Padri Karugendo
---
Na Nova Kambota,
Akiandika kupitia gazeti maarufu la uchambuzi nchini Raia Mwema mwandishi nguli na mwanaharakati wa siku nyingi Padri Privatus Karugendo kwenye toleo namba 196 la tarehe 27 julai 2011 Karugendo anahoji “Kwa nini tupoteze fedha nyingi kujadili “ndiyo” bungeni?”.
Niliposoma makala ile nilimwelewa vilivyo padri Karugendo labda niseme kuwa ingawaje makala yake ilichota nukuu kutoka kwenye Biblia takatifu ““UKISEMA, ‘ndiyo’, basi, iwe ‘ndiyo’, ukisema ‘siyo’, basi iwe kweli ‘siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu” (Mathayo 5:37)” lakini acha niseme ukweli kuwa Karugendo alifanikiwa kuweka mambo hadharani bila kificho, aliweza kuonyesha jinsi taifa linavyopoteza fedha nyingi kwa vikao vya Bunge ambavyo vimetamalaki kwa unafiki wa wabunge hususani wa CCM kwa kuendesha sarakasi za chama chao ndani ya bunge.
Padri Karugendo alitoa pendekezo la kupunguza muda wa kukaa Dodoma kwa wabunge wetu na akashauri wabunge wa upinzani waanze kusambaza taarifa za kimaandishi juu ya michango yao kwenye maswala ya kitaifa kuliko kuendeleza mijadala ambayo mwisho wake huzaa NDIYO kutokana na tabia ya wabunge wa CCM kutetea chama chao na kusahau taifa, Karugendo anajenga hoja yake kwa mtindo wa swali anapohoji “yanini kwenda kujadili mambo yaliyokwishaariwa”
Naam! hakika Padri Karugendo ameibua mjadala mkubwa iwapo kweli tunahitaji bunge hili la sasa? ambalo limemezwa na hoja za ndiyo hata panapostahili siyo?. Ni ukweli usiopingika kuwa kilio cha Karugendo ni cha watanzania wengi ambao wanaamini kuwa vikao vya bunge vinavyoendeshwa kwa mazoea ya kujibu ndiyo havina maana kwa sababu hata Mungu hapendi unafiki huu!
Labda nirudi nyuma kidogo kwa kuhoji, je wabunge wa CCM wanapotetea chama chao bungeni wana maana gani? je wanamaizi kwa kiasi gani wanatukera? watafanya hivyo mpaka lini? huku watanzania tukiendelea kusota kwenye lindi la umasikini? hakika wanajidanganya, kwa mbali naona wabunge wa CCM wanajipiga mtama wenyewe wao na chama chao, ni swala la muda tu kama si leo basi kesho wataanguka tu, kwani mtu akijipiga mtama anategemea nini? kama si kuanguka? Tafakari!
Nova Kambota Mwanaharakati,
+255717 709618
novakambota@gmail.com
www.novakambota.com
Tanzania, East Africa
Agosti 10, 2011.
+255717 709618
novakambota@gmail.com
www.novakambota.com
Tanzania, East Africa
Agosti 10, 2011.
No comments:
Post a Comment