Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeamua kuunda Kamati maalum itakayochunguza sakata la Katibu Mkuu Kiongozi Philomeni Luhanjo kutangaza matokeo ya uchunguzi tuhuma za Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na madini David Jairo na kumrejesha kazini kabla ya matokeo ya uchunguzi wa tuhuma kujadiliwa Bungeni.
Akitangaza hatua hiyo Naibu Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai amesema "Spika wa bunge mama Anne Makinda ataunda Kamati kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge la Bajeti, ili ripoti hiyo ya kamati ijadiliwe na waheshimiwa wabunge katika kikao kijacho cha bunge".
Hatua hiyo imetokana na hoja iliyotolewa na Zitto Kabwe mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini CHADEMA kuwa kutona na hatua ya kumrejesha Jairo Kazini na mkwamba hana hatia ni kulidhalilisha bunge na Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za bunge Bungeni.
Alisema kitendo alichofanya Katibu Mkuu Kiongozi ni kulidhalilisha Bunge na Waziri Mkuu na kuagiza kuwa kitendo kisirudiwe tena.
Hapo jana Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu Bw. Filemon Luhanjo alitangaza kuwa baada ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kutenga mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kuhonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo, kubainika kuwa si za kweli.
Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo alitangaza uamuzi huo katika mkutano wake na waandishi uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana akisema Jairo hana hatia na leo anapaswa kurejea kazini mara moja.
Alisema matokeo ya uchunguzi dhidi yake yamebainisha kwamba hakuwa na hatia hivyo kusema kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Sheria namba 8 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003, anamrejesha kazini Jairo... “Ninaamuru David Jairo arejee kazini kuanzia siku ya Jumatano (leo).”
Julai 18, Jairo alituhumiwa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwamba amezitaka taasisi, vitengo na idara zilizo chini ya wizara hiyo, zichangie Sh50 milioni kila moja, ili kufanikisha bajeti hiyo.
Tuhuma hizo zilitolewa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo na kumfanya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuzitolea maelezo Bungeni akisema akama angekuwa na mamlaka, angelitolea uamuzi lakini akaahidi kulifikisha kwa Rais ambaye alisema ndiye mwenye mamlaka ya uteuzi.
Tuhuma nyingine zilizokuwa zimetolewa na Shellukindo ni za kulipa masurufu ya safari za watumishi walio chini ya wizara hiyo na taasisi zake, ambao tayari walikwishalipwa na wizara na taasisi hizo.
Kutokana na tuhuma hizo Luhanjo alimpa likizo ya malipo katibu huyo na Julai 21 alimwandikia barua Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh na kumpa siku 10 kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ambao alisema haukuweza kuthibitisha tuhuma hizo. Luhanjo ambaye katika mkutano huo wa waandishi alikuwa na Utouh alisema: “Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi wa awali, mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu Nishati na Madini (Jairo), sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma. Pia sitampa Hati ya Mashtaka kwa sababu Jairo hajapatikana na kosa la kinidhamu kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi maalumu.”
No comments:
Post a Comment