KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday 29 June 2012


Pinda ayumba tena
•  KIPIGO CHA ULIMBOKA CHAMTESA

na Martin Malera, Dodoma

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda kwa mara nyingine tena jana katika hali isiyotarajiwa na wengi, aliyumba na kushindwa kutoa tamko zito kuhusu mgomo wa madaktari kinyume na alivyokuwa ameahidi mbele ya Bunge juzi mjini Dodoma.
Pamoja na kushindwa kwake, Pinda pia alijikuta katika wakati mgumu kuelezea ukweli wa kile kinachodaiwa kuhusika kwa serikali katika tukio la kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Steven Ulimboka.
Akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA), katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu, ambaye alitaka kujua hatua ya serikali ya kutotoa tamko wakati juzi alitoa kauli nzito ya ‘liwalo na liwe’ kuhusu mgomo wa madaktari na kuibua hofu kubwa kwa wananchi, serikali inalieleza nini taifa kuhusu hali hiyo na inafanya nini kumaliza mgomo huo.
Akijibu swali hilo, Pinda kwanza alikiri kuahidi kutoa tamko la serikali akitumia neno la “liwalo na liwe’, lakini akadai kuwa serikali haitaweza kutoa tamko hilo tena baada ya kupata ushauri wa kisheria kwa kuwa jambo hilo liko mahakamani.
“Kwa bahati mbaya sana kauli yangu ya ‘liwalo na liwe’ imetafsiriwa kwa namna tofauti. Hata dada yangu Halima Mdee nilimsikia akitilia shaka kauli hiyo na kuhusisha na tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka.
“Nilichoaminisha ni kwamba hili jambo liko mahakamani, lakini tungetolea tamko la serikali bila kujali kwamba suala hilo liko mahakamani; ndiyo maana nikasema liwalo na liwe.’
Alisema baada ya mashauriano na wataalamu wa serikali jana usiku waliona si vyema kuendelea na tamko hilo hadi kesi iliyopo mahakamani itakapomalizika.
Kuhusu tukio la kutekwa, kupigwa kwa Ulimboka, Waziri Mkuu Pinda alisema serikali imeguswa na kushtushwa na tukio hilo, na akadai kuwa amesikitishwa na kuwepo kwa taarifa zinazoituhumu serikali kuhusika na unyama huo.
Waziri Mkuu aliliambia Bunge kuwa madai hayo ya kuituhumu serikali yanashangaza kwa sababu, yeye mwenyewe alipata taarifa ya kufanyiwa vitendo hivyo akiwa bungeni na hata wakati alipoahidi kutoa tamko la serikali hakuwa anajua chochote.
“Dk. Ulimboka tumekuwa naye kwenye vikao vya ndani vya majadiliano, tuko naye mahakamani. Leo serikali ihusike kumteka, kumpiga na kumtesa kwa kiasi kile ili iweje?”
Alisema Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, ameshatoa kauli juu ya tukio hilo, hivyo alisisitiza kuwa serikali itafanya uchunguzi wa kina kuwanasa waliohusika.
Akijibu swali la nyongeza la Mbowe aliyetaka kujua hatua za dharula zilizochukuliwa na serikali kumaliza mgomo huo hasa baada ya kusitisha tamko lake Bungeni, Pinda alisema serikali itaendelea na majadiliano na madaktari hao ili kufikia muafaka.
“Hatua nyingine ya dharura tuliyochukua serikali ni kuzungumza na Hospitali ya Lugalo na zingine ndogo kubeba jukumu hilo kwa sasa, pia tumeagiza madaktari wastaafu wote warejee kazini katika kipindi hiki cha mgomo,” alisema Pinda.
Lissu amtaka ajiuzulu
Majibu ya Pinda yalimkoroga Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliyesimama na kumuuliza sababu gani zinazomfanya aendelee kushikilia wadhifa wake huku akitambua kuwa ameshindwa kumaliza mgogoro huo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Februari mwaka huu wakati wa mgomo wa madaktari uliahidi kwamba mgomo huo hautatokea tena, leo mgomo umerudi tena, je, kwa nini usijiuzulu?” alihoji Lissu.
Pinda alidai kuwa tangu kuanza kwa mgogoro huo, amefanya jitihada za kutosha kujaribu kuunusuru na kwamba anaamini amefanya kazi kubwa kuufikisha hapo ulipo.
Hata hivyo, Lissu alisimama na kumwambia Waziri Mkuu, kwamba hapo alipoufikisha ni pabaya zaidi na haoni sababu ya yeye kuendelea kuwepo madarakani, kauli iliyoonekana kumkera Pinda ambaye alidai kuwa yapo mambo ambayo yanaweza kumfanya akajiuzulu, lakini sio katika sakata la mgomo wa madaktari.
“Mheshimiwa Lissu hii sio lugha nzuri ya kusema, nakuheshimu sana,” alisema Pinda na kuzima swali hilo.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlacha (CCM), alihoji endapo serikali inajua kama kuna kikundi cha watu kinachochochea mgomo huo kwa kuwapa fedha. Akijibu hoja hiyo, Pinda alikiri kupata taarifa hizo na akadai kuwa serikali inafanya uchunguzi kubaini ukweli, ikiwa ni kweli wahusika watachukuliwa hatua.
Juzi Pinda aliahidi kutoa kauli ya serikali wakati akijibu mwongozo Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Dhambi (CCM), aliyetaka kujua msimamo kuhusu mgomo wa madaktari.
Madaktari waikataa Tume ya Polisi
Jumuiya ya Madaktari Nchini imesema haina imani na tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuchunguza unyama aliofanyiwa Dk. Ulimboka huku wakisisitiza kuwepo kwa chombo huru zaidi.
Licha ya kutaka tume huru, madaktari hao wamesema wataendelea na msimamo wao wa kuhakikisha wanatetea maslai yao pamoja na mazingira magumu ya kufanyia kazi yanayowakabili kwa sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la MOI Katibu wa Jumuiya hiyo Dk. Edwin Chitage alisema madaktari nchini wanahitaji chombo kilicho huru kitakachochunguza tukio hilo kwa undani zaidi kuliko Jeshi la Polisi.
Alisema hawana imani na tume hiyo kwa sababu si huru; wanataka chombo kitakachopatikana kwa utaratibu unaoeleweka, kuliko polisi hasa wakizingatia mazingira ya kutekwa na kupigwa kwa mwenzao ingawa hawawezi kusema kama jeshi la polisi linahusika.
“Tutaendelea kupigania masuala ya mazingira bora ya kazi kwani hatufurahii kuona msongamano wa wagonjwa wodini, mgonjwa akilala chini, watoto wachanga kulala zaidi ya watano kitanda kimoja na kukosekana kwa dawa na vifaatiba,” alisema.
Awali aliwataka madaktari wote nchini kuwa watulivu hasa katika kipindi hiki kigumu na kusisitiza kwamba tukio hilo limewaimarisha na kuwazidishia mshikamano.
Afya ya Ulimboka yaimarika
Hali ya afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Dk. Steven Ulimboka inaendelea kuimarika licha ya maumivu makali yanayomkabili.
Akizungumza kwa taabu na waandishi wa habari kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kwenye Kitengo cha Mifupa (MOI) Dk. Ulimboka alisema, “Namshukuru Mungu naendelea vizuri tofauti na nilivyofikishwa hapa jana…bado nina maumivu makali naomba kama kuna watu wanataka kuja kuniona wasije ili nipumzike,” alisema.
Awali Ofisa Uhusiano wa MOI Jumaa Almas alisema hali ya Dk. Ulimboka inaendelea vizuri tofauti na alivyoletwa juzi asubuhi kwa kuwa sasa ana uwezo wa kutambua watu wanaofika kumjulia hali na kuzungumza kidogo.
Almas alisema madaktari wameshauri mgonjwa huyo kupumzika na kutaka idadi ya watu wanaofika kumjulia hali mgonjwa huyo ipungue ili kumwepusha na maambukizi zaidi.
“Kwa sasa hali yake ni nzuri na yuko chini ya uangalizi wa jopo la madaktari linaloongozwa na Profesa Joseph Kahamba,” alisema.
Kuhusu mgomo katika kitengo hicho Almas alisema ni huduma za dharura pekee zinazotolewa huku zile za kawaida zikiwa hazifanyiki kabisa.
Dk. Ulimboka alifikishwa hospitalini hapo baada ya kutekwa na watu wasiojulikana kisha kumpiga, kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kutupwa kwenye msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo ambaye amekuwa akiratibu mgomo ya madaktari unaoendelea, aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono akiwa amejeruhiwa vibaya.
Vyama vyaendelea kulaani
Kutoka mkoani Mwanza, Sitta Tumma anaripoti kuwa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti nchini (RAAWU), Kanda ya Ziwa, kimelaani vikali kitendo cha kinyama cha kupigwa na kuumizwa vibaya, alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka, na kuelekeza tuhuma hizo kwa serikali.
RAAWU imesema, ushahidi wa mazingira unaonyesha dhahiri kwamba serikali imehusika kwa namna moja au nyingine kumdhuru kiongozi huyo wa madaktari nchini, ikiwa ni lengo la kutaka kuzima mgomo wa madaktari unaoendelea katika kudai maslahi na huduma bora ya matibabu kwa Watanzania.
Katibu wa RAAWU Kanda ya Ziwa, Ramadhan Mwendwa, ameiambia Tanzania Daima ofisini kwake kuwa kuna haja ya serikali kujisafisha kwa sababu mazingira ya tukio hilo yanaiweka katika hali ya kutuhumiwa.
Mwendwa ambaye pia ni Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Mkoa wa Mwanza, alizidi kudai kuwa manyanyaso na ukandamizwaji mkubwa unaofanywa na serikali vinaonyesha wazi kwamba viongozi wa Tanzania wanawapeleka wananchi wao katika machafuko.
“Tusifike huko kama nchi nyingine zinavyopigana. Viongozi wa wafanyakazi tuweni wamoja na wafanyakazi wote katika kutetea maslahi ya taifa. Tusirudi nyuma,” alisema Mwendwa.
CUF, CHADEMA wanena
VYAMA vya CUF na CHADEMA, vimelaani kitendo cha kutekwa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, huku vikiitaka serikali kuunda tume huru ya uchunguzi.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Benson Kigaila, alisema kuwa kitendo hicho ni jitihada za serikali kuwanyamazisha watetezi wa maslahi ya umma.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alisema hizo ni dalili za wazi za serikali ya CCM kushindwa kuhimili demokrasia ya wengine.
“Tumeshuhudia hali hii ikiwakumba wengi, kumbukeni tukio la mhariri wa Mwanahalisi Sued Kubenea kumwagiwa tindikali, mauaji ya Masudi Mbwana kule Igunga na hata kuuawa kwa mwenyekiti wa CHADEMA kule Arumeru ni katika njia za kutaka kuwanyamazisha na kuwatisha wengine,” alisema Kigaila.
Alisema katika mgomo wa kwanza wa madaktari Rais Jakaya Kikwete aliuhakikishia umma kuwa watayashughulikia matataizo ya madaktari na kwamba suala la mgomo kwao litakuwa ni ndoto.
Kwa upande wao CUF, kwa mujibu wa wa Naibu Mkurugenzi wa Itikadi na Uenezi, Abdul Kambaya, walilitaka jeshi la polisi kuacha kuchunguza tukio hilo kutokana na kutolitilia maanani tangu awali lilipopewa taarifa.
Akizungumza jana na Tanzania Daima, alisema kuwa kitendo alichofanyiwa Dk. Ulimboka ni aibu kwa taifa kwa kushindwa kufanya ulinzi wa viongozi na watu wake.
Alisema uchunguzi huo wa tukio unatakiwa kufanywa na taasisi zingine huru ili kutoa majibu sahihi kwa wananchi lakini si jeshi la polisi.
“Serikali haiwezi kujitoa katika tukio hili la kinyama alilofanyiwa Dk. Ulimboka hasa ukizingatia ni katika kipindi kifupi ambacho madaktari wako kwenye mgomo na huyu ni kiongozi wao,” alisema Kambaya.

No comments:

Post a Comment