KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Saturday, 6 August 2011

Chadema kuamua hatima ya Shibuda, madiwani leo

 
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda
Mussa Juma, Dodoma
KAMATI Kuu ya Chadema leo inatarajia kutoa hatima ya Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda na madiwani sita wa chama hicho wa Jimbo la Arusha baada ya baada ya kujieleza kwenye kikao hicho.

Shibuda anatuhumiwa kuisaliti kambi ya upinzani bungeni kwa kuteteta suala la wabunge kupata posho kinyume na msimamo wa sera zao. kwa upande wao, madiwani hao wamegoma kuomba radhi uongozi wa chama hicho na pia wamekataa kuukatana muafaka waliosaini baina yao na madiwani wa CCM.

Habari kutoka ndani ya Chadema zimebainisha kuwa madiwani hao wa Arusha waliandikiwa barua za kuitwa mjini hapa leo na walitarajiwa kuwasili jana.

"Tayari wameandikiwa barua waje, kwani kamati kuu ilikuwa bado haijawahoji na kufikia uamuzi wake. Kamati iliyowahoji awali iliundwa na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa," alisema kiongozi mmoja wa chama hicho ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Dk Slaa alithibitisha kufanyika kwa kikao cha KamatiKkuu leo mjini hapa lakini hakuwa tayari kutaja ajenga.

Madiwani watakaohojiwa ni Estomih Mallah wa Kimandolu ambaye katika muafaka huo alichaguliwa kuwa Naibu Meya wa Jiji la Arusha. wengine ni Diwani wa Elerai, John Bayo ambaye alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Baraza la Madiwani Manispaa ya Arusha.

Wengine ni Reuben Ngoi wa Kata ya Themi, Charles Mpanda wa Kaloleni, Crispian Tarimo wa Kata ya Sekei na Rehema Mohamed wa Viti maalumu.

Kuitwa Dodoma kwa madiwani hao kumekuja siku chache baada ya Baraza la Uongozi Chadema Mkoa wa Arusha kwamba kupendekeza kuwa wafukuzwe katika chama hicho.

Habari kutoka Chadema zinasema huenda leo chama hicho kikaunda kamati ndogo nyingine ya kikatiba ili kuchunguza migogoro hiyo na kutoa mapendekezo ya mwisho. Hata hivyo, madiwani hao wamekuwa wakipinga uamuzi huo kwa madai kwamba walisaini muafaka kwa manufaa ya wananchi wa Arusha hasa baada ya kukomaa kwa mgogoro katika halmashauri ya jiji hilo.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba alisema jana kwa simu kutoka Arusha kwamba wamependekeza kuwafukuza madiwani hao kutokana na kudharau maelekezo ya chama na pia kusaini muafaka bila ridhaa ya chama hicho.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ndiye aliyekuwa wa kwanza kupinga muafaka huo akisema kwamba hauna maslahi kwa wananchi wa Arusha na wala ya watu ambao ndugu zao walifariki na wengine kujeruhiwa katika harakati za kudai uchaguzi wa haki wa meya wa jijini humo.

"Kwanza kuna kesi mahakamani inayohusu viongozi wa kitaifa na wabunge na chanzo ni kutetea haki na kufuata taratibu katika uchaguzi. Watu walifariki bado hatima yao na kulikuwa na mazungumzo ya muafaka kwa kushirikisha viongozi wa kitaifa wa Chadema na serikali," alisema Lema.

No comments:

Post a Comment