KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday, 19 August 2011

Vigogo watatu wasimamishwa kazi kashfa ya wanyamapori

 
Thursday, 18 August 2011 22:09

MKURUGENZI ATIMUA MBIO BAADA YA UAMUZI KUTANGAZWA BUNGENI
Neville Meena, Dodoma na Fidelis Butahe, Dar
MOTO wa wabunge jana uliendelea kuiunguza Serikali kufuatia tuhuma mbalimbali za ufisadi kuibuliwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii, hali ambayo imemlazimisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutangaza kusitishwa kwa ukamataji na usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi, huku Waziri husika, Ezekiel Maige, akitangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi mpya wa Idara ya Wanyamapori, Obeid Mbangwa.

Mbangwa alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa usafirishaji wa wanyamapori hai wenye thamani ya Sh116 milioni na ndege 16 uliofanyika Novemba 24, mwaka jana kwenda nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Akihitimisha hoja ya bajeti ya Wizara yake bungeni jana, Waziri Maige alisema Mbangwa na maofisa wengine wawili wa wanyamapori wamepewa likizo ya malipo, hadi hapo uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili utakapokamilika.

Mara baada ya Maige kutoa kauli hiyo, Mbangwa ambaye alikuwa mmoja wa maofisa wa wizara waliokuwa kwenye ukumbi wa Bunge, alitoa nje na alionekana akikimbia kutoka nje ya eneo la bunge.

Moto wa wabunge
Wakichangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo jana, mapema wabunge hao walimtaja Mbangwa kuwa anahusika na utoroshaji wa wanyamapori 116 na ndege 16 uliofanyika Novemba 24, 2010 kupitia KIA.

Mbangwa alikuwa mkurugenzi mpya wa idara hiyo akichukua nafasi ya mtangulizi wake Erasmus Tarimo, alistaafu kwa mujibu wa sheria.  Wakati Tarimo akiwa Mkurugenzi, Mbangwa alikuwa Mkurugenzi Msaidizi (Matumizi Endelevu).

Wabunge wa CCM, Christopher Ole Sendeka (Simanjiro) na Beatrice Shellukindo (Kilindi) ndio walioongoza kuwasha moto dhidi ya Serikali huku wakibaini kuwa Idara ya Wanyamapori imejaa watendaji wa kabila la Wabena ambao wamewekwa ili kulinda maslahi binafsi ya kiongozi wa juu Serikalini.

Katika mchango wake, Ole Sendeka alisema Mbangwa hawezi kukwepa tuhuma za kuhusika na utoroshaji wa wanyamapori hao ambao walisafirishwa kwa ndege ya Jeshi la Qatar na kulaumu kuwa mtendaji huyo amepandishwa cheo badala ya kuchukuliwa hatua.

“Kinachotia fedheha kuliko yote ni kwamba, waliofanya kazi hiyo walipewa zawadi nyingine ya kupandishwa vyeo. Nataka niseme wazi kuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori wa sasa, ndugu Mbangwa, hawezi kukwepa lawama ya kutoroshwa wanyama hao,” alisema Ole Sendeka na kuongeza:

 “… ukizingatia kwamba kazi iliyokuwa inafanywa na kampuni zote 180 kukamata wanyama wetu pamoja na kwamba, sheria inakataza kampuni ya kigeni kukamata wanyama, katika utoroshaji wa wanyama zaidi ya 100, wageni walipewa leseni za kuwakamata na waliotoroshwa chini ya ulinzi wa baadhi ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama”.

Ole Sendeka aliwataja watendaji wengine ambao uwepo wao katika idara hiyo ni wa utata kuwa ni Nebbo Mwina ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo nyeti anayeshughulikia masuala ya Utafiti na Mafunzo, Luis Nzali ambaye ni Katibu wa Mfuko wa Kuendeleza Wanyamapori na ofisa mwingine aliyemtaja kwa jina la Nziku ambaye anasimamia masuala ya uwindaji katika idara hiyo.

“Lakini nataka kusema kuwa CITS wako wenyewe, hao sasa sitaki kuhoji mamlaka ya Rais ya kumteua Katibu Mkuu, mama Maimuna Tarishi, ambaye ni mchapa kazi, lakini bahati mbaya sana amekuta mtandao na kama hakuukuta…, bahati mbaya mtandao huu wa sehemu moja ya nchi hautoi matumaini,” alisema Ole Sendeka na kuongeza:

“Nataka kusema kwa utaratibu huu mnaweza mkaweka pale Sendeka, Lekule, Nangoro, Laizer , Mollel wakikaa pale wanaweza wakakaa wanaongea Kimasai na kusafirisha wanyama hao kwenda ugaibuni na hakuna mtu anayekamatwa”.

Shellukindo
Kwa upande wake Shellukindo alisema Idara ya Wanyamapori inaharibiwa na kigogo wa ngazi za juu ambaye amekuwa akitumia nafasi yake vibaya kulinda maslahi yake katika wizara hiyo.

“Kama mwezi uliopita hivi, nikapata ‘meseji’ ya mtu anatuma anasema Mama unafahamu Idara ya Wanyamapori imegeuka kuwa ya Wabena, nikasema eeh! Akaniambia Katibu Mkuu kaja na sifa zake vema, Mkurugenzi wa Wanyamapori naye Mbena, njoo kwenye Kitengo cha TWPF Mbena, hata kama kweli ndugu zangu wana sifa, lakini kiasi hicho?,” alihoji Shellukindo na kuongeza:

“Na hawa watu wote mara nyingi unakuta ni ‘ma-god father’ (miungu watu).  Jamani ifike mahali wasiokuwa watoto wa Shellukindo nao wafikiriwe wana uwezo. Idara tunaiua kwa sababu ya kuweka watu kwa maslahi yetu binafsi”.

Kuhusu Mbangwa, Shellukindo alisema Serikali inapaswa kuchukua hatua dhidi yake kwani anahusika na utoaji wa vibali 180 vya ukamataji na usafirishaji wa wanyama nje ya nchi.

“Mkurugenzi aangaliwe upya, hastahili kuwa pale mnampa taabu. Amehusika kama wenzangu walivyosema kwenye utoaji vibali 180 majuzi tu. Tunalalamikia utoaji holela wa vibali aliyetoa ni yeye leo Mkurugenzi, kuna ajenda gani?” alihoji mbunge huyo na kuongeza:

“…..mimi naomba kama kuna mtu huko juu unanisikia upo, kwa sababu Mungu ananionesha upo na wewe upo tunakujua na unajijua upo, imetosha! Huwezi kuweka Wilaya yako yote kwenye uongozi ndani ya nchi hii, huwezi kuweka kabila lako lote ndani ya nchi hii, kuna wengine wenye sifa.

Luhanjo
Juzi ndani ya kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo alitajwa kuwa ndiye anayetumia nafasi yake kushawishi uteuzi wa watendaji wa idara hiyo kwa lengo la kulinda maslahi yake.

Hata hivyo Luhanjo alipozungumza na Mwananchi alikanusha tuhuma hizo dhidi yake akisema zinapaswa kupuuzwa kwani yeye ni Katibu Mkuu Kiongozi wa nchi nzima na si wa wizara moja.

Serikali yanywea
Katika hali inayothibitisha kubanwa vilivyo na wabunge, mbali na kumsimamisha Mbangwa, Serikali ilitangaza kusitisha ukamataji na usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi kwa zaidi ya mwaka mmoja kuanzia sasa.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa msimamo huo jana wakati akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni jana na kusisitiza kuwa, katika muda huo, mfumo mzima wa usafirishaji wa wanyama utatazamwa upya kuona kama una tija au la.

Juzi, Kamati ya Bunge ya Maliasili na Utalii chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli, ilihoji ni lini twiga waliosafirishwa kwenda nje ya nchi  kupitia Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), watarejeshwa nchini na kutaka Idara ya Wanyamapori ifumuliwe.

Wakijadili hoja hiyo, wabunge wa CCM walimtaja Katibu Mkuu Kiongozi, Luhanjo kuwa ni chanzo cha ufisadi katika wizara ya hiyo. Juzi, watuhumiwa wa usafirishaji wa wanyamapori waliokamatwa Novemba 26, mwaka jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Pudenciana Kikwembe, Pinda alisema: “Kwanza tunataka tukubaliane na mawazo ya Wabunge kwa ujumla kwamba, inaonekana eneo hili bado utaratibu wake wa usimamizi na hata namna biashara yenyewe inavyofanyika, ni eneo ambalo kwa kweli linahitaji kutazamwa upya.

“Kwa hiyo, kama Serikali tumeamua kwamba, tutasimamisha usafirishaji au biashara za wanyama zote na tuangalie tena upya jambo hili na ikitokea kwamba tunakubaliana tuendelee nalo, ni dhahiri na lazima masharti yabadilike.

No comments:

Post a Comment