KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Tuesday, 2 August 2011

Magufuli: Barabara za juu zimeanza kujengwa Dar

Serikali imeanza ujenzi wa barabara za juu (flyover), lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Mpango huo wa kupunguza msongamano huo ambao umekuwa ukisababisha kero kubwa kwa wakazi wa Jiji ulitangazwa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, wakati akisoma hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Waziri Magufuli aliliambia Bunge kuwa usanifu wa barabara ya juu ya Tazara, ulianza Juni mwaka huu kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Japan (Jica). Kadhalika, Dk. Magufuli alisema kuwa serikali imepeleka maombi kwa serikali ya Japan kupitia JICA ili kusaidia ujenzi wa barabara hizo.
BABABARA ZA KUUNGANISHA JIJI
Kwa upande wa barabara za chini, Dk. Magufuli alisema katika mwaka wa fedha huo, serikali itajenga na kukarabati mitandao ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni jitihada za kupunguza msongamano wa magari. Alizitaja barabara zitakazohusika katika mpango huo kuwa ni Ubungo Bus Terminal-Mabibo hadi Kigogo Roundabout yenye urefu wa kilomita 6.4.
Kwa kujibu wa Dk. Magufuli, kazi ya ujenzi wa barabara hiyo inaendelea na utekelezaji wake umefikia asilimia 75.
Dk. Magufuli alisema pia barabara ya Kigogo Roundabout hadi bonde la Msimbazi-Twiga /Msimbazi Junction yenye urefu wa kilomita 2.7 inaendelea kujengwa na utekelezaji wake umefikia asilimia 42.
Waziri Magufuli alisema kuwa barabara nyingine katika mpango huo ni ya Tabata Dampo-Kigogo-Ubungo Maziwa External yenye urefu wa kilomita 2.5 na kuongeza kuwa kazi ya usanifu wa barabara hiyo imekamilika na hatua inayofuata ni kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wake.
Aidha, alisema barabara ya Old Bagamoyo hadi Garden Road yenye urefu wa kilomita 9.1 ipo katika mchakato wa kumpata mhandisi mshauri kwa ajili ya usanifu unaoendelea wakati barabara ya Jet Corner-Vituka-Davis Corner yenye urefu wa kilomita 10.3 kazi ya ujenzi inaendelea.
Dk. Magufuli alisema pia kazi ya usanifu katika barabara za Mbezi (Morogoro Road)- Maramba Mawili-Kinyerezi-Banana yenye urefu wa kilomita 14, Tegeta-Kibaoni-Wazo-Goba-Mbezi Mwisho yenye urefu wa kilomita 20 na Tangi Bovu–Goba yenye urefu wa kilomita 9, imekamilika na kufafanua kuwa hatua inayofuata ni kutafuta fedha kwa ajili ujenzi wa barabara hizo.
Pia alisema kazi ya usanifu inaendelea na itakamilika katika mwaka 2011/2012 kwa barabara za Kimara Baruti-Msewe-Changanyikeni (Km 2.6 ) na Kimara –Kilungule-External Mandela Road (Km 9).
Hali kadhalika, alisema serikali ipo katika mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kimara-Magomeni (kilomita 10.4) na Magomeni–Kivukoni, Kawawa (kilomita 10.5), zitakazotumika na Mradi wa Mabasi yaendao Kasi (DART).
KAMATI: MSONGAMANO ATHARI KWA UCHUMI
Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilisema kuwa tatizo la msongamano lina athari nyingi kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.
Akisoma taarifa ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Anne Kilango Malecela, alisema wafanyakazi wanachoka kabla ya kuanza kazi kwa kuwa wanatumia muda mwingi barabarani na kuwa hali hiyo imekuwa ikipunguza tija.
Kilango alisema kuwa wastani wa mwendo katika barabara kuu za jiji hilo umefikia kilomita tano hadi 10 kwa saa.
Alisema utafiti uliofanywa na mradi wa DART ulibaini kuwa Tanzania inapoteza Sh. bilioni nne kila siku kutokana na msongamano wa magari katika Jii la Dar es Salaam.
Kamati hiyo ilipendekeza kuwa ili kuondokana na tatizo hilo, mipango yote iliyopendekezwa na wataalam na watafiti mbalimbali itekelezwe.
Aliitaja mipango hiyo kuwa ni kujenga na kuimarisha barabara za michepuo, uboreshaji wa usafiri wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), kujenga barabara za juu, usafiri wa boti kutoka Bagamoyo mpaka Feri, usafiri wa reli jijini na usafiri wa DART.
WATUMISHI WAKOPESHWE MAGARI
Wakati huo huo, Kamati ya Miundombinu impendekeza kubadili sera ili serikali ibakie na mzigo wa kugharimia magari ya huduma badala ya kugharimia magari yanayotumiwa na maofisa kwenda na kurudi kazini. Akisoma maoni ya kamati hiyo, Kilango alisema katika nchi zinazoendelea watumishi wa serikali wanatumia magari yao na usafiri wa umma kwenda na kurudi kazini.
“Ujenzi wa miradi ya barabara unahitaji fedha nyingi, kwa kuwa serikali haina fedha za kutosha kamati inashauri iangalie maeneo ambayo inaweza kubana matumizi kwa mfano, kupunguza matumizi ya magari yasiyo ya lazima,” alisema Kilango ambaye ni pia ni Mbunge wa Same Mashariki.
Alisema jambo hilo lifanyike kwa kuhakikisha kuwa maofisa wa serikali wanaostahili kutumia magari ya serikali wanakopeshwa magari na kupewa posho maalum kwa ajili ya kununulia mafuta na kuendeshea magari hayo badala ya kutumia magari ya serikali.
Alisema kamati hiyo ilifanya utafiti na kubaini kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 kiasi cha Sh. 74,637,915,279 zimepangwa kutumika kwa ajili ya kununua mafuta, oil na vilainishi pamoja na kufanya matengenezo ya magari ya serikali.
Aidha, alisema kutokana na aina ya magari yanayotumika na maofisa wengi wa serikali ya Toyota Land Cruiser VX kuwa ya gharama kubwa, serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua magari hayo ikiwa ni wastani wa Sh. 260,000,000 kwa gari moja ambalo hutumiwa na ofisa mmoja tu.
UPINZANI: MASHANGINGI YAPIGWE MNADA
Kwa upande wake, kambi ya upinzani ikiwasilisha bajeti yake mbadala, ilitaka magari ya kifahari yanayotumiwa na viongozi na watumishi wa umma yauzwe kwa mnada ndani ya miezi sita na viongozi hao wakopeshwe magari kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao mbalimbali.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Ujenzi, Salvatory Machemli, aliitaka serikali kuandaa utaratibu utakaowawezesha viongozi na watendaji kupata usafiri wa gharama nafuu badala ya utaratibu uliopo.
SENDEKA ALALAMIKIA FEDHA ZA BARABARA
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, amelalamikia mgawanyo wa fedha za ujenzi wa barabara akisema serikali inayoelekea kufa, kila mmoja hunyofoa kitu chake.
“Siku zote serikali iliyoanza safari ya kifo ni kila mmoja kunyofoa kitu chake,” alisema Ole Sendeka wakati alipoomba mwongozo wa Mwenyekiti bungeni jana.
Mbunge huyo alitaka bajeti ya Wizara ya Ujenzi, ifumuliwe kwa kuwa haikuzingatia usawa, bali imejaa upendeleo wa maeneo yanayotoka viongozi.
Akizungumza mara baada ya kupewa ruhusa na Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene, alisema upendeleo uliopo katika miradi ya barabara ni dalili mbaya kwa serikali. Alisema kuna barabara kadhaa zikiwemo za Mkoa wa Kilimanjaro, na kuzitaja barabara ya Sadala-Masama iliyotengewa fedha kwa ujenzi wa kiwango cha lami, barabara ya Kibosho Shine-Kwa Raphael, Rau-Madukani hadi Mawela Uru, Kwa Nduoni na nyingine ni ile ya Tarakea Rongai hadi Kamwanga.
“Huu ni mgawanyo wa rasilimali usio na uwiano sawa, inafika hali hii kila mtu anataka kunyofoa kipande chake, serikali inatakiwa kuwa makini,” alisema.
Alisema cha kusikitisha ni kwamba katika ujenzi wa barabara ya Kia kwenda Mererani ilitengewa fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2010/2011 haikutekelezwa na pia haimo katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi iliyosomwa jana bungeni. Akijibu mwongozo huo, Simbachawene alisema kuwa jambo hilo ni zito hivyo mwongozo utatolewa leo.

No comments:

Post a Comment