafiti huo utakagharimu dola za marekani milioni 450 utafanywa na kampuni hiyo,ambapo. Mradi huo utahusisha ujengaji wa reli kutoka Tanga- Musoma- Arusha zikiwemo bandari mpya.Fedha za utafiti huo zimetolewa na Tanzania, ambapo utafiti huo utafanyika kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita
No comments:
Post a Comment