NI IWAPO UCHAGUZI MKUU UNGEFANYIKA SASA ANGESHINDA. Leon Bahati MATOKEO ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Synovate yanaonyesha kwamba iwapo Rais Jakaya Kikwete angeamua kujiweka kando na ukaitishwa Uchaguzi Mkuu sasa, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa angeibuka mshindi wa nafasi hiyo.Ripoti ya Synovate iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana ambayo inawapa wapinzani fursa ya ushindi kwa mara ya kwanza, wagombea kutoka vyama vya upinzani wana uwezo wa kupata asilimia 67 iwapo uchaguzi ungefanyika sasa. Dk Slaa anaongoza kwa kupata asilimia 42, akifuatiwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (asilimia 14), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (asilimia 12) na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe asilimia tisa. Synovate inaeleza kwenye ripoti hiyo kwamba matokeo ya utafiti huo yanatokana na watu mbalimbali wenye umri zaidi ya kuanzia miaka 18 walioulizwa maswali ya ana kwa ana vijijini na mijini. Katika kupata maoni juu ya mtu ambaye wangependa awe rais waliuliza: “Mbali na Rais Jakaya Kiwete, ni mtu gani ungeweza kumchagua kuwa Rais iwapo atakuwa miongoni mwa wagombea?” Kwa mujibu wa matokeo hayo, iwapo uchaguzi ungefanyika sasa, Pinda angeambulia nafasi ya tatu licha ya kwamba CCM ndicho chama kinachoongoza kwa kuaminika mbele ya umma ikilinganishwa na vyama vingine vya siasa.Katika utafiti wake huo uliofanywa kati ya Mei 2 hadi 29, mwaka huu, jumla ya watu 1,994 walihojiwa. CCM wamtaka Dk Slaa Utafiti huo unaonyesha kuwa wanachama wengi wa CCM walionyesha kuvutiwa na Dk Slaa ikilinganishwa na viongozi wengine ndani ya chama hicho tawala.Hii inatokana na takwimu kuonyesha kuwa kati ya waliohojiwa katika utafiti huo, wengi wanatokana na CCM, lakini wakamchagua Dk Slaa. Takwimu za ripoti hiyo zinaonyesha kuwa kati ya waliohojiwa, walipoulizwa kuhusu vyama vyao asilimia 51 walisema ni CCM, asilimia 35 wakasema Chadema, 10, CUF na TLP asilimia moja. Mbali na Dk Slaa, Profesa Lipumba, Pinda na Zitto wanasiasa wengine wanne wanaofuatia ambao asilimia walizopata zimo kwenye mabano ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (4), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (2) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (2). Kadhalika, vigogo tisa waliofungana kwa kupata asilimia moja ya kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya. Katika utafiti huo, Synovate iliegemea nyanja tatu za utafiti ambazo ni siasa, uchumi na masuala ya kijamii na utamaduni. Mgombea urais CCM 2015 Ndani ya CCM, anayepewa nafasi ya kwanza kuwa mgombea urais kwa mwaka 2015 ni Pinda aliyepata asilimia 35 akifuatiwa na Dk Magufuli asilimia 14. Wanaofuatia kwa mvuto pamoja na asilimia walizopata kwenye mabano ni Membe (8), Sitta (3), Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye (3), Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa (3) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi (2). Vigogo tisa ndani ya CCM walifungana kwa kupata asilimia moja nao ni Makinda, Dk Mwakyembe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Magembe na Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim. Wengine ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose Migiro, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba. Uvuaji gamba CCM Utafiti huo wa Synovate unaonyesha kuwa Watanzania wengi wanatofautiana juu ya uelewa wa mpango wa CCM wa kujivua gamba. Katika mpango huo ripoti hiyo inasema asilimia 41 walisema ni mpango wa kuwataka watu kujiuzulu kwenye uongozi wakati asilimia 29 walisema ni mpango wa kutaka kukisafisha chama. Inaonyesha kuwa asilimia 15 ya waliohojiwa walielezea kujivua gamba kuwa ni mabadiliko ya uongozi kwa kuondoa viongozi wabovu na asilimia tano wakasema ni mpango wa kuondoa viongozi wote watuhumiwa wa ufisadi. Asilimia mbili walisema ni mpango wa kukifanya chama hicho cha siasa kiwe na mfumo wa wazi na unaoeleweka wakati asilimia moja walisema ni suala la kujizuzulu, kutafuta viongozi wachapakazi na wenye tija. Kuna wanaouchukulia kuwa ni mkakati wa kisanii wa kuwadanganya wananchi. Kwa ujumla, taarifa hiyo ilisema ni asilimia 45 tu ambao wana taarifa kuwa kuna Sekretarieti ya CCM ilijiuzulu na Mwenyekiti wake, Rais Kikwete amekwishateua wengine kushika nafasi hizo. Kero kubwa nchini Asilimia 56 walisema tatizo kubwa linalowakumba ni kupanda kwa bei ya vyakula, gharama za maisha na umaskini na asilimia 46 walisema njaa na tatizo kwenye kilimo.Tatizo la ufisadi nchini lilichukua nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 36, ukosefu wa ajira (31), tatizo la nyumba, barabara na umeme (27), elimu (23), afya (21), maji (16), uharibifu wa mazingira (12), taasisi za siasa (10), haki za binadamu, uhalifu (6) ubeberu na usafirishaji wa dawa za kulevya (3). Katiba Mpya Miongoni mwa mambo ambayo yanatajwa kuwa ni vikwazo kwa Tanzania kupata Katiba Mpya ni rushwa (26), kukosekana kwa umoja (19), maslahi ya kisiasa (18), ufahamu mdogo (11) na kukosekana kwa msukumo wa kisiasa (9). Hata hivyo, asilimia 78 walisema wanataka yawepo mabadiliko ya katiba nchini wakati asilimia 21 hawaoni umuhimu wake.Lakini asilimia 42 walisema wana uhakika kwamba mpango wa Katiba Mpya utafanikiwa. Lakini pia makosa ya Katiba iliyopo yalielezwa kuwa ni kupitwa na wakati, kuandikwa kwa Kiingereza zaidi kuliko Kiswahili, kukosekana kwa utawala bora, kutokuwepo kwa sheria za haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari. |
KARIBUNI
Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.
Wednesday, 3 August 2011
Dk Slaa ang’ara urais
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment