|
James Magai MKUU wa Upelelezi wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam,Abdallah Zombe ameibuka tena na kutoa kali kwa kudai kuwa siku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiingia madarakani yeye atajinyonga. Zombe ambaye alishinda kesi ya mauaji, iliyokuwa ikimkabili yeye na askari wengine 12, alitoa kali hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Dar es Salaam kufuatia hotuba ya chama hicho bungeni kuhoji kuachiwa kwake. Katika kesi hiyo iliyovuma tangu walipokamatwa mwaka 2006, walikuwa wakituhumiwa kuwaua kwa makusudi wafanyabiashara wanne wa madini Kutoka Mahenge na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam, katika msitu wa Pande wilayani Kinondoni nje ya Jiji la Dar es Salaam. Walikuwa wakituhumiwa kuwaua Sabinus Chigumbi maarufu kama Jongo, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi Juma Ndugu wa Manzese Dar es Salaam. Hata hivyo Agosti 17, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwaachia huru baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani Salum Masatti aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo kuridhika kuwa hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili. Lakini Julai 28, mwaka huu, Waziri kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alihoji sababu za kuachiwa kwa Zombe na wenzake. Katika hotuba yake bungeni mwishoni mwa wiki, Lema alihoji kuachiwa kwa Zombe na wenzake wakati akisoma hotuba ya kambi ya Upinzani, baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha kuwasilisha bajeti ya wizara yake hiyo.Hatua hiyo ya Chadema kuhoji kuachiwa kwake ilimkera Zombe ambapo jana alizungumza na waandishi wa habari na kuelezea kushangazwa na hatua hiyo ya Chadema kuhoji bungeni mamlaka ya mahakama. Zombe alisema kuwa ni dhahiri kuwa wabunge wa chama hicho hawajui majukumu yao kama wabunge wala sheria na Katiba ya nchi licha ya kuapa kuilinda Katiba hiyo na kwamba ndio maana wanafanya mambo ya kitoto bungeni. Aliongeza kuwa kutokana hali hiyo hawafai kupewa nchi kuiongoza na akatamka kuwa siku wakiongoza nchi yeye atajinyonga. “Julai 28 mwaka huu nilishangaa sana sana na kauli ya mbunge aliyeonyesha kutokujua taratibu za sheria za nchi hii; Baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha kumaliza kuwasilisha bajeti ya wizara yake, Godbless Lema mbunge wa Chadema akiwa waziri kivuli wa wizara hiyo, wadhifa ambao nadhani hastahili kuwa nao aliuliza swali kuwa ni kwa nini Zombe aliachiwa”, alisema. Alisema “Ile hotuba sijui ilitengenezwa na nani lakini huyu ni mtu hatari sana maana haijui kabisa Katiba,” alisisitiza Zombe, huku akinukuu Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayosema kuwa chombo chenye mamlaka ya mwisho katika kutoa haki ni mahakama. “Mbunge anahoji uamuzi ya mahakama bungeni, kwanza uamuzi ule haujui, hajawahi kuusoma kujua Zombe amedhulumiwa haki zake kiasi gani; “Anapaswa kujua mgawanyo wa madaraka wa mihimili ya dola ambayo ni Serikali Bunge na Mahakama.Mbunge hawezi kuingilia maamuzi ya mahakama. Mahakama iliamua Zombe aachiwe wewe unahoji ameachiwaje?” alisema huku akionyesha kukerwa. Hata hivyo, Zombe alisema kuwa kama angehoji kuhusu askari wengine walioua raia ni kwanini hawajafikishwa mahakamani ingekuwa ni sahihi lakini si kuhoji uamuzi wa mahakama.Akizungumza kuhusu kesi aliyoifungulia Serikali akiidai Sh5.2bilioni alisema inatarajiwa kuanza kusikilizwa Septemba 8, 2011, mbele ya Jaji Upendo Msuya. Lema ajibu Naye Lema alipoulizwa jana mjini Dodoma alisema hotuba ile yeye aliitoa bungeni na hivyo hawezi kujibizana na Zombe bali anaweza kujibizana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.Lema alisisitiza kuwa Zombe alikuwa ni mtuhumiwa wa mauaji ya raia na kwamba mahakama kumwachia huru haina maana kwamba hakuwa na kosa.“Huyu si saizi yangu, yeye ni mtuhumiwa tu na mimi sina tuhuma yoyote katika kituo chohote cha polisi kuhusu tuhuma hizo. |
No comments:
Post a Comment