KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday, 18 August 2011

Mchungaji Peter Msigwa:Tuna ushahidi kuwa,Pius Msekwa.......................

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Mzee Pius Msekwa
---
BUNGE limeendelea kuwa chungu kwa vigogo CCM, baada ya Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Pius Msekwa (pichani) kutuhumiwa kwamba amekuwa akiingilia watendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), kwa kujihusisha na utoaji wa ofa kwa wafanyabiashara wanaotaka kujenga hoteli za kitalii akitumia wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Bodi ya hifadhi hiyo.

Mbali na Msekwa Kambi ya Upinzani Bungeni, jana pia ilihoji vigezo alivyotumia Waziri wa Maliasili na Utalii,Ezekiel Maige kumteua Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa kuingia katika Kamati ya Kumshauri Waziri juu ya Sekta ya Vitalu vya Uwindaji.


Akiwasilisha maoni ya Kambi hiyo bungeni kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/12, Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii,
Mchungaji Peter Msigwa alimtaja Msekwa kwamba ni mmoja wa wanaokwamisha maendeleo katika hifadhi ya Ngorongoro.

"Tuna ushahidi kuwa,Pius Msekwa ambaye ndiye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, amegeuka kuwa mwenyekiti mtendaji anayefanya kazi ya kutoa ofa kwa wafanyabiashara wenye mahitaji ya kujenga hoteli za kitalii, huku akiwaelekeza maeneo hayo, kazi ambazo si zake,” alisema Mchungaji Msigwa.


Kutajwa kwa Msekwa na Benno, ni mwendelezo wa vigogo wa CCM kutajwa bungeni wakihusishwa na tuhuma mbalimbali baada ya juzi kambi hiyo ya upinzani kutaja orodha ya viongozi waandamizi wa zamani wa chama hicho na Serikali kwamba wamehodhi ardhi kubwa mkoani Morogoro.


Vigogo hao waliotajwa wakati wa Bajeti Kivuli ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2011/12 ni pamoja na Marais Wastaafu Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri Wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na John Malecela, Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho, Philip Mangula na aliyekuwa Naibu wake, Tanzania Bara, Hassan Ngwilizi.


Waziri mwenye dhamana ya Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka, akizungumzia madai ya viongozi hao kumiliki ardhi bila ya kuiendeleza alisema: “honeymoon is over" (fungate imekwisha).


Jana, Mchungaji Msigwa akifafanua tuhuma moja baada ya nyingine, aliliambia Bunge: “...Huu ni mgongano mkubwa sana wa kimaslahi na wenye madhara makubwa kwa hifadhi hii. Haiwezekani Mwenyekiti wa Bodi ya Ngorongoro, ambaye moja ya majukumu yake ni kukagua hali halisi ya hifadhi hiyo, ajiingize pia katika shughuli za utendaji tena zilizo nyeti kama hizo.”


Msemaji huyo wa upinzani mwenye dhamana ya maliasili na utalii, alisema Serikali inapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya Msekwa kwa kukiuka mipaka ya majukumu yake na kwamba kambi ya upinzani ipo tayari kuipa ushirikiano kuhusiana na tuhuma hizo.


Kuhusu Malisa kuingizwa katika kamati hiyo ya kumshauri waziri juu ya sekta ya vitalu vya uwindaji, Mchungaji Msigwa alisema: “Kijana huyu hana vigezo vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na ujuzi na uzoefu kwenye masuala ya utawala unaohusiana na uwezeshaji wa kiuchumi.’’


Msigwa alisema kambi ya upinzani imeshtushwa na uteuzi wa Malisa pamoja na kada mwingine wa CCM, Daniel Nsanzungwako na kusisitiza kwamba hawana vigezo vinavyotakiwa.


Alisema Malisa, anafahamika kitaaluma kuwa ana elimu ya sheria lakini hana uzoefu wowote katika masuala ya utalii na mazingira zaidi ya kujihusisha tu na shughuli za UVCCM.


“Ni dhahiri waziri amekiuka Sheria ya Wanyamapori na vigezo vyake katika uteuzi huo. Kambi rasmi ya Upinzani inalitaka Bunge hili tukufu kupitia kamati yake husika, ichunguze sababu za Mheshimiwa Waziri wa Maliasili kukiuka sheria katika uteuzi huo ili kujua alifanya hivyo kwa maslahi ya nani.”


"Kwa kuwa uteuzi huo haukuwa wa wazi, haukufuata misingi ya utawala bora na ulikiuka vigezo vya kisheria, Kambi rasmi ya Upinzani, inataka kamati hiyo iliyoundwa na waziri ivunjwe yote mara moja na kuundwa nyingine."


Ufisadi wizarani

Kuhusu ufisadi wizarani, alisema kumekuwapo ufujaji wa rasilimali za umma unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya watendaji wa umma, “kwa kisingizio cha udhaifu wa kimfumo.”

“Upembuzi wetu kuhusu ripoti na nyaraka za Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, umeonyesha mwaka wa fedha wa 2009/2010 pekee, wizara hii ilifanya ukiukwaji mkubwa wa Sheria na Kanuni za Fedha, wa jumla ya Sh9.2bilioni na kusababisha taifa lipate hasara ya moja kwa moja ya zaidi ya Sh1bilioni.”


Waziri kivuli huyo aliongeza: “Wizara hii kinyume kabisa na Sheria ya Misitu (CAP 323) na Kanuni za Misitu za mwaka 2007, ilipunguza tozo ya mrabaha wa mazao ya misitu tena bila kibali cha mamlaka husika ya misitu na kusababisha taifa lipate hasara ya Sh874.8 milioni.”


Alisema sehemu nyingine ni malipo ya posho ya samani kwa watumishi ambao hawakustahili wanaoishi kwenye nyumba zao binafsi, kinyume cha sheria na kwamba malipo hayo yalisababisha hasara ya Sh119.3 milioni, huku malipo ya mishahara ya watumishi hewa na wastaafu yakisababisha upotevu wa Sh10 milioni.


Msigwa alisema upo ulazima wa watumishi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii, waliohusika katika kukiuka sheria na kanuni za usimamizi wa fedha za umma na kulisababishia taifa hasara kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.


Ubadhirifu Tanapa

Kambi hiyo ya Upinzani ilisema ina taarifa za uhakika kuhusu matumizi makubwa ya fedha za umma yanayofanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) ikilinganishwa na fedha wanazokusanya.

“Kwa mwaka wa fedha 2008/2009, gharama za uendeshaji za Tanapa zilikuwa Sh66.0 bilioni wakati shirika lilikusanya kiasi cha Sh70.4 bilioni na katika kipindi hicho Tanapa ilitumia Sh3bilioni tu kwa ajili ya kusaidia jamii,” alisema Msigwa na kuongeza:


“Kwa hali hii, ni dhahiri kuwa mapato mengi ya Tanapa yanaishia kwenye kugharamia zaidi utawala wake kuliko kuingia serikalini na kusaidia jamii.”


Alisema lazima Serikali itekeleze jukumu lake la kuhakikisha inadhibiti matumizi makubwa yasiyo ya lazima ya fedha za umma yanayofanywa Tanapa.


Msigwa pia alizungumzia taarifa za amri ya Serikali kuitaka Tanapa kuhama katika jengo lake ili kupisha Mahakama ya Afrika.


“Ni vyema ikakumbukwa kuwa huko nyuma, Tanapa walijenga jengo lao la kitega uchumi (commercial wing) mkabala na makao makuu, ambalo Mahakama hiyo ya Afrika walipangishwa, lakini leo taarifa tulizonazo ni kwamba wamepewa jengo hilo kwa nguvu na Rais na Tanapa wametakiwa kutafuta sehemu nyingine ya kupanga kwa ajili ya ofisi,” alisema Msigwa.


Msigwa alisema taarifa hizo zinasikitisha kwani zinathibitisha utayari wa Serikai kuyapokonya mashirika ya hapa nchini mali zake kwa sababu tu ya kuzibeba taasisi za nje.


“Taarifa za Serikali kutaka kuipokonya Tanapa jengo lake, inadhihirisha kuwa Serikali yetu haijui inakokwenda, kwani jengo hilo halikujengwa kwa ajili ya Mahakama ya Afrika, bali, lilijengwa kwa ajili ya Tanapa kwa malengo ya Tanapa,” alisema.

No comments:

Post a Comment