Mussa Juma, Dodoma |
SERIKALI imeombwa kuwakamata mara moja, Meya ya Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Massaburi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam(Uda), Iddi Simba na wote waliohusika katika katika mchakato wa kuuza mali na hisa za Uda kinyamela.Licha ya kukamatwa, Serikali imeombwa kuzisimamia akaunti za watuhumiwa wote hadi hapo shauri lao litakapomalizika. Hoja ya kukamatwa mara moja kwa vigogo hao, pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uda, Victor Milanzi na maofisa wengine wa jiji, lilitolewa muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Joseph Serukamba na Msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni wa Wizara y Uchukuzi, ,Mhonga Ruhwanywa kutaka Takukuru na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kuingilia kati haraka kuchunguza sakata la kuuzwa shirika hilo. Mbunge wa Jimbo la Mafia (CCM),Abdulkarim Shah ndiye aliyewasha moto kwa vigogo hao,wakati akichangia ,Hotuba ya Waziri wa uchukuzi, Omar Nundu ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya mwaka 2011/12. Mbunge huyo, alisema ni aibu kuendelea kusikiliza jinsi Uda ilivyouzwa hisa na mali zake kihuni tena kwa fedha kupitia katika akaunti za watu binafsi.“Eti wanapitisha fedha kwenye akaunti ya mtu binfsi kwa maelezo kuwa Uda inadaiwa na benki, je ina maana hawa viongozi wanaibia mpaka benki”alihoji Shah. Shah alisema ni aibu Serikali kuendelea kukaa kimya wakati mali za Serikali zikiuzwa na akaitaka kuzisimamia mara moja akauti za watuhumiwa hao wakati uchunguzi wa suala hilo ukiendelea. “Ni aibu wameuza hadi eneo la maegesho ya magari ya Kurasini kiasi cha Sh1.4 bilioni, wameuza kiwanja pale Station,nyumba na mali nyingine”alisema Shah.Hata hivyo, aliunga mkono uamuzi wa kuzuiwa kutolewa hati mpya za umiliki wa viwanja vilivyouzwa na watendaji hao wa Uda. Awali, Serukamba akisoma taarifa ya Kamati ya Miundombinu, alisema Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeunda kamati ndogo ili kufuatilia sakata la Uda na taarifa ya ufuatiliaji wa kamati itatolewa katika mkutano wa tano wa Bunge. Kamati hiyo ya Bunge pia imeshauri Serikali kufanya tena mapitio ya mkataba wa mauzo ya hisa zilizogawiwa(unallocated shares) ulioingiwa kati ya Uda na kampuni ya Simon Group. “Kutokana na taarifa zilizowasilishwa kwenye vikao ,kamati imebaini utendaji wa Uda umeendelea kuzorota na kwamba kuna dalili za ubadhilifu wa mali na mapato ya shirika hili, kwa mfano mchakato wa kuendelea kuuza hisa za Serikali umeonekana kuwa na shaka", alisema Serukamba. Mwenyekiti huyo, pia alifafanua kuwa katika ubinafsishaji unaoendelea ,malipo yanaonekana kufanyika kwa kupitia kaunti yta watu binafsi.Kwa mujibu wa nyaraka za sakata hilo, zimebainisha kuwa aliyekuwa mwenyekiti wa bodi Idd Simba ndiye alipitishiwa katika akauti yake sehemu ya malipo ya mauzo ya hisa kiasi cha Sh300 milioni. Naye Msemaji wa upinzani, Mhonga Ruhwanywa, alisema mchakato wa kuuzwa hisa za Serikali za Uda, umekiuka taratibu na sheria kwani mbia muhimu Serikali hakuwahi kushirikishwa. “Bodi ya Uda bila kuhusisha Serikali (msajili wa hazina) zilipatikana taarifa kuwa hisa ambazo zilikuwa hazijagawiwa ziliuzwa kwa kampuni ya Simon Group hisa 7,880,000 kwa Sh1.142 bilioni kwa mkataba uliosainiwa Februari 11,2011. Akizungumza nje ya Bunge, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azzan aliungana na wabunge na kamati zote kutaka wahusika wa waliuza Uda kuwajibishwa. Mapema juzi, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Simon Group iliyouziwa Uda kwa kununua asilimiua 52 ya hisa, Robert Kisena alizungumza na wanahabari mjini hapa na kusisitiza wameuzwa hisa kihalali na tayari wamewekeza Uda Sh760 milioni na kwamba kiasi cha Sh500 milioni zitalipwa mwezi huu |
No comments:
Post a Comment