KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Sunday, 11 September 2011

NI MSIBA MKUBWA ZANZIBAR NA TANZANIA KWA UJUMLA

Sunday, 11 September 2011 07:13 
*MELI YAZAMA, WATU ZAIDI YA 190 WAFA
WATU 160 wamefariki dunia na wengine 521 kujeruhiwa baada ya meli ya abiria LCT Spice Islanders, iliyokuwa ikisafiri kutoka Unguja kwenda Pemba, kupinduka na kuzama baharini.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa meli hiyo iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya 600, ilizama usiku wa kuamkia jana kwenye Bahari ya Hindi kati ya Nungwi na Pemba, kilomita 20 kutoka Bandari ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa habari hizo, meli hiyo iliyotokea Unguja kwenye Bandari ya Malindi, ilipata hitilafu ikiwa njiani, kisha ikapinduka na kuanza kuzama taratibu. Ilikuwa na makoti ya uokoaji 200 tu.

Mwandishi Mkongwe nchini, Salim Salim, aliambia gazeti hili kwamba juhudi za kuoka zilianza kufanyika mapema kwa ushirikiana wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), KMKM, Jeshi la Polisi na wananchi kutoka eneo la Nungwi.

Salim alisema saa tata baada ya ajali hiyo kutokea jeshi la polisi lilifika katika eneo la polisi pamoja na wananchi walitoka sehemu mbalimbali. Polisi walitumia helikopta mbili na wananchi asilimia kubwa akiwa wavuvi walitumia mashua.

Pia boti za uokoaji za Azam na Express Zakhir zilifika katika eneo la tukio mapema na kuifanya kazi kubwa ya uokoaji.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP, Said Mwema alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana na kwamba chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana.

Alisema mpaka kufikia jana mchana watu waliokolewa katika ajali hiyo wakiwa hai walikuwa 525 na waliofariki 62.

Mwema alisema imeunda kamati maalum ya kufuatilia tukio hilo ambayo pia itahusisha Usalama wa Taifa.

“Hivi sasa Jeshi la Polisi, JWTZ, Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na KMKM ndio wanashughulikia suala zima la upelelezi ili kujua chanzo cha ajali hiyo,” alisema Mwema

Aliongeza: “ Eneo la Usimamizi wa mawasiliano na uratibu itakuwa chini ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, pia kuna kikosi kazi cha uokoaji na kikosi cha kukusanya taarifa na upelelezi wa tukio hilo,”.

Alipoulizwa idadi kamili ya watu waliofariki katika ajali hiyo pamoja na uwezo wa meli hiyo kubeba abiria na mizigo Mwema alisema: “Hivi sasa ndio tunaendelea na uchunguzi ili kubaini idadi kamili ya waliofariki, ila kwa sasa kinachofanyika ni uokoaji”.

Rais Shein

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, alifika kwenye eneo la tukio na kushiriki kikamilifu kutoa huduma ya kwanza kwa walinusurika katika ajali hiyo.

Akizungumza katika kijiji cha Nungwe, Dk Shein aliwataka Wazanzibari kuwa wavumilivu katika kipindi hiki wakitiana moyo kwa yote yaliyotokea.

"Huu ni mtihani wa Mwenyezi Mungu. Wazanzibari tuwe wavumilivu, Serikali itakayogharimia shughuli zote za mazishi," alisema Dk Shein.

Dk Shein alisema maiti waliotambuliwa watachukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi ila wale ambao ndugu hawataonekana watazikwa na Serikali kwa utaratibu maalumu.



Shuhuda
Mwandishi Mkongwe wa habari Zanzibar, Salim Salim, amelieleza gazeti hili kuwa meli hiyo ilizama katikati ya Kisiwa cha Pemba na Unguja eneo ambalo ndilo lenye mkondo mkuu bahari kuliko mikondo yote ya bahari barani Afrika.

Mikondo mingine mikuu ya bahari inayoufuatia mkondo wa Bahari wa Nungwi ni Pemba Channel ulioko nchini Msumbiji na Affond ulioko Somalia

Alisema ajali hiyo ilisababisha maduka yote kisiwani Pemba kufungwa kutokana na wakazi wengi wa pemba kwenda  kutambua miili ya marehemu, iliyofanyika katika Viwanja vya Maisara vilivyoko kiwani humo.

"Wananchi walianza kutambua miili ya marehemu saa 8:30 mchana wakiwamo viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walioongozwa na Rais Shein na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad.

"Maduka yote yamefungwa na misikitini kunafanyika sala maalumu. Pia vituo vyote vya radio na televisheni visiwani hapa, vimeacha kupiga muziki na pia kutakuwa na maombolezo maalumu ya ajali," alisema Salim.

Salim alisema katika viwanja hivyo vya Maisara walikusanyika madaktari kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar ambao kwa pamoja wanatoa huduma ya kwanza katika mahema maalum kwa majeruhi.

"Sanda zinashonwa hapohapo uwanjani na Serikali imesema itagharimia shughuli zote za mazishi," alisema Salim.

Salim alisema maiti zote zilizokuwa zikitolewa, zilikuwa zimepewa namba na mpaka anaondoka uwanjani hapo jana mchana, maiti 160 zilikuwa zimeopolewa.

"Kazi ya uokoaji inaendelea ila mpaka mimi naondoka eneo la tukio, kulikuwa na maiti 160. Niseme tu kwamba, Serikali safari hii imeonyesha kuwajali wananchi wake, kwa kuharakisha kuanza uokoaji," alisema.


Dk Shein ashiriki kutoa
huduma ya kwanza

Katika hatua nyingine, jana Rais Shein alikuwa miongoni mwa madaktari waliokuwa wakitoa huduma ya kwanza kwa majeruhi wa ajali hiyo ya meli.

Dk Shein ambaye siku nzima alikuwa katika eneo la tukio, akishirikiana na madaktari kuwapokea wagonjwa katika mahema maalumu na kuwapa huduma ya kwanza.

Watu wengi walionusurika katika hali hiyo walionekana kupata mshituko mkubwa, ingawa hawakuwa na majeraha makubwa.
Kazi hiyo ya uokoaji ilikuwa ikiongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na  KMKM.
Wakati Dk Shein akiwa anashiriki kutoa huduma ya kwanza kwa majeruhi, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alionekana muda wote akiwa sambamba na vikosi vya uokoaji akisimamia kwa karibu zoezi hilo.

"Maalim Seif alionekana akisimamia upatikanaji wa vifaa na vitu vingine muhimu vya uokoaji," kilisema chanzo cha habari kutoka Pemba

Kichanga aokoka kifo

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi minne hadi mitano, aliokolewa katika ajali hiyo.

Televisheni ya Channel Ten, ilieleza kuwa mtoto huyo alikutwa akielea juu ya maji licha ya kutovalishwa kifaa chochote maalumu vya kuogolea. Kwa mujibu wa Kituo hicho cha Televisheni, mtoto huyo anaendelea vizuri.

Sumatra wazungumza

Akizungumza na Mwananchi Jumapili Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), David Mziray.
Alisema taarifa walizonazo zinaeleza kuwa meli hiyo iliondoka Unguja kwenda Pemba saa 4:20 usiku jana.

“Mpaka sasa meli ya Mv Jitihada imeelekea eneo la tukio kwa ajili ya kuokoa watu, meli ilikuwa na abiria 500 na wafanyakazi 12,” alisema Mziray.

Aliongeza: “Meli hii imesajiliwa Zanzibar na taarifa za kuzama kwake zilifika saa 9:10 usiku wa kuamkia leo(jana),”.

Kikosi cha wanamaji Dar
Awali gazeti hili lilifika katika ofisi za kikosi cha wanamaji jijini Dar es Salaam na kuelezwa kuwa meli hiyo iliondoka jana (juzi) jioni ikiwa na abiria 229.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu akiwa njiani kuelekea ilipozamia meli hiyo Kamanda wa Kikosi hicho, Mboje Kanga, alisema meli hiyo ilizama ikiwa na zaidi ya watu 500.

“Mpaka sasa sijui kinachoendelea ndio niko njiani naelekea eneo la tukio, nipigie baadaye nitakuwa nimetapa kila kitu,” alisema Kanga.

Wafanyakazi Bandarini
Baadhi ya wafanyakazi wa bandarini pamoja na wabeba mizigo walilieleza gazeti hili kuwa huenda meli hiyo ilizama kutokana kubeba mizigo mingi.
Wafanyakazi hao ambao walikuwepo katika bandari hiyo wakati ikiondoka katika bandari ya Zanzibar wanasema kuwa jinsi ambavyo ilipakia abiria na mizigo huenda itakuwa ndiyo sababu ya kuzama kwake.
Mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema wakati meli hiyo ikiondoka Unguja alikuwepo na kwamba ilikuwa imeelemewa upande mmoja.
“Meli iliruhusiwa kuondoka bandarini Unguja kwa nguvu kwa kuwa watu waliokuwa wakitaka kupanda licha ya kuwa kuambiwa imejaa na walikuwa wengi. Meli ilipakiwa idadi kubwa ya nondo, madirisha, magunia ya unga wa ngano na mahindi,” alisema.
Mfanyakazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Shadrack alisema meli nyingi zinazotoka Unguja kwenda Pemba huwa zinajaza mizigo na watu wengi na kusisitiza kuwa, eneo la Nungwi ni baya hasa kama meli ina mzigo mkubwa kwa kuwa eneo hilo lina mkondo mkubwa wa maji.
“Nakwambia wazi meli hii ilikuwa na watu zaidi ya 600 maana wanasema waliookolewa tu ni 500…,” alisema Shadrack.

Hekaheka Bandarini Dar
Mwananchi Jumapili lilifika asubuhi bandarini jijini Dar es Salaam na kuta idadi kubwa ya watu wakitafuta usafiri wa meli kuelekea Zanzibar kwenda kutambua ndugu zao waliokuwa katika meli hiyo.
Ally Hamisi alilieleza gazeti hili kwamba, katika meli hiyo kulikuwa na ndugu zake saba ambao hajui kama wako hai ama wamekufa.
“Walikuwa wametoka katika harusi…, kwa kweli nimechanganyikiwa kabisa, pia alikuwemo jirani yangu ambaye nilikabidhiwa ili nimpeleke Zanzibar na mpaka sasa hajaonekana,” alisema Hamis.
Alisema meli hiyo ilipofika Unguja walipanda ndugu zake wengine watatu.
 “Ni jambo la kusikitisha sana, usiku nilipigiwa simu na mmoja wa ndugu zangu akanieleza kuwa tumuombee kwa kuwa meli ilikuwa ikizama, baadaye simu yake haikupatikana tena na sijui kama yupo salama au la,”.
Naye Khamisi Abdallah alisema kwa masikitiko kuwa katika meli hiyo alikuwa na ndugu 10.
“Nimekata tiketi ili niende kushuhudia mwenyewe…, mpaka sasa siamini na sijui nani kapona nani kafariki, inaniuma sana,” alisema Abdallah kwa masikitiko.
Mwantumu Suleiman ambaye ni mkazi wa Zanzibar, alisema alikuja jijini Dar es Salaam na mume wake na mdogo ambao waliondoka na meli hiyo.
“Wao walikwenda ila mimi nilibaki hapa Dar es Salaam nilikuwa naumwa tumbo, niliposikia habari hizi nimechanganyikiwa kweli,  bado sijapona, lakini acha niende nikashuhudiwa kilichotokea,” alisema Mwantumu kwa masikitiko.

Hii ni mara ya pili meli kuzama katika bahari ya Malindi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mei 29, 2009, meli ya mizigo inayomilikiwa na Kampuni ya Seagul, MV Fatih, ilipinduka na kuzama katika Bandari ya Malindi, Zanzibar na kuua watu watatu na kujeruhi wengine 27.

Meli hiyo ilipinduka na kuzama ghafla ikiwa tayari imeshafunga gati katika Bandari ya Malindi majira ya saa 4.00 usiku na abiria waliokuwemo walikuwa wanataka kushuka.

Akisimulia mkasa wa ajali hiyo kepteni aliyekuwa akiendesha meli hiyo, Ussi Ali Ussi, alisema wakati akiingia bandarini ghafla aliona meli hiyo ikijaa maji na kulala upande wa kushoto.

Habari hii imeandaliwa na Talib Hamad,  Fidelis Butahe, Claud Mshana, Elias Msuya na Geofrey Nyang’oro, Igunga

No comments:

Post a Comment