Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewekwa kitanzini baada ya Umoja wa Wanazuoni wa Kiislam Tanzania (HAY-AT) kutoa muda wasiku tatu kwa viongozi wake wa taifa kulaani na kumuomba radhi Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Fatma Kimario kwa kumvua sitara yake na kumdhalilisha.
Pia umoja huo umeonya kuwa iwapo CHADEMA hawatafanya hivyo wataandaa maandamano nchi nzima kutangaza chama hicho kuwa adui mkubwa wa dini hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Umoja huo, Bw. Sherally Sherally alisema kitendo kilichofanywa na baadhi ya wafuasi wa CHADEMA ni udhalilishaji kwa mwanamke wa kiislamu hivyo ni lazima viongozi wake wa juu walaani waliohusika na kuomba radhi.
Tayari watu watatu wakiwamo wabunge wawili wamefikishwa mahakamani mkoani Tabora wakituhumiwa kwa kumshambulia Bi. Kimario na kumwibia simu yake yenye thamani ya sh 400,000. Watuhumiwa hao waliachiwa juzi kwa dhamana hadi Agosti 10, mwaka huu.
Bw. Sherally alisema iwapo chama hicho kitapuuza agizo hilo kwa muda waliowapa umoja huo utapita nchi nzima kutafakari hatua stahiki za kukabiliana na dharau hizo dhidi ya mwanamke.
"Tunalaani na kupinga kwa ukali kabisa kitendo kilichofanywa na wanaodaiwa kuwa ni wafuasi na viongozi wa CHADEMA kumvua hijabu Bi. Kimario na kumuacha bila stara huko Igunga Septemba 15," alisema Bw. Sherally na kuongeza:
"Kitendo hiki kumvua hijabu Bi. Kimario, kumsukasuka na kumtolea maneno yasiyofaa ni kitendo kiovu sana mbele ya Mwenyezi Mungu, Waislam na Watanzania wote wapenda haki na amani na wanaojiheshimu," alisema.
Katika hatua nyingine Bw. Sherally alisema wamesikitishwa na kushitushwa na kukaa kimya kwa asasi za kijamii zinazodai kutetea haki za binadamu na wanawake kwa kutolaani kitendo hicho cha mwanamke mwenzao kudhalilishwa kijinsia.
"Kuendelea kukaa kwao kimya kutatulazimisha kuwaona kuwa wanaafiki na ndumilakuwili," alisema.Chanzo Gazeti Majira.
No comments:
Post a Comment