Sunday, 07 August 2011 |
MGAWANYIKO wa makundi ya kisiasa ndani ya CCM na utendaji wa Serikali yake unaotia shaka vimechangia kwa kiasi kikubwa kumpandisha chati Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, hadi kuwa tishio kwa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Matokeo ya utafiti uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya Utafiti ya Synovate ni ishara tosha kwamba, kama hali itaendelea hivi ilivyo ndani ya CCM, utawala utaenda kambi ya upinzani na Dk Slaa atakuwa tishio kwa wagombea wote wa urais katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015 kama atagombea. Wachambuzi wa mambo ya siasa na wasomi nchini, wanayaona matokeo ya utafiti huo kuwa yanamfanya Dk Slaa, ambaye alikuwa mgombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita kuwa mwiba mkali kwa CCM katika uchaguzi mkuu ujao, kama chama hicho tawala hakuyapatia ufumbuzi mambo yanayokifanya kipoteze mvuto kwa wananchi. Matokeo ya utafiti huo si tu kwamba yamweka juu Dk Slaa bali yanaifanya CCM iamke na kuweka mikakati dhabiti kukabiliana na changamoto inazohatarisha nafasi ya chama hicho kuendelea kuongoza nchi. Ni dhahiri kuwa Dk Slaa amepata ushindi huo kutokana mambo makubwa matatu ambayo ni, kwa sasa ukimwondoa Rais Kikwete, CCM haina mgombea tishio. Pili, utafiti huu unafanyika wakati kuna mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM unaochochewa na makundi hasimu ya wanasiasa yanayoviziana na kumalizana, tofauti na miaka iliyopita. Tatu, hivi sasa CCM inakabiliwa na changamoto nyingi zinazoifanya ipoteze mvuto. Baadhi ya changamoto hizo ni ugumu wa maisha unaotokana na mfumuko wa bei na kuanguka kwa uchumi, matatizo ya umeme, mgogoro wa bei ya mafuta, kashfa mbalimbali za kifisadi zilizoibuka na zinazoendelea kuibuka na utendaji mbovu wa Serikali uliojionyesha dhahiri katika bajeti ya mwaka huu. Nape Mnauye Alipoulizwa jana na gazeti hili kuhusu mtazamo wake juu ya matokeo ya utafiti huo kwa uchaguzi wa 2015, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, alisema hawezi kutoa maoni yake kwa kuwa bado hajasoma ripoti ya utafiti huo. Kwa mujibu wa Nape, utafiti unahusisha mambo mengi, ikiwa ni pamoja na namna ulivyofanywa, watu walioulizwa, walipatikana vipi na ulilenga watu wa kada gani. “Mimi sijapata ripoti hiyo na nimeagiza ofisi yangu waitafute ripoti hiyo, kwa sasa siwezi kutoa maoni yeyote,” alisema Nape. Mtazamo wa utafiti Utafiti uliofanywa na Synovate kuhusu nafasi ya urais na ripoti kutolewa Oktoba 10, mwaka jana kabla ya uchaguzi mkuu, ulionyesha kuwa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipata asilimia 61 ya kura zote, akifuatiwa na Dk Slaa wa Chadema ambaye alipata asilimia 16 na nafasi ya tatu ikashikwa na Ibrahim Lipumba wa CUF aliyepata asilimia tano. Matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita Rais Kikwete aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 61 huku, Dk Slaa akiwa wa pili kwa kupata asilimia 26. Lakini katika utafiti huu wa sasa wa taasisi hiyo unaonyesha kuwa kama Rais Kikwete angeamua kujiweka kando na ukaitishwa uchaguzi mkuu sasa, Dk Slaa angeibuka mshindi wa nafasi hiyo. Nafasi ya wapinzani Ripoti ya Synovate iliyotolewa jijini Dar es Salaam wiki hii inabainisha kuwa, kwa ujumla CCM katika uchaguzi huo ingeanguka na nafasi yake hiyo kuchukuliwa na wapinzani wakiongozwa na Chadema. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo inawapa wapinzani fursa ya ushindi kwa mara ya kwanza, wagombea kutoka vyama vya upinzani wana uwezo wa kupata ushindi wa jumla wa asilimia 67 iwapo uchaguzi ungefanyika sasa. Dk Slaa anaongoza katika kundi la wapinzani kwa kupata asilimia 42, akifuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, asilimia 14 huku Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe akipata asilimia tisa. Kutokana na utafiti huo ni wazi kuwa hali kama itaendelea kama ilivyo hivi sasa ni Dk Slaa anazidi kupanda chati huku wapinzani wake wakizidi kushuka katika medani ya siasa nchini. Dk Mkumbo Akichambua matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kada wa Chadema, Dk Kitila Mkumbo, alisema utafiti huo ni ishara njema kwa Dk Slaa na onyo kwa CCM kwani haijawahi kutokea kiongozi wa upinzani kuongoza kura za maoni. Hata hivyo, alisema licha ya utafiti huo kutoa picha nzuri kwa Chadema, bado una upungufu mwingi. Dk Mkumbo alisema kufanya utafiti kama huo wakati watu wametoka kwenye uchaguzi na kuacha mambo ya msingi kama utendaji wa Serikali na kukubalika kwa vyama ni sawa na kuhamisha hisa za watu na kuzima ajenda za maana. Kwa mujibu wa Dk Mkumbo, Synovate wangepaswa kufanya utafiti unaohusu utendaji wa Rais Jakaya Kikwete hadi sasa na kukubalika kwa vyama vya upinzani, si kutafiti nani atakuwa rais ikiwa rais aliyepo madarakani angekaa kando. “Mimi kama mwanataaluma nadhani utafiti huu una upungufu wa msingi. Huwezi kufanya utafiti wa kutaka maoni kwa kumtoa mtu ambaye alishinda katika uchaguzi na unamuacha aliyemfuatia kwa mbali akipambana na wengine ambao ni dhaifu,” alisema Dk Mkumbo. Mchungaji Mwamalenga Naye Mchungaji William Mwamalanga wa Kanisa la Kipentekoste, alipinga matokeo hayo akisema utafiti huo umekuja haraka sana. Aliongeza kuwa muda ulitumika kufanya utafiti huo ni mfupi sana, na yeye kama mtaalamu wa masuala ya utafiti, mambo nyeti kama Siasa na Uchumi si ya kufanyiwa utafiti kwa muda mfupi. Mchungaji Mwamalanga pia alikosoa utafiti huo kwa kusema kuwa umekuja wakati nchi ikiwa kwenye matatizo mengi ya kiuchumi na hasa suala la mgao wa umeme, bei ya mafuta na ongezeko la ugumu wa maisha. Kuhusu wana CCM walioshiriki katika utafiti huo na kusema kuwa Dk Slaa anafaa kuwa rais kama uchaguzi utafanyika hivi sasa, Mchungaji huyo alisema kuwa wana CCM hao ni ndumila kuwili. Mallya wa TGNP Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya, alisema ni vema tafiti zinazofanywa hivi sasa zikalenga fursa zilizopo kwa maslahi ya taifa. Akifafanua Mallya alisema wakati huu kuna mambo kama mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya ambayo yangepaswa kutiliwa mkazo na si masuala ya uchaguzi kwani nchi ndio kwanza imetoka kwenye uchaguzi. “Mimi nadhani hata nyie mnaweza kujiuliza kwa nini utafiti huo uje waka huu? Kuna mambo ya msingi ambayo tukitumia fursa hii yanaweza kuwa na manufaa kwa nchi yetu,” alisema na kuongeza: “Ni vema kama mtu anafanya utafiti akaelezea mambo ya msingi, kwani kuja na mambo ambayo si ya msingi sana hivi sasa, kutafanya nafasi zilizopo hivi sasa kupotea na hivyo kuja kujuta baadaye.” Katika kupata maoni juu ya mtu ambaye wangependa awe rais waliuliza: “Mbali na Rais Kiwete, ni mtu gani ungeweza kumchagua kuwa rais iwapo atakuwa miongoni mwa wagombea?” Kutoka CCM, kiongozi anayeonekana kukubalika zaidi ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amepata asilimia 12, akiwa nyuma ya Dk Slaa na Profesa Lipumba. Hali hiyo inathibitisha kwamba iwapo uchaguzi ungefanyika hivi sasa, Pinda angeambulia nafasi ya tatu. Katika utafiti wake huo uliofanywa kati ya Mei 2 hadi 19, mwaka huu, jumla ya watu 1,994 walihojiwa. Mbali na Dk Slaa, utafiti huo unatoa pia nafasi kubwa kwa wanasiasa wengine wa upinzani kung'ara katika uchaguzi mkuu ujao, akiwamo Profesa Lipumba na Zitto. Wanasiasa wengine wanne wanaofuatia kwa umaarufu na asilimia walizopata kwenye mabano ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (4), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samweli Sitta (2) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (2). Kada wa CCM ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema kilichowaponza baadhi ya vigogo wao, akiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta (2), Naibu Waziri wa Ujenzi,Dk Harrison Mwakyembe (1), Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya (1) na Spika wa Bunge Anne Makinda (1) ni kushiriki katika siasa za makundi. Alitoa mfano wa Waziri Mkuu Pinda na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, walipata kura nyingi kunaonyesha kuwa hawajajiingiza katika siasa za makundi ndani ya chama hicho kikongwe nchini. |
KARIBUNI
Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.
Saturday, 6 August 2011
Slaa tishio CCM Uchaguzi 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment