KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 3 November 2011

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Maalim Seif Akutana na Mwakilishi wa UNDP

 MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Maalim Seif Sharif Hamad akibadilishana mawazo na mwakilishi wa UNDP bibi Ana Barradas wakati ujumbe wa Shirika hilo ulipofika Ofisini kwake Migombani kujadiliana juu ya Tathmini ya uchaguzi mkuu uliopita.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akibadilishana mawazo na ujumbe wa UNDP uliofika ofisini kwake Migombani kutathmini juu ya hali ya uchaguzi uliopita.
--
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesifu ustaarabu na hali ya kuvumiliana iliyokuwepo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Amesema hali hiyo ilipelekea uchaguzi uliopita kufanyika kwa utulivu mkubwa na kuiletea sifa kubwa Zanzibar ambayo ilikuwa ikikumbwa na vurugu kila ifikapo kipindi cha uchaguzi.

Maalim Seif ameeleza hayo leo Ofisini kwake migombani mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP bibi ANA BARRADAS kuhusiana na tathmini ya shirika hilo kwa uchaguzi uliopita.


Amebainisha kuwa licha ya kuwepo mafanikio katika kipindi chote cha kampeni na uchaguzi kwa jumla, uchaguzi huo ulikuwa na kasoro ndogo ndogo ambazo zinapaswa kurekebishwa ili kujenga mazingira bora zaidi katika uchaguzi ujao.

Ametaja baadhi ya kasoro hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kutopata fursa ya kupiga kura kutokana na kukosa vitambulisho vya uzanzibari ukaazi pamoja na kutokuwepo na uwazi katika hatua za mwisho za kujuisha matokeo.

Amesema wakati umefika kwa taasisi zinazohusika kurekebisha kasoro hizo ili chaguzi zijazo zifanyike katika misingi ya uwazi na haki na kumfanya kila mmoja kuridhishwa na mchakato wa uchaguzi.

Akizungumzia hali ya siasa baada ya uchaguzi Maalim Seif amesema imepata mafanikio makubwa kwani vyama vya CCM na CUF vimekuwa vikifanya kazi kwa pamoja na kuweka kando tofauti zao katika kuangalia mustakbali wan chi.

“Mfano mzuri ni kuundwa kwa Jumuiya ya Maridhiano Zanzibar (ZAMA). Jumuiya hii inawahusisha vijana wa CCM na CUF na inafanya kazi vizuri sana kwa mashirikiano”, amedokeza maalim Seif.

Makamu wa kwanza wa Rais amelishukuru shirika hilo kwa kuunga mkono uchaguzi uliopita na kuliomba kutoa misaada yake mapema ili kurahisisha mchakato wa uchaguzi kuanzia hatua za awali na kuipelekea Zanzibar kuendesha chaguzi kwa misingi ya demokrasia ya kweli.

Amesema ipo haja kwa shirika hilo kusaidia elimu ya uraia hasa kwa wananchi wa vijijini, kwani wananchi wengi wa maeneo hayo wamekuwa wakikosa uelewa juu ya mchakato wa uchaguzi na kupelekea kuharibika kwa kura nyingi na kushindwa kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi.

Nae kiongozi wa ujumbe huo bibi ANA BARRADAS amesema ameridhishwa na hali ya siasa za Zanzibar baada ya uchaguzi, hali ambayo inafaa kuendelezwa kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa jumla.

Aidha ameahidi kuwa shirika litaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kufanikisha chaguzi za kidemokrasia nchini.
 
IMETOLEWA NA:

Hassan Hamad 
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment