KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Wednesday, 23 May 2012


Makao Makuu Ya Benki Ya Azania Kuhamia Mawasiliano Towers

UONGOZI  wa benki ya Azania umeridhia uhamisho wa makao makuu ya benki hiyo kutoka Masdo House, mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam kwenda jengo la Mawasiliano Towers iliyopo mkabala na barabara ya Sam Nujoma kuanzia Jumatatu wiki ijayo kwa lengo la kuwatumikia wateja wa benki hiyo katika mazingira yenye nafasi ya kutosha.

Hata hivyo, tawi la Masdo litaendelea kuwahudumia wateja waliopo katikati ya Jiji huko makao makuu mapya ya benki hiyo yaliyopo Mawasiliano Towers yakitoa huduma za kibenki kwa maeneo yaliyopo karibu na Ubungo, Mwenge ,Sinza na mengineyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa benki hiyo kwa vyombo vya habari jana, benki ya Azania itaendelea na mpango wake wa kujiimarisha zaidi kwa kuendelea kufungua matawi zaidi nchini ikiwa na lengo la kusogeza huduma za kifedha karibu na watu na pia kuhakikisha usalama kwa pesa zao.

Kupitia taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Charles Singili alisema benki yake ipo mbioni kufungua tawi jingine jipya katika Wilaya ya Geita na maeneo mengine yakiwemo Lamadi, Katoro na Kagongwa ifikapo mwisho wa mwezi ujao, hatua ambayo itasaidia kuimarisha uwepo wa benki hiyo katika kanda ya ziwa.

 "Tunatarajia kufungua matawi mengine zaidi nchi nzima ifikapo mwisho wa mwaka huuambayo yatasaidia benki yetu kuwa kitovu cha huduma za kifedha kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini.

“Tangu benki ifunguliwe mwaka 1995, benki imekuwa haraka hali ambayo imesababisha mali za kampuni kufikia shilingi bilioni 190 mwishoni mwa mwaka 2011,” alisema Singili.
Singili aliongeza kuwa benki yake imelenga zaidi katika kutoa huduma za kibenki za kipekee kwa bei nafuu ukiilinganisha na mabenki mengine.

 “Nawahakikishia kwamba tutaendelea kutoa huduma za kipekee zinazokidhi mahitaji ya kila mteja wetu kwa upekee wake. Katika miezi sita iliyopita benki imejikita katika mpango madhubuti wa kujitanua kwa kufungua matawi matatu katika maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam, Arusha mjini katika barabara ya Wapare na mtaa wa sokoni jijini Moshi,” alisema.


 "Ninawaomba wateja wa benki ya Azania wa sasa na umma kwa ujumla kuendelea kupata huduma mbalimbali za kibenki na huduma zinazotolewa na benki hii ya Kitanzania yenye mafanikio," alisema.

Benki ya Azania iliaanzishwa mwaka 1995 kama  Adili Bancorp Limited baada ya Serikali kuruhusu mfumo wa uchumi wa soko huria  na kwa sasa benki hiyo ina wanahisa wakuu wakiwa pamoja na mashirika ya serikali yakiwemo, National Social Security Fund (NSSF) 34.8%, Parastatal Pensions Fund (PPF) 30.1%, Public Service Pensions Fund (PSPF) 17.2%, Local Authorities Pensions Fund (LAPF) 14.2%, na mengine.

No comments:

Post a Comment