na moshi lusonzo
Kampuni ya Simon Group ambayo ina hisa kwenye Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) imekiri kuingiza sh. milioni 400 katika akaunti binafsi ya waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara, Idd Simba kama malipo ya mchakato wa kumiliki shirika hilo.
Akizungumza kwenye mdahalo wa "Sakata la ununuzi wa UDA" uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Robert Kisena alisema pesa hizo ziliingizwa kwenye akaunti hiyo binafsi ya mzee Simba kutokana na sababu mbili ikiwemo kama dhamana ya ununuzi na heshima ya mzee Simba.
Kisena alisema malipo hayo yalifanyika kabla ya malipo ya ununuzi wa hisa asilimia 51, Februari 22, mwaka huu.
Akifafanua juu ya pesa zilizowekwa kwenye akaunti ya mzee Simba, alieleza wakati wanajadiliana juu ya ununuzi wa hisa hizo Bodi ya UDA iliitaka Simon Group kutoa pesa kama dhamana ili kuepuka usumbufu.
Alisema hakuweza kuingiza pesa hizo mpaka walipopatiwa barua ya maelekezo ya kisheria ndipo walipoingiza pesa hizo kwenye akaunti ya Simba.
Kisena alisisitiza kwamba pesa hizo lazima zitalipwa na jitihada zinafanyika ili zirudishwe haraka na kuingizwa katika akaunti ya UDA.
Alisema mpaka sasa Simon Group imefanya malipo ya hisa walizonunua kwa awamu mbili ikiwa awamu ya kwanza ililipwa tarehe 22 Februari na Februari 25, mwaka huu.
Alisema Shirika la UDA lilipoanzishwa lilikuwa linamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali. Alisema Jiji lilikuwa na hisa ya asilimia 51 na serikali asilimia 49 kupitia Msajili wa Hazina.
Alisema katika mchakato wa kununua UDA ilionekana Halmashauri ya Jiji ilikuwa mmliliki mkubwa na baada ya mgawanyo uliofanyika, Halmashauri ya jiji ilibaki kuwa na asilimia 24, Serikali asimilia 23 na Simon Group ikanunu asilimia 52 ambazo zilikuwa hazijakuwa kwenye gawio.
Alisema thamani ya hisa hizo ni sawa na Sh. Milioni 7.8 na thamani wanazomiliki Serikali na Halmashauri ya jiji ni Sh. Milioni 7.1 pekee.
Alisema kilichopelekea kwa Shirika hilo kuuza sehemu ya hisa inatokana na Shirika hilo kujiendesha kwa hasara kutokana wanahisa wake wawili kushindwa kuongeza mtaji tangu mwaka 1983.
Alisema kimsingi kampuni yake kuingia ubia kwenye shirika hilo itawezesha kuweka mtaji mkubwa na kuhakikisha kuanzia mwaka huu magari 200 yatanunuliwa ambapo kati ya hayo mabasi makubwa yanayobeba watu 150 kwa wakati mmoja, yatakuwa 150.
Hata hivyo alipinga vikali kuwa Simon Group inamilikiwa na baadhi ya vigogo na kueleza huko nyuma mmoja wa wanahisa alikuwa Profesa Juma Kapuya aliyemiliki asilimia tano za hisa lakini kwa sasa amejitoa na Kampuni hiyo inamilikiwa na familia mbili ambazo hazina uhusiano na vigogo
No comments:
Post a Comment