KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Monday, 12 September 2011

WAZAMIAJI TOKA AFRIKA KUSINI WATUA ZENJI KUTAFUTA WALIOZAMA BAHARINI

Meli ya MV Spice Islander ikiwa imepinduka na kuzama katika pwani ya kisiwa cha Nungwi Zanzibar usiku wa kuamkia juzi.
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Wazamiaji 12 kutoka nchini Afrika ya Kusini, wamewasili usiku huu mjini Zanzibar kuungana na wazamiaji wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini ili kufanya uhakiki wa kujua kama bado kuna mili iliyokwama kwenye Meli ya MV Spice Islander iliyozama chini ya bahari eneo la Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja usiku wa Jumamosi wiki iliyopita.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mh. Aboud Mohammed, amesema kuwa wazamiaji hao wamewasili wakiwa na zana za kisasa za uzamiaji na kwamba kazi ya kwanza itakayofanywa na timu hiyo ni kuhakikisha kuwa wanaifikia meli hiyo iliyozama umbali wa karibu nusu kimometa kwenye mkondo mkubwa wa maji na majabali.
Bado Serikali na wananchi mbalimbali wanadhani kuna miili ya watu waliokwama katika vyumba vya meli hiyo tangu ilipozama usiku wa Jumamosi Septemba 10 mwaka huu ikiwa na idadi ya watu isiyojulikana.
Makundi ya wananchi wamekuwa wakitaja idadi ya ndugu na jamaa waliosafiri na Meli hiyo na ambao hawajapatikana wakiwa hai ama miili yao kiasi cha kutia shaka kuwa huenda bado wamenasa ndani ya vyumba vya meli hiyo iliyozama chini ya kina kirefu cha mkondo wa bahari ya Hindi.
Tangu kuokolewa kwa abiria 619 na kuopolewa kwa miili ya watu 197 hadi jana jioni, hakujapatikana mtu hai ama mwili wa abiria aliyekufa maji ukielea juu ya maji ama kukokotwa kupelekwa mwambao mwa nchi kavu.
Katika eneo ilipo Meli hiyo zipo Meli nyingine za MV Kasa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na MV Mamba ya Jeshi la Polisi ambazo zote ziliwasili alfajiri siku ambayo tukio hilo la kuzama kwa MV Spice Islander.

No comments:

Post a Comment