• Awatuhumu kujimilikisha kinyemela ardhi ya wanyonge na Salehe Mohamed, Dodoma |
VIGOGO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwamo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wastaafu, John Samwel Malecela na Frederick Sumaye wanatuhumiwa kujimilikisha ardhi yenye ukubwa wa hekta 5,700, ambazo wameshindwa kuziendeleza hadi sasa. Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, alisema hayo alipokuwa akitoa maoni ya kambi hiyo kwa bajeti ya wizara husika kwa mwaka 2011/2012. Alisema migogoro ya ardhi hapa nchini inasababishwa na vigogo wa chama tawala na serikali, kwa kunyang’anya wanyonge ardhi na kujimilikisha au kuwapa wawekezaji bila kufuata taratibu zinazotakiwa. Alibainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imekumbwa na mgogoro wa ardhi ambao unahusu shamba namba 299 (iliyokuwa NARCO ranches), lenye ukubwa wa hekta 49,981. Aliongeza kuwa taarifa zinaonyesha kwamba hekta 30,007 walipewa Mtibwa Sugar licha ya malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba eneo walilopewa wawekezaji hao ni kubwa sana. Alisema taarifa za kiuchunguzi zinaonyesha kwamba maeneo ambayo yalikuwa yamepangwa kugawiwa wanakijiji wa Wami yamegawiwa kwa vigogo wa CCM. Aliwataja vigogo hao ni Philip Mangula, (hekta 2,000), John Malecela (hekta 100) Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi (hekta 100), Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (hekta 2,000), Frederick Sumaye (hekta 500) na Rais Mkapa (hekta 1,000) ambazo ameziendeleza tofauti na wenzake. “Kambi ya Upinzani inahoji, hawa watajwa hapo juu ni wakazi wa Kijiji cha Wami- Dakawa? Na ni vigezo gani vilitumika kuwanyima ardhi wanakijiji na kuwapa wakubwa hawa? “Serikali haioni kwamba mgawo huu wa ardhi uliojaaa dhuluma na upendeleo unahatarisha maisha ya Watanzania na usalama wa nchi kwa ujumla?” alihoji. Mdee alisema wananchi wa maeneo haya wana hasira na serikali yao kwa kuwa wameshaambiwa hakuna tena eneo la kugawa, wakati walitozwa shilingi 20,000 kila mmoja kwa madai kwamba wangepewa hekta tano, ahadi ambayo mpaka sasa imeota mbawa. Mdee alisema katika Wilaya ya Mbarali, shamba la mpunga la Mbarali (Mbarali Rice Farm - ekari 14,437) na shamba la mpunga la Kapunga (ukubwa ekari 18,425) yalikuwa ndiyo chanzo cha mapato cha wananchi wa eneo husika. Alieleza kuwa mashamba hayo yalikuwa yanahudumia watu zaidi ya 30,000 na vijiji 10 lakini serikali iliamua kuuza eneo husika kwa Kampuni ya Highland Estates Ltd inayomilikiwa na Nawab Mulla, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya. Aliongeza kuwa shamba la Kapunga lilibinafsishwa na kukabidhiwa kwa Kampuni ya Export Co. Ltd kwa bei ya kutupa ya shilingi bilioni 2.3 na mmiliki wake sasa ni Jeetu Patel. Alibainisha kuwa hivi karibuni Kampuni ya Agri - Sol Energy LLC na Kampuni ya Serengeti Advisors Ltd, inayoongozwa na Iddi Simba na Betram Eyakuze, kwa pamoja wameunda Kampuni ya Agrisol Energy Tanzania. Alisema kampuni hiyo wameingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda mkataba unaotarajia kuipa kampuni husika miliki ya miaka 99 ya maeneo ya Lugufu, hekta 80,317 na Mishamo hekta 219,800. Aliongeza kuwa masharti ya msingi katika makubaliano baina ya halmashauri husika na wawekezaji ni kodi ya ardhi ambayo ni sh 200 kwa hekta, ushuru wa kisheria wa halmashauri, ada itakayolipwa halmashauri ni sh 500 kwa hekta. Sharti jingine ni iwapo mgogoro utatokea baina ya pande zote mbili, busara itatumika kutatua mgogoro, ikishindikana Chemba ya Biashara ya Kimataifa (ICC) ndiyo atakuwa msuluhishi. Mdee alisema katika hatua za awali, madiwani wa halmashauri husika walikataa kutoa maeneo yote mawili, waliagiza mwekezaji apewe eneo moja na kwa kipindi cha miaka 20. Kama ataonekana kufanya vizuri, wangefikiria kumwongezea muda na eneo. “Walioonekana kuwa wakali wakapelekwa Marekani kwa siku nne, baada ya kurejea, nchi ikaingizwa kwenye mkataba mwingine ambao utaigharimu miaka mingine 99 kuweza kujinasua. “Hii ndiyo Tanzania ambayo wazawa wananyang’anywa ardhi, maeneo yote muhimu na ya kimkakati na kukabidhiwa wageni, au watu wenye mamlaka na fedha, huku ikiwaacha wazawa kubaki vibarua au wakulima wadogo wanaotegemea hisani ya mabeberu,” alisema. Aliongeza kuwa wananchi wa Kijiji cha Mapinga, kitongoji cha Undindivu chenye idadi ya watu zaidi ya 1,400 wamekuwa wakimiliki eneo la Undindivu kwa ajili ya kilimo na ufugaji tangu mwaka 1960 lakini Kampuni ya Simba Motors (T) Ltd ilimilikishwa eneo lote la kitongoji cha Undindivu bila wananchi kushirikishwa. Alisema kampuni hiyo ilipima kwa kutumia mpimaji binafsi na ilimilikishwa shamba hilo lenye hekta 322 lakini hivi sasa ni miaka 17 kampuni husika haijawahi kuliendeleza eneo hilo, si kwa kilimo au ufugaji. |
No comments:
Post a Comment