CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeanza kukunjua
makucha yake dhidi ya Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda, ambaye
amekuwa na uhusiano tete na chama chake hicho, huku akikishambulia
hadharani na kujipendekeza kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bila kificho.
Baada ya kuwa anatoa kauli za kukishambulia chama hicho hadharani bila
kuchukuliwa hatua, juzi Shibuda aliibukia katika kikao cha Halmashauri
Kuu ya CCM, Dodoma akavishambulia vyama vya upinzani na kukisifia CCM,
akisema ndicho chenye uwezo wa kutawala, kwani vingine vyote bado
havijastahili kukabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi.
Hata hivyo, alijikanganya mwenyewe alipotamka kuwa anatarajia kugombea
urais kupitia CHADEMA; na akamwomba Rais Jakaya Kikwete awe meneja wake
wa kampeni mwaka 2015.
Baada ya kauli hizo kuvuja na nyingine kuandikwa na vyombo vya habari,
jana Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) lilitoa tamko kali likisema:
“Vijana wote wa CHADEMA sasa tujiandae kikamilifu katika kukabiliana na
mtu yeyote yule ambaye ataonekana kuwa kikwazo kwa chama chetu,
matumaini na masilahi ya Watanzania kwa ujumla wake katika kuelekea
kuchukua dola mwaka 2015.”
Katika tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John
Heche, CHADEMA kinasema kimeshtushwa na kauli ya Shibuda kusema kuwa
vyama vya upinzani havina uwezo wa kutawala, huku akitaka kugombea urais
kupitia chama hicho.
Vile vile, vijana hao wa CHADEMA walishangazwa na mbunge huyo
kutangaza nia yake kupitia vikao vya CCM na kuomba msaada kwa Rais
Kikwete, huku akijua kuwa CHADEMA kina vikao na taratibu zake katika
masuala kama hayo.
Kwa msisitizo, BAVICHA ilisema: “Tunapenda kumwambia kuwa kama anaona
kuwa yeye haendani na utamaduni wa chama chetu na anakiona kuwa hakina
uwezo wa kuongoza dola anafanya nini kwenye chama ambacho anaona kuwa
hakiwezi kuongoza dola? Kwanini atafute urais kwenye chama ambacho
anaona hakiwezi kuongoza dola? Anawatania Watanzania?
“Ni heri akaenda kwenye hicho ambacho anaamini kuwa kinaweza kuongoza
dola, kwani lengo la chama chochote kile ni kuchukua dola na si
vinginevyo. “Tunapenda kuwahakikishia vijana wote wa Tanzania na
wananchi kwa ujumla kuwa tayari CHADEMA kimejiandaa kikamilifu kuongoza
dola na wasiwe na hofu na maneno yaliyotamkwa na mbunge huyu.”
Kwa sababu hiyo, Heche alisema BAVICHA itaitisha kikao cha Baraza lao
kujadili kauli ya Shibuda na kuwasilisha mapendekezo kwenye vikao halali
vya chama, ili hatua mwafaka zichukuliwe dhidi yake.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya kikao cha CCM tangu
juzi zinasema Shibuda, ambaye alihama CCM na kujiunga CHADEMA mwaka
2010, alivishambulia vyama vya upinzani, kiasi cha kuwaacha midomo wazi
Wana CCM wenyewe.
Mmoja wa vigogo wa CCM waliozungumza na gazeti hili juzi usiku alisema
kwamba baadhi ya maneno aliyotumia Shibuda dhidi ya CHADEMA yalikuwa
makali kiasi kwamba hata katika mikanda yao ya video wanazotumia kwa
matangazo ya vyombo vyao vya habari, ilibidi wayahariri au kuyakata.
Baadhi ya Wana CCM wanaomfahamu vema Shibuda walisema kwa vyovyote
vile Shibuda bado ni Mwana CCM aliyetafuta hifadhi CHADEMA kwa ajili ya
kupata ubunge baada ya kuenguliwa na CCM.
Wengine walikwenda mbali na kusema hata kuenguliwa kwake na CCM
ulikuwa mkakati mahususi wa Rais Kikwete kupenyeza watu wake katika
CHADEMA, hasa ikizingatiwa historia ya mbunge huyo mwenye kuhusishwa na
ukachero wa kisiasa.
Mmoja wa Wana CCM hao ambaye hayumo kwenye kambi ya Rais Kikwete ndani
ya makundi hasimu ya CCM, alisema si kazi ngumu kwa serikali ya Kikwete
kutumia pesa za walipa kodi kwa “kazi chafu kama hiyo.”
Baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa na harakati za Shibuda
wanadai kwamba uhai wa mbunge huyo ndani ya CHADEMA ulidumu hadi siku ya
kutangaza matokeo ya ubunge wake. Baada ya hapo amekuwa akiwashutumu
viongozi wenzake hadharani hata katika kuchangia hoja za bungeni.
Katika matukio kadhaa, Shibuda amenukuliwa akisema viongozi wa CHADEMA
ni “wachanga na wanaharakati” na kwamba wanapaswa kuvuna uzoefu wa
kisiasa kutoka kwake kwa sababu ni “mzee, mkongwe na mzoefu.”
Hata hivyo, baadhi ya wabunge vijana, ambao yeye amezoea kuwaita
“watoto” waliwahi kumweleza kuwa uzoefu anaojidai nao Shibuda ni wa
siasa za CCM, si wa siasa za upinzani; wakasema kama ni kujifunza yeye
ndiye alipaswa kujifunza kwao waliofanya siasa za mageuzi kwa zaidi ya
miaka 18.
Amefika mahali pa kutofautiana na chama chake katika masuala muhimu ya
kisera, likiwamo suala la posho nono za watendaji wa serikali na
wabunge. Wakati CHADEMA kikisema posho hizo ama zifutwe au ziingizwe
rasmi kwenye mfumo wa malipo ya wafanyakazi wote, Shibuda amekaririwa
mara kadhaa akisema posho ni ujira wa mwira, ambao ni halali kwao, na
kwamba hazitoshi.
Baadhi ya Wana CHADEMA wamekuwa wakisitiza kuwa Shibuda alitumwa
kukisambaratisha chama chao, lakini kwa utamaduni na mkakati wa
kiuongozi ndani ya CHADEMA, hawezi kufurukuta, maana walitambua nia yake
hata kabla hajaanza kuwashambulia.
Hata hivyo wapo wanaotaka afukuzwe chama ili kutoa funzo kwa viongozi
wengine wa chama hicho wanaotaka kuleta chokochoko, huku wengine
wakisema apewe muda anaweza kujirekebisha. Wapo pia wanaodhani kwamba
Shibuda “si lolote, si chochote” ndani ya CHADEMA, na kwamba haki
anayostahili ni kupuuzwa tu, maana wananchi walishamtambua.
Hata katika jimbo lake, aliwahi kususa baadhi ya matukio ya chama
kilipokuwa kinafanya ‘Operesheni Sangara’ katika mikoa ya Kanda ya Ziwa
mapema mwaka jana, lakini wananchi waliitikia vema na kuendelea bila
Shibuda; jambo ambalo linasemekana kumshtua.
Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya wabunge wa CHADEMA walidai
kuwa Shibuda ameanza kujirekebisha, maana anashiriki katika baadhi ya
mipango na mbinu zao dhidi ya CCM. Wanadai kwamba Shibuda alianza
kushtuka walipofukuzwa madiwani watano wa CHADEMA Arusha kwa utovu wa
nidhamu.
Sababu halisi za Shibuda kuwabeza viongozi wa chama chake hazijawekwa
hadharani, lakini wachunguzi wa mambo wanasema uhusiano mbaya kati yake
na chama ulianza mwaka 2010 kabla ya uchaguzi alipoomba apewe fedha za
kampeni akanyimwa.
“Nasikia alimwendea mwenyekiti (Freeman Mbowe) akamwomba msaada wa
pesa kwa ajili ya uchaguzi. Mbowe alichomwambia Shibuda ni kwamba chama
hakina pesa za kuwapa wagombea waliokuwa wabunge kama yeye, na kwamba
kama zingekuwapo wangeombwa kusaidia vijana na wengine waliojitokeza
kugombea ubunge.
“Wakati huo, chama kilikuwa kinahaha kupata fedha za kampeni za urais,
na Mbowe mwenywe alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Hai. Shibuda
alipoambiwa kwamba hakuna pesa, aliondoka akisema maneno mabaya dhidi ya
viongozi; na hajawasamehe hadi leo,” alisema ofisa mmoja wa CHADEMA
ambaye alidai kujua siri hiyo.
Ofisa huyo alisisitiza kwamba kama si uvumilivu binafsi wa Mbowe na
wazee wengine, Shibuda angekuwa amefukuzwa chama miezi kadhaa iliyopita
kwa sababu hana mchango wowote wa maana anaokipa chama chake.
Badala yake, baadhi ya wanachama na viongozi wenzake wanasema amegeuka mzigo, na “kashfa” kwenye chama.
Iwapo hatua hii ya Bavicha itazingatiwa na vikao vya juu, na iwapo
Shibuda hatabadilika, upo uwezekano mkubwa kwake kufukuzwa uanachama na
ubunge kabla ya mwaka 2015.
Baadhi ya Wana CHADEMA wanadai asipojihadhari hata huo urais anaouota
hatapata fursa ya kuugombea akiwa CHADEMA, kwani anaweza kuwa amefukuzwa
chama.
No comments:
Post a Comment